Wataliban wapandisha bendera ya utawala 

KABUL, AFGHANISTAN

Wanamgambo wa Taliban wamepandisha bendera nyeupe kwenye jengo la rais kuashiria mwanzo wa utawala wao katika taifa la Afghanistan.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya operesheni ya kuleta amani iliyoanzishwa na Marekani ndani ya taifa hilo kukoma.

Ripoti za vyombo vya kimataifa zinaeleza kuwa wakati tukio hilo linatokea, taifa la Marekani limo kwenye kilele cha kutimiza miaka 20 tangu kutokea shambulio la kigaidi la Septemba 11, ambalo ndio msingi wa Afghanistan kuvamiwa kijeshi.

Awali, bendera kama hiyo ilipeperushwa mjini Kabul karibu na majengo ya Ubalozi wa Marekani ambayo hayana watu kwa sasa.

Vilevile bendera za vikosi hivyo zimeendelea kusimikwa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kabul kama ishara ya kuyataarifu mataifa ya kigeni kuwa utawala umebadilika katika taifa hilo.

Waziri Mkuu wa vikosi vya serikali iliyo chini ya Taliban, Mullah Mohammad Hassan Akhund, anasema kupandisha bendera zao ni ishara ya kuanza kwa shughuli za serikali mpya ndani ya taifa hilo.

Serikali ya taifa la Afghanistan imetangazwa na vikosi hivyo siku za hivi karibuni ikiwa na viongozi wa jinsia ya kiume tu, hali inayoibua minong’ono kwa jumuia za kimataifa ambazo zilitarajia vikosi hivyo vingewaweka hadi wanawake.

Kabla ya tukio la Septemba 11, jeshi la wanamgambo wa Taliban limewahi kuiongoza Serikali ya Afghanistan kwa mkono wa chuma.

Baada ya tukio hilo inaelezwa kuwa wanamgambo hao walizima televisheni ya taifa na kuzuia matangazo ya redio katika mji wa Kabul.

Hata hivyo, Desemba 7, mwaka 2001 Marekani pamoja na washirika wake walifanikiwa kuwafurusha wanamgambo hao ambao walikimbilia kusini mwa mji wa Kandahar.

Baada ya miaka 20 sasa wanamgambo hao wamerudi kwenye mji wa Kabul kuendeleza utawala wao huku mbinu za kuendesha mapinduzi zikiwa zimebadilika.

Kwa sasa hakuna milio ya risasi inayosikika mitaani, badala yake Wataliban wanatumia mbinu za uvamizi na kuweka vizuizi vingi katika miji.

Miaka ya 1990 wakati wanamgambo hao wanautawala mji wa Kabul, vibanda vya vinyozi vilizuiliwa, lakini tofauti na sasa, wapiganaji hao wanakata nywele.

Tangu wameingia madarakani, wanamgambo hao wamezuia michezo kuwahusisha wanawake, pia wamewazuia wanawake kushiriki maandamano ya kudai haki katika taifa hilo.

Mmoja wa wanawake aliyekuwa na ndoto ya kuwa maarufu katika mchezo wa ngumi katika taifa hilo, Marzia Hamidi, anasema kitendo cha Wataliban kurudia kuitawala nchi hiyo kimezima ndoto hiyo.

Hivi karibuni amekamatwa na vikundi vya wanamgambo hao akituhumiwa kuwa kibaraka wa mataifa ya nchi za Magharibi.

Analilaumu taifa la Marekani kuondoa majeshi yake ndani ya taifa hilo, akisema haishangazi, kwani taifa hilo halikuwa ndani ya taifa hilo kwa lengo la kulinda amani, bali kwa masilahi binafsi.