‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania’ ni kitabu kilichoandikwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1994. Ndani ya kitabu hiki kuna maneno mengi makali na ya kukosoa uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya wakati huo, iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi. Mwalimu aliwakosoa wazi wazi aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba. Ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya kitabu hicho kama inavyoletwa kwenu neno kwa neno kama alivyoandika Mwalimu mwenyewe. Endelea…

Kimya

 

Kimya kina mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele;

Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile

Kimya msikidharau, nami sikidharawile;

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.

Kimya ni giza kizushi, kuzukia walewale

Kimya kitazua moshi, moto msiyafumbule;

Kimya kina mshawishi, kwa daima na milele

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.

Kimya vuani maozi, vuani mato muole;

Kimya kitangusha mwanzi, mwendako msijikule;

Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya.

 

Bwana Muyaka bin Haji,

 

Kimya kimya msidhani

ni ishara ya amani

 

Yafuatayo nii maelezo mafupi ya mtiririko wa matukio ya kisiasa yaliyotufikisha kudai Utanganyika. Yalikuwa yako tayari kabla Halmashauri Kuu ya Taifa haijatangaza maoni ya wanachama wa CCM kuhusu muundo wa Muungano. Lakini sikuona sababu ya kubadili chochote.

 

Julius K. Nyerere

 

UONGOZI WETU

NA

HATIMA YA TANZANIA

 

1. RIPOTI YA JAJI NYALALI:

Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza mambo mengi, lakini yanayotuhusu hapa ni mawili:

(i) Pendekezo la kugeuza mfumo wa Chama Kimoja cha Siasa, na kuleta mfumo wa Vyama Vingi; na

(ii) Pendekezo la kugeuza mfumo wa Muungano wa Serikali Mbili, na kuleta mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu.

 

La kwanza lilikubaliwa na Chama na Serikali, na la pili likakatiliwa. Linalohitaji maelezo ni hilo la pili. Waingereza wana msemo: ‘Ignorance is bliss’; ujinga ni baraka. Wako watu wanaodhani kuwa pendekezo la Tume ya Nyalali la kutaka Shirikisho la Serikari Tatu, linatokana na maoni au matakwa ya watu. Hiyo si kweli hata kidogo. Lakini watu wanaotaka tuamini kwamba wasemavyo ni kweli si watu waongo, ni wajinga tu, maana nadhani hawajasoma Ripoti ya Tume ya Nyalali. Hotuba ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, ya tarehe 30 Aprili, 1992, katika Bunge la Muungano inaeleza vizuri sana ukweli ulivyo.

 

“Mheshimiwa Spika, mojawapo ya mapendekezo makubwa yaliyotolewa na Tume ya Nyalali lilihusu mfumo wa Muungano na Ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Tume ya Nyalali ilipendekeza kuubadili mfumo wa Muungano ili kuanzisha mfumo mpya wa Shirikisho lenye Serikali Tatu. Yaani, Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.

 

Mheshimiwa Spika, hili ni pendekezo kubwa na la msingi ambalo kama ilivyofanya Tume, Chama Cha Mapinduzi na Serikali zimelitafakari kwa undani zaidi.   Katika kufanya hivyo, historia ya Muungano tangu tarehe 26 Aprili, 1964 hadi sasa imezingatiwa. Muungano kama mnavyofahamu waheshimiwa wabunge, chimbuko lake ni mapatano ya “Article of Union” yaliyotiwa saini na waasisi wa Muungano, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mungu aiweke roho yake pema.

 

“Mapatano hayo yalifanywa kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania. Hilo halina ubishi. Miungano mingi ya aina hii duniani, imefanywa na viongozi kwa njia hii au nyingine kwa niaba ya wananchi, bila kuhojiwa na hapana sababu ya kuhojiwa kitendo hicho. Kwa msingi huo, wale wachache wanaohoji na kutaka kura ya maoni juu ya suala hili, hawaitakii mema nchi hii. Hoja hiyo haikubaliwi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (makofi)

 

“Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Muungano wa nchi zilizokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika, ziliungana na kuwa nchi moja na Taifa moja. Narudia tena, ziliungana kuwa nchi moja na Taifa moja. Kwa lugha ya kigeni, ‘One Sovereign State’. Hivyo imejenga msingi imara wa umoja kati ya wananchi wa Tanzania. Tanzania Bara na Visiwani, zimekuwa zikifaidika kisiasa, kiuchumi na kiulinzi chini ya mfumo uliopo wa Muungano. (makofi).

 

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na baadhi ya sababu zilizotolewa na Tume ya Nyalali kuwa ndizo ambazo mara nyingine zimesababisha hali ya kutoridhika na mfumo wa Muungano. Matatizo yapo, mengi ya matatizo hayo ni ya utekelezaji yaliyojitokeza wakati wa kushughulikia mambo ya Muungano. Na bila ya kuyaficha baadhi ya matatizo hayo ni mambo yanayohusu suala la uraia, milki ya fedha za kigeni, ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kutokana na kodi na ushuru wa Forodha, tatizo la formula ya kuchangia gharama za Muungano. Hakuna shaka kwamba haya ni matatizo na mara nyingine yanakera:

 

Hata hivyo, kwa heshima zote kwa Tume, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kuwa utatuzi au ufumbuzi wa matatizo hayo, hautapatikana kwa kuanzishwa Shirikisho la Serikali Tatu. Kinyume chake hiyo itakuwa ni chanzo cha kufifisha umoja na mshikamano wa Tanzania uliojengeka tangu mwaka 1964. Inatoa mwanya kwa wasiopenda umoja huo hatimaye kuuvunja. Hiyo siyo kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania nzima. (makofi).

 

Mheshimiwa Spika, matatizo ni lazima yatatuliwe. Hivyo ni azma ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali kueleza nguvu zake zote katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo. Serikali na Chama zitaendelea kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo halisi na kuyaondoa kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania chini ya mfumo wa sasa. Hivyo, kwa sasa Serikali inafanyia kazi maeneo yanayohusika. Uhusiano wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hasa katika maeneo yanayohusu matatizo niliyoyaainisha.

 

Kwa mtazamo huo, ndiyo maana katika marekebisho ya Katiba wakati huu, eneo linalohusu Rais wa Jamhuri ya Muungano pamoja na uchaguzi wake na wa Makamu wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar linawekwa kando, likisubiri mapendekezo mapya ya Serikali kwa Bunge lako Tukufu kwa kutungiwa muswada utakaowasilishwa hapo baadaye katika Bunge lako Tukufu. Kwa wakati huu sehemu hii ya Katiba itatoshelezwa kwa muda na ibara ya 37 ya Katiba ya Jamhuri. Rekebisho hili limefanywa katika muswada na kubadili katika Katiba.

 

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ukweli kwamba tangu mwanzo ulipoanzishwa Muungano waasisi kwa makusudi kabisa, hawakutarajia muundo wa Shirikisho la Serikali Tatu au Serikali moja, ni dhahiri muundo unaopendekezwa unatutoa kutoka msingi huo wa awali. Ni mfumo ambao unadhoofisha nchi nzima ya Tanzania kwani Shirikisho ambalo lingeweza kuundwa na nchi mbili huru zenyewe zikibakia kuwa ni Jamhuri na hivyo kuwa na Serikali tatu, halitasaidia lolole katika kudumisha hali ya utulivu na usalama ya wananchi wetu. (makofi).

 

Hapatakuwa na mshikamano madhubuti katika masuala ya uchumi na maendeleo ya jamii na gharama ya kuziendesha Serikali tatu, ingekuwa kubwa sana na isiyo ya lazima. Kwa sababu hizi, ndiyo maana Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake hazikubali pendekezo la Tume ya Nyalali la kuanzisha mfumo mwingine wa Muungano wa Serikali tatu. (makofi).

 

Isitoshe Mheshimiwa Spika, hata pendekezo hili silo la wananchi wengi. Kwani taarifa ya Tume inasema, na naomba ni nukuu. ‘Zaidi ya hayo wengi wa wananchi waliotoa maoni yao kwa Tume hawakuelezea chochote juu ya mfumo wa Serikali ambao Muungano uwe nao. Kati ya wananchi elfu tatu (3,000) waliojitokeza kwenye Tume huko Zanzibar ni wanne (4) tu waliozungumzia jambo hilo ambayo ni asilimia (0.13) ndio waliopendekeza kuwepo kwa mfumo wa Serikali tatu. Na kati ya wananchi 32,275 waliotoa maoni yao Tanzania Bara, ni wananchi 45 tu ambao ni asilimia (0.13) ndiyo waliopendekeza Mfumo wa Serikali tatu. Wana-Tume ambao hawakubaliani na pendekezo hilo la kuwa na Serikali tatu, walisisitiza kwamba na ningewanukuu; ‘Pamoja na kuelewa kuwa baadhi ya mambo mengine siyo lazima uamuzi wake kutegemea wingi wa watoa maoni, lakini pia tunaona kuwa siyo busara kupendekeza mabadiliko makubwa kama haya ya mfumo wa Muungano wetu kwa kutegemea maoni ya Watanzania 49 kati ya Watanzania 36,299 walioshiriki katika mjadala wote ulioendeshwa na Tume ya Rais. Idadi hii ni ndogo isiyo na uzito kitakwimu.’

 

Sisi hatuoni kuwa kuna hoja ya kisheria na ya kisiasa ya kubadili mfumo wa sasa wa Serikali mbili na kuanzisha mfumo wa Serikali tatu. Tanaamini kuwa mfumo wa Serikali tatu utadhoofisha Muungano wetu kisiasa na kiuchumi”. (makofi).

 

Hivyo ndivyo, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania alivyosema Bungeni tarehe 30 Aprili, 1992; akashangiliwa na kupigiwa makofi na Wabunge wa Tanzania. Baadaye, kama tunavyojua, Waziri Mkuu aliisahau hotuba hii; na wabunge waheshimiwa walisahau shangwe zao na makofi yao. Wakapitisha Bungeni, “kwa kauli moja”, Azimio la kutaka Serikali ya Tanzania ilete muswada wa kubadili Katiba ya Nchi yetu ili kuwa na Serikali

ya Tanganyika “ndani ya Muungano”, kwa madai ya kwamba hayo ndiyo matakwa ya wananchi wa Tanzania.

 

Lakini ukweli wa suala hili unabaki pale pale: Wananchi wa Tanzania hawadai Serikali ya

Tanganyika; na mimi nasema, ukifufua Tanganyika, utaua Tanzania. Fahali wawili hawakai zizi moja: “Yeltsin” wa Tanganyika ataua Muungano. Lakini pia sababu zile zile za ukabiIa na udini na tamaa za uongozi zitakazoua Tanzania hatimaye zitaiua Tanganyika nayo.

 

Itaendelea

 

By Jamhuri