Maneno ya Kiswahili yaliyotumika kwenye wimbo wa ‘Spirit’ wa Beyonce Knowles uliotoka hivi karibuni yamegusa hisia za Watanzania wengi.

Si jambo geni kuyasikia maneno ya Kiswahili yakitumiwa na wasanii maarufu katika nyimbo zao, alikwishawahi kuyatumia Michael Jackson katika wimbo wake wa ‘Liberian Girl’.

Hata Nas katika wimbo wa ‘Distant Relatives’ alioshirikiana na Damian Marley, mtoto wa Bob Marley wameyatumia maneno ya Kiswahili.

Mbali na wasanii hao kukitambua Kiswahili na kuamua kuyatumia maneno yake katika nyimbo zao, Rapa Nipsey Hussle naye amekitaja Kiswahili katika wimbo wake.

Ikiwa ni miezi takriban minne imepita tangu rapa huyu alipopigwa risasi na kufariki dunia akiwa mbele ya duka lake la The Marathon lililopo jijini Los Angeles, Marekani kuna mengi yameibuka ambayo wengi walikuwa hawayajui kumhusu mwanamuziki huyo.

Kwa wasio mashabiki wa muziki wa kufoka maarufu kama Hip Hop, jina la Nipsey Hussle linaweza kuwa geni masikioni mwao lakini anatajwa kuwa mtu aliyeacha heshima na jina kubwa katika soko la burudani nchini Marekani.

Mpaka mauti yanamkuta Machi 31, mwaka huu, Nipsey Hussle alikuwa kwenye kilele cha mafanikio ya albamu yake ya Victory Lap aliyoiachia Februari 16, mwaka jana.

Ni albamu inayotajwa kuleta mapinduzi katika mauzo kuliko kazi zake zote za muziki alizozifanya kwa kipindi chote cha miaka 13 alichokaa kwenye soko la burudani.

Nipsey Hussle mwenye asili ya Afrika, baba yake alihamia nchini Marekani akitokea nchi ya Eritrea iliyoko upande wa kaskazini mwa nchi za Afrika Mashariki.

Naye amekitumia Kiswahili katika wimbo wake wa ‘Keys to the City’ ulioko kwenye albamu hiyo.

Kwenye wimbo huo aliomshirikisha msanii mwenzake anayefahamika kwa jina la TeeFlii, anasikika katika moja ya mistari ya wimbo huo akisema anamiliki mwanamke wa daraja la juu (mrembo), hivyo wanawake wengine akitaka kuongea nao atatumia Kiswahili.

Pengine lugha aliyoitumia inaonekana kujaa dharau dhidi ya lugha ya Kiswahili, kwa kuwa ni kama amejenga taswira kwamba Kiswahili ni lugha ya watu wa daraja la chini.

Mbali na mtazamo huo, ni muda wa wasanii wa Tanzania kuacha kulalamika kunyimwa au kukosa fursa katika soko la muziki wa kimataifa.

Kazi zenye ubunifu na ubora wa kiwango kinachokubalika kimataifa ndizo zitakazowafungulia njia kuelekea kwenye soko hilo.

Wasanii maarufu duniani kutumia lugha ya Kiswahili katika nyimbo zao ni ishara inayojitosheleza kwamba Kiswahili kinakubalika.

Wasanii wa Tanzania wanakwama wapi? Nawashauri kutumia mwanya huu kuuteka ulimwengu wa burudani kwani Kiswahili kimeonyesha mwanga tangu enzi za Michael Jackson lakini bado Watanzania tumelala.

350 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!