Mwathirika wa ajali huhitaji ahudumiwe haraka, tena kwa muda mfupi, huku mipango ikiwa inafanywa hadi atakapotokea daktari au atakapopelekwa zahanati ama hospitali kwa tiba inayostahili…

 

Kuumwa na Vidudu

Miumo ya vidudu huwapa watu wengine madhara makubwa zaidi ya wengine. Mwiba wa nyuki (bee), dondora (steinbuck), nyigu (wasp/hornet) na miiba ya wadudu wengine wa aina hiyo, kwa kawaida, huwa inaonekana wazi mahali ilipodungwa mwilini. Hivyo, mtu akiumwa na wadudu hao kamwe usitumie vidole vyako kuminya kuutoa mwiba huo. Kuminya katika sehemu yenye mwiba wa nyuki kutaifanya sumu iliyohifadhiwa ndani ya mwiba huo kuingia katika mkondo wa damu. Mtu aliyepata shida hiyo anaweza akapata nafuu kwa kumeza vidonge vya dawa za kupunguza maumivu, kama itakavyoshauriwa na daktari baada ya kumpeleka hospitali. 

 

Kuungua na Kubabuka

Kuna aina nne za kuungua: (i) kwa mvuke (steam) au maji ya moto (boiling water), (ii) kubabuka ngozi kwa tindikali (acid) ama dawa kali (chemicals), (iii) kuungua kwa kaa la moto, na (iv) kuchomwa na umeme (flash) katika ngozi ya mwili. Ni mshtuko wa shock ama maambukizo mengine yatakayofuatia ndiyo yanayoleta balaa zaidi ya kuungua kwenyewe. Pakaza kwenye jeraha mafuta maalum ya huduma ya kwanza (first aid ointment) kwa kutumia kitambaa. 

Usipake kwenye jeraha la kuungua mafuta yanayopatikana kwa urahisi, kwa mfano siagi, mafuta ya kupikia ama siki (vinegar). Kama majeraha ni makubwa, mvue mgonjwa nguo isipokuwa kama zimeshikamana na ngozi iliyoungua. Shock ya mtu aliyeungua humfanya asikie kiu na baridi. Midomo yake huwa ya rangi ya kijivu ama zambarau kutokana na upungufu wa damu na oxygen utakaokuwapo mwilini mwake. Funika majeraha kwa kitambaa safi ama shashi (gauze). Kamwe usitumie pamba na usitoe kitu chochote kilichonasa kwenye jeraha. Mwachie kazi hiyo daktari. 

Kutokana na ngozi ya mwili kubabuliwa (skin bruising) na dawa kali (chemical burns), mathalan, maji ya betri na dawa nyingine kali, lazima mara moja ioshwe kwa maji mengi, ili kuzuia dawa hiyo isiendelee kuchimba ngozini. Majeraha yanayosababishwa na tindikali yabidi yaoshwe kwa siki  iliyopozwa makali kwa maji safi, na baadaye yasafishwe tena kwa maji. Sehemu zinazotokea kufaganzi  kwa kupigwa na baridi, zikandwe kwa maji ya uvuguvugu. Lakini usisugue sehemu iliyokufa ganzi. 

 

Malengelenge

Vipele au vimbe zenye majimaji ndani yake (blisters) yabidi zioshwe vyema kwa maji na sabuni. Halafu vitumbuliwe kwa sindano ambayo ncha yake imechomwa kwenye mwali wa moto (na kupoa) kuua vijidudu vya maambukizo ya maradhi. Usaha au majimaji yaliyo ndani yake yakamuliwe kwa uangalifu, kupitia penye kitundu kilichotobolewa. Sehemu hiyo ifunikwe na kufungwa kwa plasta ama kitambaa safi.

 

Kuzirai

Kuzirai au unyong’onyevu mkubwa wa mwili (fainting) mara nyingi hutokana na mtu kukosa kwa muda fulani damu kufika katika ubongo. Huduma ya kwanza lazima itolewe akiwa amekalishwa kitako huku ameshikiliwa au amelazwa chali huku kichwa chake kikiwa kimenyooka sawa na kiwiliwili chake. Kama kitambaa kilichomwagiwa manukato ya spiriti kali (aromatic spirits of ammonia) kitawekwa karibu na pua ya aliyezirai, mara nyingi humrejeshea haraka mwnenendo wa damu katiika ubongo. Akirudiwa na fahamu anaweza akapewa chai, kahawa ama maji ya baridi.

 

Kumeza Kitu Kigumu

Madaktari wanatushauri kuwa kama mtu amekwamwa na kitu ndani ya koo la hewa au la chakula, apinduliwe kichwa chini miguu juu, kisha apigwe konde au kofi zito mgongoni. Mara nyingi kufanya hivyo husaidia kukifanya kilichokwama kooni kutokea puani ama kinywani. 

Kama mtu aliyekwamwa na kitu anashindwa kupumua, inabidi afanyiwe huduma ya kwanza ili kuiwezesha hewa iingie na kutoka vyema mapafuni mwake. Mara nyingi punde huja akapata nafuu. Anapopelekwa hospitali itabidi afanyiwe uchunguzi wa muda wa saa nyingi, ama hata wa siku kadhaa. 

Kama kitu hicho kigumu kimeingia hadi tumboni, huwa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Na usimpe mtu huyo dawa ya kuharisha (laxative) ya aina yoyote. Vitu vingi vigumu vikimezwa na kufika ndani ya mfuko wa tumbo (stomach), vitakuja kutoka vyenyewe na kinyesi. Lakini, mathalan, mtu akimeza sindano au kitu chenye ncha iliyochongoka au yenye makali, yafaa apelekwe hospitali haraka. 

 

>>ITAENDELEA

9665 Total Views 5 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!