Kwa kukazia uanzilishi mzuri wa chombo kile, akiteua mawaziri wawili vijana aliowaamini – Maalim Seif Shariff Hamad (Elimu) na Haji Mlinde (Waziri Ofisi ya Rais, Vikosi vya SMZ) waje bara kuzuru JKT waone shughuli zinavyoendeshwa na vijana. Nia ilikuwa wakirejea Visiwani wakaharakishe uanzishaji wa hiyo JKU kutoka ule mfumo wa kambi za vijana. 

Safari iliandaliwa, tulitoka Zanzibar Jumamosi tarehe 3/2/1979 kwa ndege hadi Dar es Salaam. Jumapili tarehe 4/2/1979 ujumbe ulikwenda Nachingwea. Jumatatu tarehe 5/2/1979 mawaziri hao walizuru kambi ya JKT Nachingwea. Jumanne tarehe 6/2/1979 walitembelea Farm 17 kambi ya JWTZ kuona mafunzo ya wakimbizi wa ZANU-PF na ZAPU-PF. Jumatano tarehe 7/2/1979 ujumbe ulirejea Dar es Slaam na siku ya Alhamisi tarehe 8/2/1979 ujumbe ulifika Fishing Unit JKT Mbweni, kisha wakatembelea Kikosi cha Ujenzi (Builders Brigade)Mikocheni na Kambi Kongwe ya Mgulani JKT. 

Huko Mgulani walitembelea viwanda vya viatu, makoroboi na Lumbering. Hatimaye waliona kiwanda cha samani cha Chang’ombe. Siku ya Ijumaa tarehe 9/2/1979 ndipo walipohitimisha ziara yao ile kwa kutembelea Ruvu JKT kuona mafunzo ya kijeshi, kilimo cha mpunga, ufugaji wa kuku na kiwanda cha kushona nguo. Ikumbukwe hapa kuwa Kambi ya Ruvu ndiko Mzee Jumbe alipohenya urikruti wake katika Operation KAZI B – mwaka 1968. 

Baada ya ziara hiyo, tuliporudi Zanzibar ndipo baada ya mawaziri hawa kumwelezea Rais ripoti ya ziara yao kambi za JKT Serikali ya Mpainduzi Zanzibar kwa haraka wakatunga sheria ya JKU iitwayo Sheria No. 5 ya mwaka 1979. (Tazama Government Notice ya SMZ katika Supplement No. 4 ya tarehe 23/6/1979). Baada tu ya sheria ile kambi za vijana wa ASP sasa zikawa kambi za JKU. Maalim Seif Shariff Hamadi alisaidia sana akiwa Waziri wa Elimu, vijana wasomi kuingia Kambi za JKU. 

Nimeelezea hayo kuonesha Mzee Jumbe alivyowaandaa wasomi mawaziri vijana kama Maalim Seif kwa kuongoza Zanzibar kisasa ili kuondokana na mawazo mgando ya waasisi wa Mapinduzi. 

Hapo sasa nataka kuonesha namna Jumbe alivyomjenga Maalim ili kuondoa ile hali ya Upemba na Uunguja na kujaribu kufuta ile dhana ya wasomi vs MBM waasisi. Kulikuwa na hali mimi naiita ya kutokujiamini (inferiority complex) kwa wana MBM, hivyo walitumia ubabe zaidi kuliko hekima katika utawala kule Visiwani. Mzee Jumbe alitaka kubadili muonekano ule wa ubabe wa Baraza la Mapunduzi kwa kuingiza damu changa yenye upeo wa kisasa (modernize the rule of law) kule Visiwani. 

Mwandishi mmoja katika makala yake katika gazeti la ‘Raia Tanzania’, Toleo Na. 0544 la Alhamisi tarehe 7 Januari, 2016 Uk. 14 anaandika hivi nanukuu, “… kuna ushahidi mwingine tena wa kutosha kuelezea namna Rais wa Zanzibar, Mzee Jumbe, alivyowaona waasisi wa Mapinduzi kana kwamba hawakuwa na ELIMU ya kutosha na siyo WENYE UPEO katika mambo ya uhai wa kisiasa na utawala. 

Basi mzee huyu, Rais wa Awamu ya Il kule Visiwani akaja na fikra mpya ili kufanya Zanzibar itanue wigo wa demokrasia, iwe nchi yenye kufuata na kuheshimu misingi ya utawala bora, kudumisha uhuru wa raia kwa kutambua mipaka ya haki za binadamu, ikijumuishwa na kupatikana kwa KATIBA YA ZANZIBAR ikiwamo na kuundwa chombo cha KUTUNGA SHERIA yaani kuunda sasa Baraza la Wawakilishi, ndiyo kusema anafutilia mbali lile Baraza la Mapinduzi sivyo? Aliona BMZ lisingelimsaidia kimawazo. Kwa kulipunguzia nguvu na makali lile BMZ la waasisi, Mzee Jumbe alipalilia vijana wasomi kuandaa mabadiliko aliyoyatarajia kwa kule Visiwani. 

Hapo ndipo kulipoanzishwa hali ya sintofahamu maana kwa kuanzisha BARAZA LA WAWAKILISHI ni sawa na kuwatia usongo wazee waasisi wa Mapinduzi. Kumbe Mapinduzi matukufu yale ya Januari 12, 1964 yalikuwa kumkomboa mnyonge kutoka mikononi mwa udhalimu wa Serikali kandamizi ya usultan. 

Kwa mantiki hiyo ndipo Mzee Karume baada tu ya Mapinduzi alitoa tamko (DECREE) ili kukwepa fitina za uchaguzi usiokuwa wa haki huko nyuma na kusema katika tamko lile la Serikali. “Hakutakuwa na uchaguzi wowote Zanzibar hadi itakapopita miaka 50 tangu tarehe ya tamko hili la Serikali ya Mapinduzi kupitishwa chini ya sheria ya Mapinduzi”. Sheria Na. 6 ya Februari 25, 1964. 

Kule visiwani tamko hili lilikuwa la pili kwa wananchi wale. Mnakumbuka kuwa enzi za sultani Serikali ya Chama cha Waarabu cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Waziri Mkuu Mohamed Shamte ilitoa tamko lililoitwa “THE NATIONALITY DECREE” lililofuta ukabila na lilimtaka kila raia wa sultani ajiandikishe kama Mzanzibari, kamwe wasijiandikishe kama Waarabu au Waafrika bali wajiite kwa umoja wao AFRO-ARABS- WAZANZIBARI. Sheria ile inajulikana kama Sheria No. 10 ya mwaka 1954. Kizazi cha leo naona hawajaisikia wala kuijua ‘Decree’ hii. 

Hapo ndipo mie naanza kuchambua usintofahamu wa Wazanzibari. ‘Decree’ ya Waarabu haisemwi wala kulalamikiwa na mtu, hii ‘decree’ ya Baraza la Mapinduzi la Waafrika inalalamikiwa! Hapo ndipo naomba wasomi wanifafanulie tofauti za ‘Decrees’ hizo mbili za kule visiwani. 

Mathlani kwa utaratibu wa Serikali ya Waarabu Zanzibar (Nationalist Party Government)  ya Shamte, wapo Wazanzibari waliopinga ubaguzi wa aina yoyote ile miongoni mwa Wazanzibari. Mfano Mzee Abdulrahman Babu alitoka ZNP kwa kupinga ubaguzi wa kimbari – Uarabu na Uafrika. Hata wakati Profesa Mohamed Babu aliporejea kutoka nje mwaka ule 1990 hivi, wengi walitarajia Mzee Babu angejiunga na chama cha upinzani kimojawapo. 

Huyu Mzee alikuwa mmoja wa waasisi wa chama kilichoitwa Zanzibar United Front (ZUF) wakati akiwa London. Chama hicho ndicho kilichoibua wazo la Katiba ya hiki chama cha CUF cha Maalim Seif. Cha ajabu, aliporejea akaundiwa mizengwe mpaka akashindwa kujiunga na CUF badala yake akaingia NCCR-Mageuzi ya Mrema enzi zile. 

Kumbe Mzee Babu kule Visiwani Waarabu wanamjua kwa msimamo wake wa kupinga ubaguzi wa kitaifa (racism). Yeye na baadhi ya Waarabu kama akina Ahmed Mugheri walipinga utabaka wa rangi, Babu alisimamia umoja wa Wazanzibari, alitaka chama chake kisiwe na ubaguzi wa rangi au ukanda yaani Upemba na Uunguja ilimradi kipate uwakilishi wa kitaifa, hapo ndipo akaitwa Mkomunisti, hafai kwa dini ya nchi ile, hivyo CUF walifikiria kuwa huenda angerudisha tena mawazo ya kufuta Upemba wala Uunguja, jambo ambalo Wapemba hawalitaki wala kusikia. 

Naye Mzee Ahmed Mugheri aliwaambia Waarabu wenzake kuwa Waarabu na Waafrika sasa waweze kuoana ili kuchanganya damu kupata ule UAFRO-Arab alioutaka Shamte katika ile “decree” ya utaifa-Uzanzibari. Basi kuonesha chuki zao kwa maoni namna ile, Babu akakataliwa kujiunga na CUF wakati Mzee Mugheri alipigwa mkutanoni katika kikao cha ZNP na kupelekwa hospitalini Mnazi Mmoja (wakati ule ikiitwa Hospitali Kuu ya Karimjee) kuugulia. 

Akiwa huko hospitalini Mwarabu mwenzie mwenye itikadi kali akiitwa Mohamed Hamoud alikwenda kumjulia hali na pale pale hospitalini, akiwa kitandani huyo Hamoud akampiga jisu na kumuua. Kosa kubwa la Mzee Mugheri ni kule kutoa wazo tu kuwa sisi Waarabu sasa tujitambue Afrika siyo kwetu jamani, basi tujione tu wageni Afrika. Nchi hii ya hawa Waafrika. Mzee Hamoud mwenye msimamo mkali alimuua Mugheri hapo hapo hospitalini. 

Kwa mitazamo namna hiyo, suluhu ya kweli kimawazo inaweza kweli kupatikana? Kwa nini Wazanzibari wanakaa katika vikundi vikundi kuchokonoana na kulaumiana? Wote kule ni Wazanzibari, hakuna Wayao wala Wamakonde ingawa Mzee Moyo ni Mngoni wa Songea ameshakuwa Mzanzibari pyua. 

Mbona Mngoni mwenzake Mzee Mfaranyaki aliyeshiriki Mapinduzi kule Zanzibar siku zile za mwanzo wa Mapinduzi Serikali ya Mzee Abeid Karume ikamfukuza kule Visiwani na kumrudisha Songea maana yake hakufaa kuishi kule akiwa na ufinyu wa mawazo ya kisasi (very radical) Hamisi Darwesh, Myao wa Tunduru, mbona hakufukuzwa amefia kule Unguja kama Mzanzibari. 

Hii inaonekana Uzanzibari ni hali ya wananchi kupokea maadili, mila, desturi na maisha ya pale unapoishi, vivyo hivyo Waarabu ‘radicals’ hawafai kuishi kule Zanzibar. Wajione wao ni Wazanzibari wala si wa Omani waliohamia kibiashara kule Visiwani. Hayo yakitoweka sina wasiwasi Wazanzibari wataishi kwa umoja na utulivu. 

 

>>ITAENDELEA

1479 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!