Wiki mbili zilizopita, niliamua kubadili utaratibu wa kutumia usafiri wa daladala, nikachagua kutumia gari moshi (treni) kwenda kazini na kurudi nyumbani jijini Dar es Salaam.

 

Siku moja, takriban dakika nne baada ya kuondoka kituo cha Ubungo Maziwa kuelekea kituo cha Dar es Salaam (Mjini Kati), treni ilisimama ili kupakia abiria katika kituo cha Mabibo.

 

Kwa kawaida treni hii ya jijini Dar es Salaam hutumia dakika mbili kupakia na kushusha abiria katika kila kituo. Lakini siku hiyo ilizidisha muda wa kusimama kituoni hapo. Abiria wengi tulishangaa kuona hali hiyo isiyo ya kawaida.

 

Baada ya kuona muda unazidi kuyoyoma huku wafanyakazi wa treni wakikaa kimya bila kutujulisha sababu ya kuchelewa kituoni hapo, baadhi ya abiria tulichungulia nje kuona kinachoendelea. Ndipo tulipoona wafanyakazi wa treni na askari polisi wakijizatiti kuchungulia chini ya mabehewa.

 

Kumbe treni ilikuwa imepata hitilafu (tatizo la kiufundi), lakini wafanyakazi husika wakaamua kukaa kimya bila kujulisha abiria kilichotokea. Tulichelewa kituoni hapo kwa zaidi ya dakika 15 kabla ya tatizo husika kurekebishwa na treni kuendelea na safari.

 

Wakati wote tuliokawizwa kituoni hapo, karibu abiria wote walikuwa wakilalamika na kunung’unika tu. Abiria wengi hawakuwa tayari kujitokeza kuuliza wafanyakazi husika sababu ya treni kusimama kwa muda wote huo usio wa kawaida yake. Tuliojitokeza kuhoji hali hiyo hatukuzidi wanne kati ya abiria zaidi ya 1,300 tuliokuwa kwenye mabehewa yote manane.

 

Tangu siku hiyo nikaanza kuamini kuwa Watanzania wengi ni waoga wa kuhoji na kudai haki zao. Woga huu umeendelea kuwa chanzo kikuu cha wengi wetu kunyimwa, kudhulumiwa, kupunjwa na kucheleweshewa haki zao. Hili ni tatizo lisilo la lazima katika jamii, ni tatizo la kujitakia.

 

Fikiria kwamba abiria wote tuliokuwa kwenye treni siku hiyo tulipaswa kuhoji wafanyakazi husika watueleze, kwanini imetumia muda mrefu kusimama na sababu ya wao kukaa kimya bila kutufahamisha tatizo lililopo na hatima yake. Tena ikibidi tuwachukulie hatua za kisheria kwa kukwepa majukumu yao hayo. Lakini abiria wengi hawakuthubutu kufanya hivyo, waliogopa kuhoji na kudai haki yao.

 

Hata kwenye daladala na mabasi ya abiria, hali ni hiyo hiyo. Abiria wengi hawadai haki zao wakati madereva na makondakta wanapokiuka utaratibu wa kuwasafirisha hadi mwisho wa safari zao. Wamekuwa wakikubali kukatishiwa safari bila kurudishiwa sehemu ya nauli walizolipa.

 

Vivyo hivyo, Watanzania ni waoga kuhoji na kudai haki zao katika taasisi za umma kama vile hospitali na shuleni. Wananyanyaswa hata pasipostahili kunyanyaswa na kuburuzwa.

 

Kwa mfano, wengi tunajua huduma za matibabu kwa wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wazee wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea zinatolewa bure katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Serikali. Lakini ni wangapi walio na uthubutu wa kukataa kudaiwa gharama za huduma hizo? Ni wachache mno katika nchi hii!

 

Wamiliki wa nyumba za kupanga wanapandisha kodi za pango kila mwaka bila kufanya ukarabati au maboresho yoyote. Wengi hawahoji uhalali wa kupandishiwa kodi hivyo. Walimu wanawaongezea wazazi mzigo mkubwa kwa kuibua michango isiyo rasmi mara kwa mara. Ni wazazi wachache mno wanaohoji sababu za michango hiyo, ingawa hatimaye nao hujikuta wanakubali yaishe, wanailipa hata kama watabaini si halali.

 

Ndiyo maana baada ya kugundua ugonjwa huo (woga) wa Watanzania, baadhi ya viongozi wamekuwa ndiyo watu wa kuamua leo ijengwe barabara, kesho ijengwe zahanati na keshokutwa ijengwe shule ya sekondari. Wananchi ambao kimsingi ndiyo waajiri wa viongozi, siku zote wamekuwa waoga wa kutumia haki yao ya kuamua miradi wanayotaka kujengewa, kulingana na vipaumbele vya mahitaji yao ya kimaendeleo.

 

Watanzania wengi wamekuwa waoga wa kuhoji matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwa hofu ya kuchukiwa na mafisadi. Wanaona bora waache rasilimali hizo zifujwe na kuwanufaisha wachache, kuliko wao kuchukiwa na viongozi wachache wasio waadilifu na waaminifu katika utumishi wa umma.

 

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya viongozi wetu wamekuwa kiburi na wengine wamejigeuza miungu-watu katika ofisi za umma. Wanatumia madaraka waliyokabidhiwa na umma kujiamulia mambo wanayoona yanawapatia manufaa binafsi.

 

Ndiyo maana hivi karibuni tuliona na kusikia wabunge wetu wakiunga mkono mifuko ya hifadhi ya mafao ya jamii, kwa kupitisha muswada wa sheria ya kuondoa fao la kujitoa bila kuwashirikisha wafanyakazi husika. Hata hivyo, baadaye wafanyakazi walipata nguvu ya ziada iliyoshawishi kurejeshwa kwa sheria ya fao hilo, ingawa utekelezaji wake bado ni kitendawili.

 

Woga umesababisha Watanzania wengi kukosa na kunyimwa haki zao katika ofisi za umma, kampuni na mashirika yanayomilikiwa na watu binafsi. Wengi hawako tayari kuihoji Serikali tuliyoiweka madarakani sababu za kushindwa kusimamia taratibu za nchi, na hata kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali nchini.

 

Uchunguzi umebaini kuwa woga unachangia ugumu wa maisha ya Watanzania walio wengi. Wengi hawako tayari kuihoji Serikali kuhusu utekelezaji wa ahadi za maendeleo ilizowaahidi wakati wa kuomba madaraka ya nchi. Inawezekana pia wengi hawako tayari kuiadhibu kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

 

Tutakuwa wageni wa nani tunapoendelea kukumbatia kasumba ya woga wa kudai haki zetu katika mazingira mbalimbali ndani ya nchi yetu huru? Hivi kweli tumekubali kuendelea kupunjwa na kudhulumiwa haki zetu kwa sababu ya woga wetu? Hapana, umefika wakati tuseme imetosha.

 

Umefika wakati Watanzania wote tuseme woga kwetu sasa basi. Tujenge uthubutu na ujasiri wa kuhoji na kudai haki zetu. Penye nia pana njia. Tanzania bila wananchi waoga wa kudai haki zao inawezekana.

 

 

By Jamhuri