Wataalamu: Mtoto mpotevu Dar ana tatizo la kisaikolojia

Wanataaluma nchini wamesema kwamba wamefuatilia habari za kupotea na kupatikana kwa mtoto Happy Rioba (9), na kwa haraka wamegundua kwamba binti huyo ana tatizo la saikolojia tofauti na wengi wanaohusisha ushirikina.

Happy, anayeishi na mama yake, Sarah Zefania huko Mkuranga mkoani Pwani, aliripotiwa na vyombo vya habari kupotea na kupatikana zaidi ya mara moja, tukio lililovuta hisia za watu wengi.

Awali alipopotea, alipatikana Uwanja wa Ndege Zanzibar kabla ya kupotea tena na kupatikana Bandari ya Dar es Salaam wiki iliyopita. Kitendo cha kupatikana Zanzibar kilizua maswali mengi, lakini kubwa ni kwamba ilikuwaje akapanda ndege bila ya kukaguliwa?

Miongoni mwa watu wanaosimamia imani za ushirikiana, Sara, ambaye ni mama mzazi anasema: “Baba mzazi wa Happy ndiye mhusika kwani tangu tulipotengana miaka mitatu iliyopita, mtoto amekuwa na matukio yasiyoeleweka.”

Akisisitiza bila kutoa ufafanuzi wa kina, Sarah anasema: “Angekuwa hahusiki, basi angetoa ushirikiano katika matatizo hayo ya mtoto. Amekuwa akinitisha mara kwa mara.”

Lakini wataalamu hao wa masuala ya jamii, wameainisha sababu za kitaaluma zinazofanya kupotea kwa mtu huku wakisema matukio kama hayo ni mengi hususani kwa watoto ambao wazazi wao wana msuguano katika ndoa.

Mhadhiri wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) ya jijini Dar es Salaam, Suleiman Mtwana, akizungumza na JAMHURI kuhusiana na kupotea kwa watoto, alisema: “Kwanza tuondokane na imani za kishirikina. Kupotea kwa mtoto ama mtu kimsingi ni tatizo la kisaikolojia. Wengi wanakuwa na misongo mingi ya mawazo na akili zao huwatuma kuondoka nyumbani kwani huhisi hawako salama katika mazingira waliyopo. Hii inatokana na matatizo ya kifamilia yanayowazunguka.”

“Familia nyingi wanazotoka watu hawa ni zile zinazolelewa na mzazi mmoja. Malezi ya mzazi mmoja mara nyingi huchangia kuondoka kwa watoto nyumbani,” alisema.

“Wengine ni wale ambao hawana wazazi. Malezi ya baadhi ya walezi huchangia baadhi ya watoto kutoweka nyumbani. Kuna wanaotoka kwenye familia zenye hali duni za kiuchumi. Wakati mwingine hali duni ya kiuchumi huwasukuma watoto kuondoka nyumbani kwenda kusaka maisha mahali pengine kusikojulikana,” anaeleza Mtwana kuhusiana na upotevu wa watoto.

“Migogoro ya kifamilia nayo ni chanzo cha watu kutoweka nyumbani. Familia zilizogubikwa na migogoro husababisha watoto kuathirika kisaikolojia na wengine kuishia mitaani wakirandaranda huku na kule huku wengine wanapohojiwa hushindwa kutoa majibu yanayoeleweka,” anaongeza Mtwana.

JAMHURI ilipotaka kujua suluhisho la tatizo, Mtwana anaeleza kuwa “kama nilivyoeleza, tatizo hili kimsingi ni la kisaikolojia. Linahitaji muda kwa mtu kuweza kupona kwani linakuwa limeathiri akili ya mhusika. Mtaalamu anatakiwa afanye kazi… mara kwa mara hadi mgonjwa kurejea katika hali ya kawaida.”

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii na Afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ng’amilo Mbwalila, alipohojiwa na JAMHURI kuhusiana na upotevu wa watoto, alisema; “Kuna mambo mengi sana yanayochangia mtu kutoweka nyumbani.”

Anasema: “Ili kujua ni nini kimesababisha mtu kuondoka nyumbani ni lazima kwanza ufike nyumbani anapoishi. Ukifika hapo utaona mtindo wa maisha anaoishi na watu anaoishi nao. Hapo ndipo utakapogundua chanzo cha tatizo.”

Anaelezea, akisema, “Kuna wanaoondoka nyumbani kutokana na malezi mabovu ya wazazi ama walezi, kuna wanaoondoka nyumbani kutokana na kuhitaji uhuru uliopitiliza, wengine hukimbia manyanyaso yaliyopo nyumbani, huku wengine wakikimbia hali ngumu za maisha zilizopo nyumbani.

“Wengi wakishaonja mitindo ya maisha ya mitaani ni vigumu kurejea katika maisha ya kawaida ya familia. Hata maisha ya shule huwashinda. Na wanaporejeshwa nyumbani hutoweka tena mara kwa mara,” alisema Ng’amilo.

“Mfano, awali kabla ya kuwa hapa Muhimbili nilikuwa Afisa Usalama wa Watoto katika taasisi moja ya kijamii huko Moshi. Moja ya shughuli zangu ilikuwa ni kuwaunganisha na kuwarejesha watoto katika familia zao. Lakini tatizo, wengi wao unapowarejesha hurejea tena mitaani,” anasema afisa huyo.

Kutokana na matatizo haya niliyoyataja na mengine ya kifamilia, watoto hawa wanakuwa wameathirika kisaikolojia. Ni vigumu kurejea katika maisha ya kawaida ya kifamilia, anaeleza.

Ng’amilo anasema kuwa ni wakati sasa kwa jamii kuachana na imani za kishirikina na kushirikiana katika kutatua tatizo hili kwa kutoa malezi stahiki kwa familia zinazokabiliwa na matatizo ya kijamii.

Tatizo hili lina uhusiano mkubwa na familia zenye matatizo. Siku hizi ndugu, jamaa na marafiki hawawajibiki katika kutatua matatizo ya familia za watoto waliopoteza wazazi, na hii inasababisha wengine kuishia mitaani wakisaka maisha kwa mitindo ambayo si sahihi wala endelevu, huku ikizua maswali mengi yasiyo na majibu, anaeleza Ng’amilo.