Wakati wa Kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe akimtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kukiri serikali kushindwa kuongoza nchi kutokana na kuwepo na viashiria vya kudorora kwa uchumi wasomi wamepinga kauli hiyo.

Mbowe alimtaka Waziri Mkuu kueleza hali halisi ya uchumi ilivyo na kujibiwa kuwa suala hilo linahitaji tathmini kama uchumi umedorora au uko katika hali nzuri.

Wakati mjadala wa kudorora kwa uchumi na kupotea kwa fedha kwenye mzunguko ukiendelea, wataalamu wa masuala ya uchumi na wananchi mbalimbali wamekuwa na mitazamo tofauti.

Profesa Samwel Wangwe amelieleza JAMHURI kuwa ripoti iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 kuwa uchumi umeongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 mwaka jana kuwa hakuna tofauti kubwa inayoweza kuathiri ukuaji wa uchumi.

Profesa Wangwe anasema kwa muda uliobaki kuna uwezekano mkubwa wa ongezeko la uchumi licha ya wananchi kuona mzunguko wa fedha umepungua.

‘‘Kwa wale wanaofanya shughuli zao halali uchumi au mapato yao yameongezeka lakini wale waliokuwa wanategemea wizi wa fedha za umma (wapiga dili) kwa sasa wamekwama na wengi wao ndio wanaolalamika.

‘‘Fedha za wizi ndio zilikuwa kwenye mzunguko na watu wachache walitumia nafasi hiyo kujilimbikizia mali, mfano mtumishi mmoja wa Serikali aliyekuwa anamiliki nyumba 25 na viwanja 11 ni rahisi kwa watu wa namna hii kusema uchumi umedorora,’’ anasema Profesa Wangwe.

Anasema kwa upande mwingine Serikali inapaswa kuwaondolea vikwazo wananchi wanaofanya biashara halali ikiwa ni pamoja kodi, masoko ya bidhaa zao na mikopo kutoka taasisi za fedha.

Naye Mwadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana ambaye hakutofautiana na Profesa Wangwe anasema ushahidi wa kutosha wa kukua kwa uchumi haupimwi kwa fedha za mfukoni bali uzalishaji, ukusanyaji wa mapato na viashiria vya kisayansi na kitaalamu.

Anasema walizoea vibahasha na matumizi ya hovyo ya fedha za Serikali na sasa nidhamu ya watumishi wa umma na matumizi ya fedha yasiyo ya msingi na rushwa sasa yamefikia mwisho na watu wafanye kazi kwa bidii.

Hamis Jumanne (37) mkazi wa Temeke na mfanyabiashara wa soko la Tandika, amelieleza JAMHURI kuwa wimbi la wafanyabiashara kufunga biashara zao kwa madai ya kukosa wateja na mzunguko wa fedha kupungua halijasababishwa mdororo wa uchumi unaoelezwa.

Jumanne anasema kuwa awali wananchi wengi walizoea kuishi kwa fedha za wizi ambazo zilikuwa zinatakatishwa kupitia mzunguko wa fedha.

Anasema kwa sasa wananchi watalalamika kuhusu kuadimika kwa fedha, lakini kwa kipindi cha miaka miwili ijayo wengi watafurahia ukuaji wa uchumi ambao utamnufaisha kila mwananchi badala ya kuwanufaisha watu wachache kama ilivyokuwa kwa tawala zilizopita.

Wiki iliyopita Freeman Mbowe alieleza Bunge kuwa kuna viashiria kuwa uchumi unadorora na kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiri kwamba wameshindwa kuiongoza serikali.

Pamoja na malalamiko ya wananchi kwamba hali ya uchumi imekuwa ngumu katika kipindi hiki cha Utawala wa awamu ya Tano huku wengine wakifunga biashara zao kwa kukosekana kwa wateja, siku chache zilizopita Rais John Magufuli alieleza kuwa uhaba wa fedha uliopo ni bandia.

Rais Magufuli anasema mafisadi wameficha fedha majumbani na kutishia kubadilisha fedha ili waliozificha walazimike kuziingiza kwenye shughuli zakiuchumi na mzunguko wa fedha uwe mkubwa.

Wiki iliyopita Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hakuna uhaba wa fedha na kwamba jambo hilo halihusiani na kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Na kilichofanyika ni kuziba mianya ya upotevu wa mapato ikiwa ni jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza matumizi.

Profesa Ndulu amebainisha kuwa kiuchumi hawaoni fedha iliyopotea na kwamba wanaolalamika ni wale waliozoea kupata fedha kwa njia zisizo halali na sasa mfumo umebadilika ndio maana hawazini fedha walizozoea.

Anasema fedha imehama kutoka kwa watu waliokuwa wanazipata kwa wizi na kwenda kwenye shughuli za maendeleo ambako kila Sh 100 inayotolewa na Benki Kuu asilimia 36 inakwenda kwenye taasisi za fedha na asilimia 64 inakwenda kwa wananchi

Kuhusu kudorora kwa uchumi anasema hali ni nzuri na kwamba itaendelea kuimarika zaidi mwaka huu hadi kufikia ukuaji wa asilimia 7.2 kutokana na viashiria vingi kuonyesha mwenendo chanya.

Profesa Ndulu anaeleza viashiria hivyo ni pamoja kuongeka kwa uzalishaji wa saruji kwa asilimia saba hadi kufikia tani 725,000 katika robo ya kwanza ya mwaka, ikilinganishwa na tani 680,000 zilizozalishwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2015 na katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 uzalishaji wa umeme umeongezeka kwa asilimia 14.5 hdi kufikia kilowati (KWH) milioni 3,454.2 ikilinganishwa na kilowati milioni 3,016.7 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Profesa Ndulu anasema uagizaji wa malighafi za viwandani kutoka nje nao umeongezeka kwa silimia 19.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 hadi kufikia Dola za Marekani 520.2 milioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2015.

Anasema mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi nayo yameongezeka na kufikiaDola za Marekani 728.5 milioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.6 ikilinganishwa na ongezeko katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Ripoti ya Mwenendo wa Uchumi kwa mwaka unaoishia Juni 2016, inaonyesha mauzo ya mazao makuu ya biashara kama pamba, korosho na kahawa yameshuka kwa asilimia 8.8 hali iliyosababishwa na kushuka kwa kiwango uuzaji na kuporomoka kwa bei katika soko la dunia.

Hata hivyo mauzo ya mazao hayo yalifikia Dola za Marekani 828 milioni kwa mwaka 2016 kutoka Dola 907.8 milioni kwa mwezi Juni mwaka2015. Pia kiasi hicho ni cha chini ikilinganishwa na kile cha Juni 2014 ambacho kilikuwa Dola za Marekani 836.4 milioni.

Profesa Ndulu anasema katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016, makusanyo ya kodi yameongezeka ikilinganishwa na mwaka 2015 na hali hiyo inaonekana kuimarika kwa usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali sambamba na ukuaji wa hali ya uchumi.

Kuhusu deni la taifa, Profesa Ndulu anasema limeongezeka kutoka Dola za Marekani 19.8 bilioni mwaka 2015 na kufikia Dola 21 bilioni mwaka 2016 na kwamba takwimu zinaonyesha deni la Taifa ni stahimilivu.

Deni hilo la Taifa kwa thamani ya sasa ni asilimia 20 ya Pato la Taifa (GDP), ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya Pato la Taifa na hivyo kuonyesha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuendelea kukopa bila kuhatarisha ustahimilivu wa deni hilo.

Hata hivyo anasema Serikali imepunguza kukopa nje kwa sababu mikopo imekuwa na gharama kubwa ya riba, hivyo mikopo ya ndani imeongezeka kutoka Sh trilioni 8.6 hadi kufikia Sh trilioni 10. Deni la taifa kwa sasa ni Dola za Marekani bilioni 21 kati ya hizo deni la ndani ni Dola bilioni 5.

By Jamhuri