Wakati Simba Sports Club ikiendelea kuongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi mwishoni mwa wiki, timu za Toto African, Ruvu Shooting, Polisi Morogoro na Mgambo Shooting bado zinashindana mkiani zikionesha dalili za kuwa wasindikizaji msimu huu.

Simba imeshashinda mechi nne na kutoa sare dhidi ya mahasimu wake wakubwa wa soka nchini – Young Africans Sports Club – kwa kufungana bao 1-1 Jumatano iliyopita. Kabla ya hapo, ilikuwa imefunga mabao manane na kufungwa matatu huku Azam FC iliyoshinda mechi tatu ikitoa sare moja ikiwa na mabao saba ya kufunga na nyavu zake zikitikiswa mara mbili.


Nyuma ya timu hizo kulikuwa na JKT Oljoro ikiwa na pointi tisa kutokana na mechi tano ilizocheza na kushinda mbili, kutoa sare tatu na kufunga mabao saba, lakini ikiwa imefungwa manne ikifuatiwa na Coastal Union.


Yanga inayojaribu kulirejesha Kombe la ubingwa huo ililolipoteza msimu uliopita huku ikiadhiriwa mabao 5-0 na Simba siku ya mwisho, ilikuwa ikishika nafasi ya tano ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi tano. Ilishinda mechi mbili na kutoa sare mbili, ikapoteza moja, ikafunga mabao manane na kufungwa sita.


Kama ilivyokuwa kwa Yanga, Tanzania Prisons ilikuwa imefunga mabao sita na kufungwa matano, huku ikishika nafasi ya sita na kufuatiwa na Mtibwa Sugar iliyokuwa imecheza mechi nne.


Ikiwa na pointi saba sawa na Kagera Sugar, timu hiyo ilikuwa imeshinda mechi mbili, ikatoka sare moja na kupoteza moja, huku ikitumbukiza wavuni mabao sita na kufungwa matatu kama Simba na kuungana na Azam, kuwa ndizo zenye ngome ngumu zaidi msimu huu kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita.


Nafasi ya nane ilikuwa ikishikiliwa na Kagera Sugar iliyoshinda mechi mbili, ikatoka sare moja na kupoteza mbili, ikafunga matano, ikafungwa manne na nyuma yake ilikuwapo African Lyon, ambayo katika mechi zake tano ilikuwa imeshinda mbili, ikapoteza tatu, kufunga mabao matano na kufungwa tisa.


Nafasi ya 10 ilikuwa ikikamatwa na Ruvu JKT kwa kuwa na pointi sita, lakini ikitanguliwa na African Lyon inayofanana nayo karibu kwa kila kitu, lakini yenyewe ikiwa imefunga manne na hivyo kuzidiwa moja huku ikikung’utwa mabao 10 wakati pia imezidi moja mbele.


Toto African ipo katika nafasi ya 11 ikiwa imetoka sare mara na kufungwa moja, ikafunga mabao manne na kufungwa matano na kumiliki pointi nne mkononi. Inafuatiwa na Ruvu Shooting Stars yenye pointi tatu ilizozipata kwa kushinda mechi moja, ikafungwa nne na kutumbukiza wavuni mabao sita huku yenyewe ikifungwa 10.


Polisi Tanzania ya Morogoro ilikuwa imetoka sare mara mbili na kupoteza mechi tatu na hivyo kuwa na pointi mbili, zile ambazo zote ziliipatia bao moja na kufungwa manne. Timu hizi zote zinabebwa na JKT Mgambo iliyokuwa haijapata pointi hata moja. Ilikuwa imepoteza mechi zote tano huku ikifungwa mabao manane wakati yenyewe ilifunga mawili.


Kwa msimamo huo, timu wasindikizaji wa Ligi hiyo zimeanza kufahamika kuwa ni Toto African na Ruvu Shooting Stars zilizonusurika kushuka daraja msimu uliopita. Pia kuna Polisi Tanzania na JKT Mgambo zilizopanda daraja msimu huu. Hizi zilichukua nafasi iliyoachwa wazi na Polisi Dodoma, Villa Squad pamoja na Moro United ya Dar es Salaam.


 

By Jamhuri