‘Hivi ndivyo mtu mashuhuri hufanya’.

Ni jina la wimbo wa msanii wa Nigeria, Abbey Elias, maarufu kama Skiibii Mayana ama Swaggerlee, unaomtambulisha katika soko la muziki nchini humo na pande za dunia kwa sasa.

Pamoja na umaarufu ambao umeanza kumvaa kijana huyu kwa sasa, mwaka 2015 hatasahaulika kwa mbinu yake ya kuusaka umaarufu kimuziki kwa kujitengenezea kifo na kutangazwa kwa mashabiki zake kwamba amefariki dunia.

Tukio hilo la kujitangazia kifo lilifanya mashabiki wa muziki wake na hata wale ambao si mashabiki wake kupatwa na simanzi huku wengine wakiomboleza.

Hata hivyo, baadaye ilikuja kubainika kwa mashabiki wa muziki wake kuwa tukio hilo alilitengeneza ili kupata umaarufu, jambo lililozua hasira kwa mashabiki hao huku wengine wakieleza kuwa hawawezi kukubali kupoteza utu wao kwa lengo la kujipatia umaarufu.

Tukio hilo halikumpa umaarufu kama alivyotarajia, badala yake lilimshusha kimuziki na kuongeza idadi ya wapinzani wa muziki wake kutoka katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Kwa sababu ya kuwa na dhamira kubwa ya kufanikiwa kimuziki, baada ya tukio hilo hakukata tamaa, akaongeza juhudi na kuzidi kuachia nyimbo ambazo watu wangezikubali na kukitambua kipaji chake.

Baada ya kujituma kwa nguvu mwaka jana, Skiibii alianza kukubalika kwa watu huku nyimbo zake za ‘Sensima’ na ‘Omaema’ zikianza kulitambulisha jina lake katika soko la muziki la Nigeria.

Skiibii ambaye alianza muziki tangu akiwa shule ya sekondari, mwaka 2014 alisainiwa katika ‘lebo’ ya muziki ya Five Star Music ambapo pamoja na kuwa katika ‘lebo’ hiyo nyimbo zake hazikuwa zikifanya vizuri.

Katika moja ya mahojiano aliyofanya hivi karibuni Skiibii alisema, aliamua kujitangazia kifo mwaka 2015 ili watu waweze kutambua kipaji chake na kuanza kufuatilia shughuli zake za muziki.

“Nilijitengenezea kifo kwa sababu watu hawakuwa wanaona uzuri wa kipaji changu, nilikuwa tayari kwa kila kitu, ninachohisi watu hawakujua nina uwezo gani, ngoma kali zinakuja,” amesema.

Tangu mwaka jana Skiibii anamiliki ‘lebo’ yake ya Grace Music ambayo aliianzisha baada ya kuachana na ‘lebo’ yake ya awali ya Five Star Music.

Anaeleza kuwa baada ya tukio la kujitengenezea kifo alishuka kimuziki lakini akajinyanyua mwenyewe na kwamba kupitia ‘lebo’ yake hiyo watu watarajie nyimbo nyingi nzuri kutoka kwake.

By Jamhuri