Mkanganyiko wa matokeo mabaya ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka jana, yameendelea kuumiza vichwa vya wazazi na wadau wa sekta ya elimu mkoani Mbeya. Wazazi waliozungumza na JAMHURI wanaitupia lawama Serikali kwamba haijasimamia vizuri sekta hiyo, kwani imeruhusu walimu kujifanyia mambo yao pasipo kujali kazi yao ya kufundisha.

Wanasema sekta ya elimu imekosa usimamizi kwa sababu wahusika hawawajibiki ipasavyo, kutokana na kufumbia macho mambo yanayofanyika kinyume cha sheria.


Rehema Mwamengo, mkazi wa MIST Iyunga jijini Mbeya, anataja baadhi ya mambo yanayochangia kuzorotesha elimu kuwa ni majengo ya shule za Serikali kugeuzwa vituo vya twisheni.


Anasema hivi sasa walimu wameacha kufundisha darasani muda wa kawaida wa masomo, na badala yake wamekuwa wakisubiri kufundisha muda wa jioni kwenye vituo vyao vya twisheni, na Serikali haiwachukulii hatua yoyote.


Kwamba suala la twisheni limekuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu wanalazimishwa kuchangia fedha, ili mtoto ahudhurie twisheni kwa mwalimu yule yule anayefundisha somo husika shuleni.

 

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda, anakiri kuwapo kwa twisheni shuleni, lakini anapinga kuwa vituo hivyo ndiyo sababu ya kuwa na matokeo mabaya ya kidato cha nne.

 

Kaponda anasema mara nyingi shule za mijini ndizo zinazofundisha masomo ya ziada, na ndizo zilizofanya vizuri katika mitihani hiyo, tofauti na shule zilizoko pembezoni (vijijini) ambako wanafunzi hawajui kabisa suala la twisheni.

 

Aidha, anakiri kuwa masomo ya twisheni hayamsaidii mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi ambao Serikali inataka, badala yake wanafundishwa jinsi ya kujibu mitihani tu.

 

Anakiri pia kwamba wingi wa wanafunzi darasani huchangia kuwa na matokeo mabaya, kutokana na mwalimu kushindwa kumudu darasa kwa kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja.

 

Kwamba mwalimu anageuka kuwa mhubiri anapokuwa anafundisha darasani, badala ya kuwa mwezeshaji ili wanafunzi waweze kumwelewa kirahisi na yeye kuwaelewa wanafunzi na kuwamudu kujua maendeleo yao.

 

Hata hivyo, kutokana na kuwapo kwa mlundikano wa wanafunzi darasani, ofisa elimu huyo wa mkoa anatoa wito kwa wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.

 

Anasema kuwa suala la uchangiaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa haufanyiki sana sana mjini, kutokana na wazazi na wananchi wengi kujikita kwenye uchangiaji wa sherehe na si ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Francis ya jijini Mbeya ndiyo iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012.

 

Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya walimu wa shule hiyo wamelalamika kuwa Serikali haitambui mchango wa shule hiyo, hususan walimu ambao ndiyo wenye shughuli kubwa.

 

Wamesema mara nyingi Serikali imekuwa ikitoa pongezi kwa shule kwa kutoa vyeti, ikiwa ni pamoja na kuwaita wanafunzi kwa ajili ya kuwapongeza lakini upande wa walimu ambao hutoa wanafunzi bora kitaifa wamesahaulika.


“Tunafundisha vizuri na kutoa wanafunzi bora kitaifa, lakini hata siku moja sijawahi kusikia walimu wakiitwa kupewa zawadi au mchango wao kutambuliwa,” amesema mwalimu mmoja.


Walimu hao wanalalamika kuwa pamoja na shule yao kuongoza kwa kufaulisha kitaifa mara nyingi, Serikali haitoi majibu kuhusu nafasi wanazokuwa wameshika wanafunzi wao. Wanasema mara nyingi shule hiyo imekuwa ikishika nafasi za juu, lakini haijawahi kutokea wanafunzi wa St. Francis wakatangazwa kuhusu nafasi wanazokuwa wazishika badala yake wanakaa kimya.


“Nimekaa shuleni hapa kwa zaidi ya miaka mitano na tumekuwa tukiongoza kama kawaida, lakini bado nafasi za wanafunzi wetu kitaifa hazijulikani, sasa nashindwa kuelewa,” amehoji mwalimu mwingine.


Wanasema kuwa shule hiyo haijawahi kuweka wastani wa ufaulu ili kuwachuja kidato cha pili, bali hupokea wote hata wasiokuwa na akili wakiamini kazi ya mwalimu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anafaulu vizuri.


Wanasema shule hiyo inafundisha Watanzania na kutoa wanafunzi bora ambao wanaendelea kufanya vizuri katika ngazi za juu ndani na nje ya nchi, hivyo ni bora Serikali ikawa na utaratibu wa kutambua michango ya walimu husika.

 

Wakizungumzia shule nyingine kutofaulisha vizuri, wamesema inatokana na maslahi duni ya walimu ambapo mwalimu anakwenda darasani kutimiza wajibu na si kufundisha ili mwanafunzi aelewe.

Wameongeza kusema kuwa walimu wanajikita zaidi kufundisha masomo ya ziada, ili kuongeza vipato vyao kutokana na kuwa na maslahi duni kutoka serikalini na kwa waajiri wao.


 

1084 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!