Watanzania huu ndiyo ugaidi

Ndugu zangu nikiwa nawaza tukio baya la ugaidi lililotokea nchi jirani ya Kenya, punde napokea waraka kutoka kwa ndugu yangu Goodluck Mshana. Kipekee nianze kwa kuipa pole ya dhati Serikali ya Kenya na watu wake juu ya tukio la kigaidi lililotokea hivi karibuni. Aidha, niwapongeze wananchi wote wa Kenya kwa moyo wa kutoa pesa na damu kwa wapendwa wao.

Tunasema poleni sana na Mungu awape moyo wa ujasiri familia zote, ikiwamo ya Rais Uhuru Kenyatta, mlioguswa kwa ukaribu na maumivu ya tukio hilo. Watanzania sote tumeshuhudia yaliyojiri Kenya juu ya uvamizi wa kigaidi unaohusishwa moja kwa moja na kikundi cha Al-Shabaab. Magaidi hao waliweza kuvamia jengo la kitegauchumi la Westgate na kulishikilia kwa takribani siku nne mfululizo pamoja na raia wa Wakenya.

 

Waliweza kuingia na nyenzo za kivita zikiwamo bunduki kama AK-47, mabomu ya kurusha kwa mkono na bastola. Walikuwa katika mavazi maalum yenye kuficha sura zao. Idadi yao mpaka sasa inasemekana walikuwa zaidi ya 15.

 

Serikali ya Kenya ikitumia uwezo wake wa kijeshi na kitaalamu iliweza kupambana na magaidi hao na bendera za nchi zikapepea nusu mlingoti, kuashiria kwamba kazi imekwisha na magaidi wapo mikononi mwa jeshi, huku baadhi wakiwa wameuawa.

 

Ikumbukwe kwamba mipango ya kigaidi huwa ni ya siri kubwa inayoambatana na viapo. Mipango hii haifanyiki hotelini/mgahawani ama kwenye nyumba ya mtu; tena kwa kujirekodi na kupost youtube! Mipango yote hupangwa kitaalamu na kutokea kama ‘surprise’.

 

Wala hakuna mwanasiasa (Mwigulu case study) anayejitapa mitaani na kwenye majukwaa kwamba anao mkanda/video ya kigaidi! Tumeshuhudia watu takriban 72 wakiwamo wanajeshi, wanausalama, watoto na raia, wakipoteza maisha. Halikuwa tukio jepesi hata kidogo! Na wala tusiuhubiri ugaidi kisiasa tukidhani ndiyo kinga dhidi ya wapinzani.

 

Ugaidi hulenga makundi ili kuwaumiza maadui wao. Gaidi hamlengi mwandishi wa habari wala shabiki wa kisiasa ambaye hana madhara yoyote kwa uhai wa chama cha kisiasa. Gaidi hulenga Serikali, jeshi na mamlaka kubwa kupenyeza maumivu kwa watawala.

 

Tumeona matamko na salamu za pole kutoka mataifa mbalimbali na Tanzania ikiwamo. Yote yakioneshwa kuguswa na masaibu yaliyoipata Kenya. Huku wasomi na washauri wa kisiasa wakitoa angalizo kwa Serikali ya Tanzania kujitathmini kiusalama kwani tukio kama hilo hata hapa linawezekana.

 

Matukio ya kigaidi yanajulikana kimataifa. Na hata likitendeka basi dunia hupatwa na wingu jeusi. Ugaidi wa Tanzania sijui mlipata salamu kutoka kwa nani! Au hata Serikali yenyewe ilijipa pole kwa huo uliohubiriwa na kina Mwigulu na Nape kuwa ni gaidi?

 

Mataifa mbalimbali yamehusika kuisaidia Kenya kupambana na magaidi. Israel imekuwa ya kwanza kutoa msaada wa kijeshi na kitaalamu. Serikali ya JK nayo ikawasiliana na Kenyatta endapo atahitaji msaada wowote kutoka Serikali ya Tanzania.

 

Serikali yetu iepuke kuharibu kodi za wananchi kwa joto la kisiasa inalolipata kutoka kwa wapinzani. Niwatake Nape, Mwigulu na CCM yote kuepuka kuwatuhumu watu kwa kuwaita magaidi. Hata kule Zanzibar matukio ya tindikali yamekuwa kama kumwagiana juisi ya Azam. Makanisa kuchomwa moto n.k. Lakini hakuna niliposikia, mkiwamo ninyi wenyewe, Serikali ama mataifa yakikimbilia kuwa ni ugaidi.

 

Msiididimize nchi hii, hasa kiutalii na mambo mengi ya kiuchumi na kijamii, hasa kwa kauli zenu nyepesi za ‘ugaidi’. Watu wanaogopa kuwekeza kwa siasa chafu.

 

Mjitathmini upya kisiasa na kama mnaona joto ni kali si dhambi pia kukaa pembeni na kuwaachia wengine. Upinzani hautamalizwa kwa tuhuma za ugaidi. Kufanya hivyo ni kujimaliza.

 

Watanzania wanayaona yote yanaotendeka kuanzia kule Arusha kulikotokea mlipuko!

 

0713 246 764