Wauza ‘Unga’, wateka nchi

• Majaji, viongozi wa kisiasa watumia sheria kulinda wauzaji
• Sendeka, Bulaya wataka ibadilishwe haraka, waeleza hatari
• Lema, Kiwelu, Nzowa wawaka, Azzan ataka wauzaji wanyongwe
• Watumiaji walia kubaguliwa, Lukuvi aahidi marekebisho

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inazidi kuwa ngumu na kesi nyingi zinakwama mahakamani kutokana na mfumo mbovu wa kisheria unaotumika kuwalinda wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini.

Majaji na wanasiasa pia wameshutumiwa kutumia nafasi zao kuficha wahalifu wa dawa za kulevya nchini na wakati mwingine kuwezesha wahalifu kukwepa mkono wa sheria.
Uchunguzi uliofanywa kwa muda wa miezi minne sasa, umebaini mfumo wa ukamataji, uandaaji mashitaka, kutoa ushahidi na kuendesha kesi, una matundu mengi yanayotoa nafuu kwa watuhumiwa wa usafirishaji au uuzaji wa dawa za kulevya na hivyo kukwamisha kasi ya kesi mahakamani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka, Kitengo cha Uhalifu Uliovuka Mipaka, Anselem Daniel Mwampoma, amesema badala ya watu kuilaumu ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) au Mahakama kuwa inachelewesha kesi za dawa za kulevya, wanapaswa kuufahamu mlolongo na utaratibu wa kisheria unaopaswa kukamilishwa kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.
JAMHURI limebaini kuwa matakwa ya kisheria ni magumu hali inayokwamisha kukamilisha kesi za dawa za kulevya ndani ya muda mfupi, kwani ushahidi wa kukutwa na dawa pekee hauchukuliwi kama ushahidi mahakamani bali unapaswa kuunganishwa na ushahidi wa mwenendo wa mtuhumiwa.
“Sheria zetu zina udhaifu mkubwa. Kwa mfano, sheria haitambui tiketi zilizokatwa kwenye mtandao,” anasema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Mkadam Khamis Mkadam na kuongeza.
“Kuna mtuhumiwa mmoja tumemkamata na dawa za kulevya mwaka huu, tumekamilisha vielelezo vyote, ila tulipofika mahakamani, Hakimu akakataa kutambua tiketi iliyokatwa kwa njia ya mtandao itumike kuthibitisha kuwa mtuhumiwa alisafiri nje ya nchi pamoja na hati yake ya kusafiri kuonyesha hivyo, na hivyo akatupilia mbali kesi.”
Mbunge wa Arusha (CHADEMA) na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema, ameliambia JAMHURI kuwa sheria ya kudhibiti dawa za kulevya ya Kenya ni nzuri ikilinganishwa na ya Tanzania kwani mtu akikutwa analima bangi kwenye shamba lake, shamba husika linataifishwa hivyo Tanzania inapaswa kuiga mfano huo.
“Hata hivyo, tatizo ni kubwa zaidi ya sheria. Nchi ina ombwe la uongozi. Rais alisema anayo majina ya wauza unga ila naona anaogopa kuyataja, sasa unadhani DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi) yeye atathubutu kuwataja kama Rais anawaogopa?” Alihoji Lema. Miaka minne iliyopita, Rais Kikwete alisema anayo orodha ya wauza unga, lakini hadi leo hajawahi kuitaja hadharani orodha hiyo.
Grace Kiwelu, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), alihofu kuwa huenda orodha ya majina ya wauza unga aliyonayo Rais ni ya vigogo wenzake. “Iwapo Rais angetaja hayo majina na kama wako karibu naye akawaweka pembeni, suala hili lingepata ufumbuzi wa kudumu. Wengine wangeogopa. Tatizo leo kila mtu anaona hakuna tabu, taifa na vijana wetu wanazidi kuangamia,” amesema Kiwelu.
Mwampoma anasema ukichanganya mlolongo wa kisheria na ufinyu wa bajeti, kesi za dawa za kulevya sawa na zilivyo kesi nyingine huchelewa kukamilisha uchunguzi na hii ina madhara makubwa kwani mashahidi huanza kukata tamaa na wengine hufariki dunia kabla hawajatoa ushahidi mahakamani.
Uchunguzi unaonyesha kuwa mlolongo wa kisheria hutoa mwanya kwa watuhumiwa au ndugu zao kutorosha mashahidi, kuhonga mashahidi, kutishia maisha ya mashahidi na wakati mwingine baadhi ya mashahidi hukata tamaa na kukataa kwenda kutoa ushahidi mahakamani.
Pia kutokana na kutokuwapo sehemu nzuri za kuhifadhi ushahidi, vielelezo hupoteza ubora wake baada ya mwaka mmoja au miaka miwili na vikipimwa tena hukosa ubora uliothibitishwa na Mkemia Mkuu awali hivyo hutupwa kwa hoja kuwa si ushahidi usiotiliwa shaka mahakamani.
Godfrey Nzowa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kuleya (ADU), ameliambia JAMHURI kuwa ingawa ubora wa vielelezo unaweza kupotea, tatizo kubwa ni wasimamizi wa sheria kuliko ubovu wa sheria yenyewe.
“Mwaka 2012, Mahakama ya Rufaa ilitoa hukumu na kumwachia huru Abuu Omary kule Mtwara kwa maelezo kuwa ingawa amekutwa na dawa za kulevya, ushahidi umeziba kila kona na kuthibitika, lakini RCO wa Dar es Salaam, [Charles] Kenyela hakwenda kutoa ushahidi, eti ‘chain of custody’ (mtiririko wa kutunza ushahidi) ulikatika,” anasema Nzowa.
Anasema watuhumiwa wanatozwa faini ndogo ya Sh milioni 10, wakati sheria iko wazi kifungu cha 16 kinataka mtu aliyetiwa hatiani kufungwa maisha jela, faini ya Sh milioni 10 au mara tatu ya thamani halisi ya dawa alizokutwa nazo, lakini hili wasimamizi wa sheria ikiwamo mahakama hawalifanyi.

Rushwa yatajwa kukwamisha harakati

Christopher ole Sendeka, Mbunge wa Simanjiro (CCM), ameliambia JAMHURI kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Sendeka anasema mawakili wanachangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha kesi mahakamani kwa kutumia mbinu na uchochoro unaopatikana kwenye sheria ya sasa ya mwaka 1995.
“Tatizo ni kubwa, mawakili, wapelelezi, majaji, waendesha mashitaka na wengi wanaohusika wanaujua udhaifu wa sheria iliyopo. Matokeo yake, wanatumia udhaifu huu kupoteza ushahidi au kuchelewesha kesi ushahidi ukapotea wenyewe. Hii ni hatari kubwa na vita hii itakuwa ngumu iwapo sheria itaendelea kuwa kama ilivyo. Ni lazima sheria hii ibadilishwe haraka,” anasema Sendeka.
Sendeka amesema sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa mamlaka makubwa kwa Kamishna wa Dawa za Kulevya na nafasi hii akiipata mtu asiye mwadilifu anaweza kuitumia kujikusanyia rushwa. Ibara ya 27 (1) (b) inatamka kuwa Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya pekee ndiye anayepaswa kuthamanisha dawa zilizokamatwa.
“Nani ana-set (anayeweka) bei? Ni wapi kuna soko halali kiwango kinachoweza kutumika kama bei ya soko katika kutafuta thamani halisi ya dawa zilizokamatwa na ni wapi soko lipo? Vigezo vya bei atakavyovitumia Kamishna kwa ajili ya kutoa dhamana au kumnyima mtuhumiwa ni vipi?
Kamanda Mkadam amekiri kuwa kigezo cha thamani kina utata mkubwa kwani hakuna soko halali la dawa za kulevya duniani na hivyo akasema ingawa sheria haijabadilishwa kwa sasa wanatumia zaidi uzito wa dawa zilizokamatwa badala ya thamani. “Ukiacha thamani kushawishi vijana kujiingiza katika janga hili, hakuna soko tunaloweza kulitumia kupima thamani halisi. Naamini sheria ikibadilishwa itaondoa upungufu huu,” anasema.
Sendeka aliongeza pia: “Hivi kupungua kwa thamani ya dawa za kulevya kunapunguza athari na kuhalalisha kama thamani ni ndogo maana yake ni halali au kosa dogo? Ukimpapasa mwanamke kwa nia ya kumbaka na kumwingilia, bado kosa lipo paleple… sheria hii inatengeneza njia nyingi za kuchomokea.”
Amekwenda mbali zaidi na kusema inawezekana hii sheria “waliiandika wauza unga” ikapelekwa bungeni kupiga mihuri tu. “Maana ukiitazama kwa jicho jingine unajiuliza iwapo wanaonufaika na biashara hii si walioshiriki kikamilifu katika uandishi wa muswada na hatimaye utunzi wa sheria hii,” anasema kwa masikitiko na kuongeza: “Nashukuru Mungu sikuwa sehemu ya utungaji wa sheria hii ya hovyo inayotengeneza mazingira ya watu wanaoharibu maisha ya vijana wetu.”
Sendeka anapendekeza: “Adhabu iwe kifungo cha maisha, isiwepo nafasi ya faini. Hii itawafanya wale wengine wajue dhamira ya dhati ya jamii kukomesha hiyo biashara haramu.”
Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), anasema pamoja na kuwasilisha Maelezo Binafsi bungeni, Aprili, mwaka jana yaliyosheheni taarifa lukuki, Serikali imekaa kimya bila kuyatolea majibu.
“Katika maelezo hayo (tunayo), nilitaka itungwe sheria mpya itakayodhibiti dawa za kulevya nchini na kutoa adhabu kali kwa wanaoshiriki biashara hii, lakini hadi leo sijapata majibu. Binafsi naamini njia sahihi ya kupambana na tatizo hili ni kutunga sheria kali inayoweka udhibiti na si vinginevyo, lakini kuendelea na sheria ya sasa ni hatari,” anasema Bulaya.
Anasema kwa makusudi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka imekuwa ikitumia vibaya sheria hii kwa kufungua na kufuta mashitaka dhidi ya watuhumiwa kisha kuwafungulia kesi zisizokuwa na adhabu kubwa.
Bulaya ametoa mfano wa kesi namba CC 433/2009 iliyohusisha Jamhuri dhidi  ya Shirima, kuwa mtuhumiwa alifunguliwa kesi katika Mahakama ya Kisutu chini ya kifungu 16 (1)(b)(i) kinachotoa adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka 20 hadi maisha, lakini mtuhumiwa huyu aliyekamatwa na kilo moja ya heroin yenye thamani ya Sh milioni 18, alibadilishiwa mashitaka thamani ya dawa ikashuka hadi Sh milioni 4 na kushitakiwa chini ya kifungu cha 12(d) kinachotoa faini ya Sh milioni 1 au kifungo kisichozidi miaka 20. Mtuhumiwa alilipa faini ya Sh milioni 1 na kuachiwa huru.
Ofisi ya DPP pamoja na kupelekewa maswali Septemba 3, mwaka huu, hadi wakati tunachapisha habari hii walikuwa hawajatoa majibu. Hata DPP aliyeteuliwa Biswalo Mganga, pamoja na kuwasiliana naye mara kadhaa, ahadi za kutoa majibu hakuzitekeleza.
Mgongano huu wa vifungu unatoa fursa kwa waendesha mashitaka, majaji na mahakimu kutoa hukumu zisizo kali kwa kiwango kinachokwaza nia ya watunga sheria, hivyo Bulaya anasema sheria inapaswa kubadilika na kutoa adhabu ya kifungo pekee bila fursa ya faini.
Idd Azzan, Mbunge wa Kinondoni aliyepata kutuhumiwa kuwa anajihusisha na biashara ya kuuza dawa za kulevya (tutachapisha mahojiano naye kwa kina), ameliambia JAMHURI kuwa tuhuma hizo dhidi yake ni za kisiasa zaidi, na akaunga mkono juhudi za Mbunge Bulaya kwa kusema sheria ni legelege.
“Esther Bulaya aliwahi kutoa hoja binafsi bungeni, kutaka sheria zibadilishwe. Nikubaliane na wazo la Ester Bulaya adhabu iwe kifungo pekee, kwa sababu ukimwambia faini [muuza ‘unga’] atalipa, maana anazo hela huyu. Hawa wasafirishaji na wauzaji wakifungwa, wakitoka watakuwa hawana hamu tena na biashara hiyo na wakiona mwenzao ameadhibiwa vile, nao watakosa hamu.
“Kesi ikisikilizwa ushahidi ukamtia mtu hatiani, adhabu iwe ni kunyongwa au kufungwa maisha. Kutokana na adhabu kali ya kosa la mauaji, kwa sasa ugomvi ukitokea mtu anajitenga. Adhabu ikiwa kali watu wataogopa kujihusisha na dawa za kulevya maana watajua adhabu yake ni kunyongwa tu,” anasema Azzan.
Pia anatilia shaka uendeshaji wa kesi za dawa za kulevya mahakamani: “Uendeshaji wa hizo kesi pia ni tatizo. Mtu amekamatwa mnaona pipi zimetokea tumboni mwake mbele ya mashuhuda, lakini kesi inachukua muda mwingi sana kumalizika. Mahakama ihamie eneo la tukio, mtu akimaliza kuzitoa hizo pipi, ahukumiwe aende jela au anyongwe mara moja. Kuwe na uharakishaji wa kesi hizi ambazo tayari vidhibiti na ushahidi vipo.”
Kutokana na ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya, baadhi ya watu wamekuwa wakitaka iwepo Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya nchini kwa nia ya kuharakisha kesi. Hata hivyo, Azzan hakubaliani na wazo la mahakama maalum kwa ajili ya dawa za kulevya kwani likikubaliwa hata watuhumiwa wa rushwa, wezi wa kuku, mauaji, na nyingine nao watataka wawe na mahakama zao. “Naamini mahakama zilizopo zinaweza kushughulikia suala hili. Majaji ni wengi, mawakili ni wengi. Ni jukumu la mahakama kuendesha kesi bila kuzichelewesha. Hata ukianzisha Mahakama ya Dawa za Kulevya, tatizo linaweza kuwa lilelile kinachotakiwa ni kuharakisha kesi.
“Mtu anashuka airport, kamamatwa [anazitoa kwa njia ya haja kubwa dawa] zimeonekana, kitu gani kinachelewesha? Kama anahitajika Mlinzi wa Amani awepo, aende mbele ya mahakama, hukumu inatoka mchezo unakwisha. Kuna wengine wako ndani, wengine ujanja ujanja wanapata dhamana wako nje. Kasi ya hukumu itaongeza woga,” anasema Azzan.
Job Ndugai, ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania anasema kitendo cha Sheria kumtaka Kamishna wa Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya pekee ndiye asaini cheti cha thamani ya dawa za kulevya zilizokamatwa ni upungufu mkubwa kisheria.
“Hiyo sheria ilitungwa vibaya. Yapaswa kufanyiwa marekebisho kwani huyu wa juu kama hayupo wa chini yake afanye kazi kama kawaida. Hata serikalini Waziri kama hayupo Naibu Waziri anafanya kazi,” anasema Ndugai.
Madhara ya kifungu cha 27 cha sheria hii kinachomtaka Kamishna pekee ndiye asaini thamani ya dawa za kulevya zilizokamatwa, kilisitisha kesi za dawa za kulevya kubwa nchini kwa mwaka mzima kati ya Agosti 2013 hadi Agosti 2014 ambapo watuhumiwa waliendelea kukaa ndani na matukio ya dawa za kulevya yakaongezeka kutokana na kutokuwapo hukumu yoyote ambayo ingewaogofya wenye nia ya kufanya biashara hizo.
Hii ilitokana na aliyekuwa Kamishna wa Tume Christopher Shekiondo kustaafu kwa mujibu wa sheria na nafasi yake ikawa inakaimiwa na Aida Tesha, ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kusaini vyeti vya thamani.
Mwanasheria Deus Kibamba, ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa Tanzania (TCIB), amesema sheria hiyo ilivyo inamzuia mtu mwingine yeyote asiye Kamishna kusaini cheti cha thamani ya dawa za kulevya na akisaini mtuhumiwa atashinda kesi kutokana na saini hiyo kutokuwa na mamlaka kisheria.
Katika kuthibitisha hilo, Kamishna wa Tume aliyeteuliwa mwezi Mei mwaka huu na kuingia rasmi ofisini Agosti kushika wadhifa huo, Kenneth Kaseke, ameliambia JAMHURI kuwa mara tu alipoingia ofisini amesaini vyeti vya thamani kwa kesi 50 zilizokuwa mezani kwake kwa mwaka mmoja ambao Tesha alikaimu nafasi hiyo.
“Mimi nimesaini vyeti 50, kimsingi siwezi kukupa majina kwani itakuwa ni kuingilia mwenendo wa kesi Mahakamani, lakini sitaki matatizo yaonekane kuwa ofisini kwangu. Mimi natekeleza wajibu wangu, na wengine watekeleze wao,” alisema Kaseke.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa hadi mwishoni mwa Agosti mwaka huu, zilikuwapo kesi 140 za dawa za kulevya nchi nzima zilizokuwa zinafanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola kabla ya kufikishwa mahakamani.
Taarifa kutoka ndani ya Tume zinaonyesha kuwa Dar es Salaam ilikuwa na kesi kubwa  71, Arusha kesi 25, Kilimanjaro 22, Pwani (6), Tanga 3, Morogoro (5), Mbeya (3), Lindi (1), Mwanza (1), Dodoma (1) na Manyara (2).
Aliyekuwa mtumiaji wa Dawa za Kulevya, Very Kunambi, ameliambia JAMHURI kuwa anatamani sheria ingekuwa kali ikawafilisi wote wenye kufanya biashara hii na ikibidi wauawe.
“Nimetumia dawa za kulevya kwa miaka 15 nikitumia heroin… nilianza kutumia bangi mwaka 1985 nikiwa kidato cha pili. Hasara niliyopata, sitakaa niisahau. Nasema yeyote anayefanya biashara hii, sheria inapaswa kumbana ikibidi aondoshwe uraiani,” anasema Kunambi.
Hata hivyo, Kunambia anasema waliokuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanapaswa kusaidiwa badala ya kushutumiwa. Anasema hasara waliyokwishapata ni kubwa na kuendelea kulaumiwa kutawafanya wajione ni binadamu wa daraja la pili na hii itaifanya vita dhidi ya dawa za kulevya kuwa ngumu.
Godfrey Teu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Watumiaji wa Dawa za Kulevya Tanzania (TanPUD), anasema tatizo linalowapata watumiaji wa dawa za kulevya ni kwamba sheria inatumika kwa ubaguzi.
“Vita hii ni ngumu mno. Tatizo ni kwamba wakati polisi wanakimbizana na sisi watumiaji wadogo, watu wakubwa wanapelekewa dawa hadi nyumbani kwao na hawafuatwi kukamatwa. Tunasema sheria iwe sawa kwa wote na hili ni janga la kitaifa, ni lazima tuwe na mpango wa kudhibiti hali hii,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, anayesimamia Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya amesema kilio cha wananchi kimekuwa kikubwa na Serikali tayari inalifanyia kazi suala la kubadili sheria.
“Mwaka jana tumebadili (tumefanya marekebisho ya) sheria sasa inataka watu watakaokamatwa na dawa za kulevya wafungwe hadi maisha. Sheria yenyewe imefikia ngazi ya Baraza la Mawaziri, si muda mrefu itatungwa sheria itakayokuwa haina mianya yoyote na kuruhusu upuuzi unaoendelea sasa na itafikishwa bugeni wakati wowote kuanzia sasa,” amesema Lukuvi.
Kati ya mapendekezo yaliyomo ndani ya sheria hiyo ni kuondoa mwanya wa kuwatoza faini wauza dawa za kulevya na sheria kutamka kifungo peke yake. “Hawa wakubwa hawataki kufungwa. Tukiondoa dhana ya faini, watajua kuwa atakayekamatwa na dawa za kulevya na ikathibitika mahakamani hatima yake itakuwa ni kifungo, wataacha hawa, wataogopa,” amesema Lukuvi.
Uchunguzi huu umefanywa kwa udhamini wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa (UNDOC), na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCC).
Mwisho 

Ufunguo
• Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 1995, inataka anapokamatwa mtuhumiwa wa dawa za kulevya kuzihusisha taasisi nyingi kukamilisha ushahidi ikiwamo polisi wanaofanya ukamataji na uchunguzi, Wizara ya Afya ambako Mkemia anapaswa kupima na kuthibitisha iwapo ni dawa za kulevya au la, Idara ya Uhamiaji kujiridhisha iwapo mtuhumiwa alisafiri kihalali nje ya nchi na Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya, inayopaswa kuthamanisha kiasi cha dawa zilizokamatwa.
• Katika kukamilisha ushahidi, sheria inataka kuthibitishwa pasipo shaka kuwa mtuhumiwa alikamatwa, aliyekamatwa ndiye aliyepekuliwa na kukutwa na vitu vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya vikiwa ama kwenye mizigo au maungoni mwake na vitu hivyo vinapaswa kuthibitishwa na Mkemia Mkuu iwapo ni dawa za kulevya na ni aina ipi.
• Utaratibu wa kuthibitisha kuwa mtuhumiwa ana dawa za kulevya maungoni mwake unahusisha kupiga picha ya mionzi (x-lay) na wakati mwingine kumfanyia upasuaji mtuhumiwa kutoa dawa tumboni. Baada ya kuthibitishwa na Mkemia Mkuu, Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya inapaswa kuthamanisha dawa hizo. Hatua hizo zikiishakamilika, mtuhumiwa anapaswa kuandika maelezo yatakayoambatanishwa na vielelezo kwa ajili ya kutolewa kama ushahidi mahakamani.
• Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Januari 1, 1967 nayo inataka mtuhumiwa anapofikishwa mahakamani kusomewa maelezo ya awali na kama ushahidi haujakamilishwa kila baada ya wiki mbili awe anafikishwa mahakamani.
• Pia sheria ya ushahidi ya Mwaka 1967 inataka dawa alizokutwa nazo mtuhumiwa kufanyiwa uchunguzi wa awali kisha zifanyiwe uchunguzi wa kuthibitisha kuwa ni dawa za kulevya kweli, na baada ya hapo zifungwe na kurejeshwa kwenye mikono ya waendesha mashitaka kwa ajili ya kuhifadhiwa kama kidhibiti zikiwa zimefungwa kwa rakili.
• Mwenendo unaozungumzwa ni kuwapo wa taarifa zisizotiliwa shaka kuwa mtuhumiwa alisafiri nje ya nchi, hii ni kwa kuangalia hati yake ya safaria na viza aliyopewa na uhamiaji, kisha awepo shuhuda aliyemwona mtuhumiwa kama alitolewa dawa za kulevya tumboni azione zikitolewa na athibitishe hivyo mbele ya mahakamani.
• Mtu mwingine anayepaswa kuthibitisha iwapo mtuhumiwa alisafiri kweli ni kampuni za simu za ndani na za kimataifa kwa kuchunguza simu ya mtuhumiwa iliwasiliana na nani kabla ya kuondoka nchini na wakati yuko nje ya nchi au wakati anarejea nchini kuthibitisha kuwa yalikuwapo mawasiliano yenye kutia shaka.