#Waandamana hadi Ubalozi wa Tanzania mjini Moroni

#Ufaransa, Ulaya, Uarabuni maelfu wasaini ‘petisheni’

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Mamia ya wananchi ndani na nje ya Muungano wa Visiwa vya Comoro wamejitokeza kushinikiza kuachiwa huru kwa aliyekuwa Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi.

Sambi yumo kizuizini kwa miaka mitatu sasa kwa amri ya Rais wa Comoro, Azali Assoumani, kwa sababu za kisiasa.

Habari kutoka makao makuu ya Visiwa vya Comoro, Moroni, zimesema askari walilazimika kutawanya makundi ya watu walioshika mabango nje ya Ubalozi wa Tanzania uliopo Mtaa wa Oasis, wakiomba Tanzania iingilie kati ili Sambi aachiwe huru.

Baadhi ya wananchi walioshiriki maandamano hayo walisema Sambi anateseka kizuizini bila sababu zozote za msingi, isipokuwa ni kutokana na udikteta wa Rais Assoumani anayemhofu kisiasa.

“Tunaomba Tanzania iingilie kati Sambi awe huru, tunajua Tanzania ni ndugu zetu, wametusaidia tangu tukidai uhuru na baadaye wametusaidia sana kuikomboa Anjouan na kurudisha amani nchini mwetu,” amesema mmoja wa waandamanaji hao.

Naye mwananchi mwingine amesema: “Tanzania ina nafasi nzuri ya kumaliza hili jambo. Tunamuomba Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) atusaidie, na yeye kama mama atakuwa na huruma – hatakubali kuona Sambi anateseka bila kosa.”

Haya yakiendelea nchini Comoro, huko Ufaransa, hadi mwishoni mwa wiki iliyopita Wacomoro takriban 2,000 walikuwa wameweka saini kwenye ‘petisheni’ wakitaka Rais Assoumani amwachie Sambi bila masharti.

Idadi ya watu wanaojitokeza kuweka saini zao imekuwa ikiongezeka Ufaransa na katika mataifa mengine ya Ulaya na Uarabuni.

Nchini Tanzania, Rais Assoumani aliwasili kwenye sherehe za miaka 60 ya Uhuru, akiwa miongoni mwa wageni walioalikwa na Rais Samia.

Gazeti la JAMHURI limefanya juhudi za kuzungumza na Mkurugenzi wa Mawasiliao Ikulu, Jaffar Haniu, kujua hatua iliyofikiwa kutokana na maombi ya Sambi kwa Rais Samia kuhusu kutolewa kizuizini, lakini Haniu hakupatikana mara moja kuelezea kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, mara kadhaa Rais Samia ameonekana akiteta na Rais Assoumani katika kile kinachotajwa kuwa ni kupata suluhu ya mgogoro huo.

Kutokana na maombi ya kuachiwa kwa Sambi, Rais Samia amechukua hatua kadhaa, ikiwamo kumtuma mwakilishi wake kwenye mgogoro huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwenda kuonana na Rais Assoumani. 

Rais Kikwete alikwenda huko Septemba, mwaka huu lakini tangu wakati huo Rais Assoumani hajakubali kumwachia huru Sambi.

Hatua ya Sambi kumuomba Rais Samia aingilie kati kumnusuru imetokana na Rais Assoumani kukaidi maombi ya Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), taasisi za kitaifa na kimataifa, na watu maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika.

Sambi amekuwa kizuizini ambako haruhusiwi kuonana na mke wala watoto wake kwa miaka mitatu sasa huku afya yake ikidorora.

Sehemu ya barua ya Rais mstaafu Sambi kwa Rais Samia inasomeka hivi: “Mheshimiwa Rais, familia na mawakili wangu wamejitahidi kufanya kila linalowezekana ili niwe huru kutoka kizuizini, lakini hadi sasa imeshindiikana. UN, AU kupitia Tume ya Haki za Binadamu – wote wametoa mwito niachiwe huru, lakini wamepuuzwa.

“Mheshimiwa, kwa miaka mitatu sasa nimetengwa na dunia. Kwa miaka yote hii nimezuiwa kuonana na mke wangu, watoto wangu wala mtu yeyoye awaye. Mtu pekee ninayeonana naye ni mtoto wa dada yangu. 

“Nimefungiwa kwenye selo ndogo nyumbani, ninanyimwa haki zote za msingi ambazo mtuhumiwa au mfungwa kama mimi ninastahili kuzipata kwa mujibu wa sheria za Comoro na kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.

“Afya yangu imedhoofu, nimenyimwa matibabu kwa muda wote huo licha ya kutakiwa kuonana na madaktari na kupewa matibabu. Hii ndiyo sababu kuu iliyonifanya mheshimiwa nikuandikie barua hii ili unisaidie niweze kutibiwa. 

“Daktari wangu Said Ali Petit, baada ya kunichunguza mara kadhaa ameshauri nipate vipimo na matibabu zaidi, lakini nimezuiwa kabisa. Hata jaji anayechunguza shauri langu Januari 2, 2020 alitoa kibali nipate matibabu, lakini uamuzi wake umepuuzwa. Mimi kama wengine nina haki za msingi za kibinadamu za kutibiwa, na zaidi kupata matibabu ya uhakika hata kama hayapatikani ndani ya nchi hii (Comoro).

“Mheshimiwa Rais, hali yangu ya sasa inanipa shaka mimi na jamaa zangu. Mimi kama rais mstaafu, kama raia, baba na mume, si haki kuzuiwa kizuizini na kunyimwa matibabu… kuwekwa kwangu kizuizini kumetokana na sababu za kisiasa, na mara zote nimesema sina kosa la kunifanya niwekwe jela. Kwa hiyo nakuomba ujadili suala langu la afya na mamlaka za nchi za Comoro ili nirejeshewe uhuru wangu.

“Mheshimiwa Rais, ili kupata ukweli juu ya mashitaka haya niliyofunguliwa, naambatanisha nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na barua niliyomwandikia Rais Azali Assoumani, na nyingine iliyoandikwa na marafiki zangu kuelezea mkasa ulionipata.”

Rais mstaafu Sambi pia ameiandikia AU barua, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Mahamat, akiomba Umoja huo usaidie kumrejeshea uhuru aliopokwa na Rais Assoumani.  

Anasema Mei 12, 2018, alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Rais Azali Assoumani kubadili Katiba ya Comoro ili kumwezesha kuendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2029. Hatua hiyo, anasema ilikuwa inafuta utaratibu wa kikatiba wa kuwa na urais wa mzunguko kwa kila kisiwa kwa miaka mitano.

Anasema Mei 18, 2018, alikamatwa na kuwekwa kizuizini nyumbani kwake kwa amri iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

Hatua hiyo anasema ni kinyume cha sheria, kwani mwenye mamlaka hayo ni jaji. Anasema licha ya mamlaka za dola kutambua kuwa kuwekwa kwake kizuizini ni kinyume cha sheria, ziliridhia pengine kwa hofu na hila.

Sambi anasema watu mbalimbali wamezuiwa kumtembelea, akitoa mfano kuzuiwa kwa Balozi wa Marekani nchini Comoro ambaye alitaka kufanya hivyo, lakini akazuiwa.

“Bila kufunguliwa kesi wala kusikilizwa, wala bila kuwapo ushahidi wa makosa ninayotuhumiwa kwayo, Serikali ya Comoro imeamua niwekwe kizuizini kwa muda usio na ukomo ikiwa nadhulumiwa haki zangu za kibinadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa,” anasema Rais mstaafu Sambi kwenye barua ambayo JAMHURI ina nakala yake.

Anasema Serikali ya Comoro imekataa katakata asitibiwe licha ya Serikali ya Tanzania kupitia kwa Rais Samia kukubali kugharimia matibabu yake.

Mwaka 2001 visiwa vitatu – Grande Comoro, Moheli na Anjouan – viliunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Comoro. 

Katiba hiyo, pamoja na mambo mengine, ilianzisha utaratibu wa mzunguko wa urais katika visiwa hivyo kwa miaka mitano, yaani The principal of rotating presidency between islands for five years. 

Utaratibu huo ulianza vizuri ambako kuanzia mwaka 2002 – 2006 alishika Rais Azali anayetoka Grande Comoro. 

Mwaka 2007 – 2011 urais ulishikwa na Rais Abdallah Mohammed Sambi kutoka Kisiwa cha Anjouan, na mwaka 2012 – 2016 Jamhuri ya Comoro iliongozwa na Rais Dk. Ikililou Dhoinine kutoka Kisiwa cha Moheli. 

Mwaka 2008 wakati Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Kisiwa cha Anjouan kilifanya jaribio la kujitenga na visiwa viwili vingine; jambo ambalo Umoja wa Afrika ulilikataa. 

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kibali cha Umoja wa Afrika lilikwenda kuzima jaribio hilo kwa kumwondoa kiongozi muasi Kanali Mohamed Bacar na kukirejesha kisiwa hicho kwenye utawala wa Jamhuri ya Comoro. Operesheni hiyo iliyojulikana kwa jina la Operesheni Comoro iliongozwa na Brigedia Jenerali Chacha Igoti.

Wacomoro wana uhusiano wa kinasaba na Watanzania, ikikadiriwa kuwa kati ya Wacomoro 10, mmoja ana ndugu, ama Zanzibar, au Tanzania Bara.

Mahitaji karibu yote muhimu kwa maisha ya Wacomoro yamekuwa yakitoka Tanzania, hali inayofanya kuwapo mwingiliano wa hali ya juu.

Sambi anatajwa kama mtu muhimu kwenye ujenzi wa Comoro moja, yenye mshikamano, akihakikisha amani na utulivu vinadumishwa. Anakubalika vizuri katika jumuiya ya kimataifa.

By Jamhuri