Kasi ya utendaji kazi za Serikali katika awamu hii ya tano, imeanza na dalili njema ya kuwaletea mabadiliko ya kweli ya kurudisha mfumo wa utawala bora ambao utaboresha maisha ya Watanzania, uchumi imara na maendeleo himilivu.

Watanzania wameanza kupiga mayowe na kujijengea hamasa za kufanyakazi na kurudisha matumaini ya kuondoa umasikini na unyonge ambao kwa kitambo kilichopita kilitawala pale watu wachache walipohodhi hatamu za uongozi dhalimu dhidi ya wengi na neema dhidi ya wachache.

Hakika kitambo hicho kilikuwa cha kilio na manung’uniko makubwa kwa wananchi juu ya taratibu za utawala, utendaji na usimamizi wa kazi za taifa usioridhisha; ugawaji wa rasilimali usio eleweka na amani iliyojaa mashaka. Wananchi walibaki tu kukodolea macho watu wachache wasio wazalendo na wageni wa kutoka ughaibuni wakifaidi na kufilisi rasilimali za taifa hili na wananchi wenyewe kubaki wakiwa masikini.

Utaratibu na uendeshaji shughuli za Serikali usioridhisha umejenga dhana inayofikiriwa ndiyo mfumo wa uendeshaji maisha ya wananchi. Mathalan, Serikali kuwaminya walalahoi, wachuuzi na wafanyabiashara wadogo; akina kijungu jiko kulipa kodi kila siku kutokana na kipato chao kidogo mno.

Wakati huohuo serikali inafanya huba ya kutowatoza wala kuwabana wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi ambazo ndiyo kubwa na ni chanzo pia cha uwekezaji mitaji mikubwa inayoweza kuleta maendeleo ya kiuchumi. Ukweli zipo sababu za kufanya hivyo.

Serikali kushindwa kudai kodi inatokana na baadhi ya watendaji na wasimamizi wakuu wa chombo hicho wanapojaza zaidi urafiki, udugu na kuweka mahaba kwa walipa kodi wakubwa kuwapozea. Wengine hufurahisha na kunufaisha nafsi za watu kudai rushwa na kufanya ufisadi.

Matendo hayo yamepewa nafasi kubwa na baadhi ya viongozi wetu na watanzania wenzetu kuanzia ngazi za chini hadi juu za uongozi katika serikali, makampuni, mashirika na katika ofisi binafsi za kutoa huduma. Wenzetu hao kushiriki bila haya wala woga kucheza ngoma ya kuhujumu uchumi wa taifa.

Ngoma hiyo imewatia kilingeni watanzania na kuwaweka chini ya lindi la umasikini na kuwachezesha wale wachache katika uga wa neema na utajiri mkubwa huku ukistawisha na kutunza maisha bora kwao. Ngoma hiyo imetoa matabaka wawili ya watanzania. Tabala la walionacho na tabaka la wasionacho; walalahoi masikini.

Tabaka la wanyonge na maskini limekuwa katika kilio cha muda mrefu hatimaye limepata viongozi wenye uwezo, ujasiri na uthubutu wa kuleta mabailiko ya kweli kwa wananchi wa taifa hili ili nao waweze kujenga na kuwa na maisha bora kwa kila mtu. Nakiri kunena kilo hicho kimesikika mbinguni. Nani anabishaa? 

Hivi ninavyozungumza viongozi wenye sifa hizo wamepatikana katika awamu hii ya tano ya serikali yetu na wanachapakazi bila hofu. Mambo yanayofanywa ya kumtoa nyoka pangoni, kumfunga paka kengele, kusema “NO” badala ya “YES” na kutumbua majibu hayasemeji.

Mamlaka mbalimbali zinatikisika, biashara kadhaa zinaanguka, na walarushwa wanakiona cha mtema kuni. Sina haja kueleza kwa undani kwa sababu nilieleza wiki iliyopita. Leo naangalia baada ya misukosuko hiyo na vigelegele hivyo watanzania tuelekee wapi katika lengo letu la kujenga nchi yetu.

Nadhani tunahitaji kuchapakazi na kutambua kuwa kazi ni uhuru; ndiyo utu, ndiyo maisha na ndiyo heshima ya kila mtanzania na hasa kila mzalendo. Tuelekee vijijini ndiko kwenye maskani yetu ya kuondoa umaskini na njaa na kujenga uchumi imara kupitia kilimo.

Idadi kubwa ya Watanzania iko vijijini na ndiko iliko nguvu kazi kubwa. Kilimo kitastawi na kunawili na mazao ya chakula na fedha yatapatikana na kukuza pato la mtu na kutunisha hazina ya taifa kwa makusanyo ya mapato na kodi. 

Viwanda vyetu vilivyodororeshwa na mabazazi tuvifufue, tuviboreshe na tuanzshe vipya kwa lengo la kujenga Tanzania ya viwanda na kutoa ajira bwerere kwa vijana wetu. Vikao vya vijiweni vitakufa kifo ya mende, chali.

Ukusanyanyi wa kodi, kilimo vijijini, kazi viwandani na utowaji huduma timilifu ukweli kutatukomboa kutokana na omba omba, mikopo yenye masharti na misaada yenye hila  ambayo yanaangamiza taifa letu na kuwa masikini kinyume na utajiri tuliyonao.

Tukumbuke misaada na mikopo vimehatarisha UHURU wetu na kutufanya tuamini kujitawala si kujitegemea bali ni kuwa tegemezi!! Ili hali kujitwala ni kujitegemea. Hili ni kosa na dhambi kubwa kwa watanzania tulilolifanya ndani ya miaka thelathini iliyopita. Utakumbuka mtanzania mwenzatu hivi sasa taifa kubwa duniani Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) linasta/linakataa kutoa uamuzi wa kuipatia msaada wa fedha Tanzania kwa shughuli za maengeleo. Eti “ Tanzania ifuate matakwa ya wazungu na vibaraka wao wanavyotaka katika kuichezea serikali yetu”. Upuuzi huu unafanywa kwa sababu ya kosa letu tulilofanya la kupuuza kutambua kuwa kujitawala ni kujitegemea na kuwaacha baadhi ya viongozi wetu kutukaririsha kuwa kujitawala ni kujitegemeza. Leo wakubwa hao wanaleta chokochoko ya kutaka kuhatarisha amani yetu. TUSIKUBALI. 

Namalizia kusema na nukuu ya maneno yafuatayo, “Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa maendeleo yake”  Azimio la Arusha. Lau kama azimio hilo hatulitaji !! Je, falsafa yake siyo kuntu? 

By Jamhuri