Moja ya maeneo yanayotajwa mara kwa mara kuliwezesha Taifa kukabiliana na maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umasikini ni uboreshaji wa sekta ya elimu na ongezeko la wataalamu na wanataaluma wa ndani.

Sekta ya elimu inayoanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu imo kwenye orodha ya sekta zinazokabiliwa na changamoto nyingi huku zikiendelea kuongoza kwa umuhimu wake kwa jamii.

Kwa kutambua umuhimu na uboreshaji wa sekta hiyo, Serikali ilianzisha Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa mujibu wa Sheria Namba Tisa ya mwaka 2004, iliyoanza rasmi majukumu yake Julai 2005. HESLB ina umuhimu wa pekee kulisaidia Taifa kupitia wasomi hasa vijana wanaojiunga vyuo vikuu ama taasisi za elimu ya juu, kumudu gharama za masomo na hivyo kuwa miongoni mwa wanaowajibika kuchagiza kasi ya maendeleo ya nchi na ustawi wa watu.

Ndio maana miongoni mwa mifumo bora ya HESLB ikajikita katika kumwezesha mwanafunzi wakati wa masomo, lakini pia anapohitimu na kupata ajira ama shughuli rasmi ya uzalishaji inayomuingizia kipato, anapaswa kurejesha fedha alizozikopa.

Kwa maana fedha hizo zinastahili kuwa kwenye mzunguko wa kutoka kwa mwanafunzi mmoja hadi mwingine kadri ya misimu ya masomo na kwa namna hiyo, vijana wengi zaidi wa Tanzania hususani wanaojiunga na vyuo vikuu ama taasisi za elimu ya juu watanufaika.

Lakini katika hali isiyofaa, zipo taasisi zinazotajwa kutowasilisha makato ya wadaiwa wa HESLB kwa wakati. Miongoni mwa hizo zimo taasisi za umma. Si jambo jema hali kuwa hivyo ilivyo.

Taarifa ya HESLB kupitia tovuti yake wiki iliyopita, imetoa majina ya taasisi hizo huku Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji Mikopo wa bodi hiyo, Phidelis Joseph akisema jumla ya wanufaika wa mikopo imefikia 119,497.

Hali hiyo inatokea wakati kukiwapo njama za makusudi ama zinazotokana na kutokuelewa kwa baadhi ya waajiri, kutowasilisha taarifa za waajiriwa waliohitimu elimu ya juu ili wafanyiwe tathmini kama walikopa na hatimaye kurejesha mikopo hiyo.

Sisi tunatambua umuhimu wa elimu bora kwa jamii na taifa kwa ujumla, kisha umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi kupata elimu pasipo ‘kubebesha msalaba’ kwa wazazi.

Mazingira bora yanayomuwezesha mwanafunzi kumudu gharama za elimu ya juu ni pamoja na mikopo inayotolewa na HESLB na kwa hali hiyo, JAMHURI tunaamini kwamba njia pekee ya kuufanya mpango huo kuwa endelevu ni uwajibikaji katika kurejesha mikopo.

Hakuna njia ya mkato, kwa hali hiyo wanaohusika kwa namna yoyote kukakwamisha urejeshwaji wa mikopo ya HESLB  wanastahili kudhibitiwa kwa ukali na haraka ili kuepusha hatari ikiwamo kufilisika kwa mfuko wa Bodi hiyo..

By Jamhuri