Wavamizi wa ardhi wasifumbiwe macho

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kubomoa nyumba ambazo zimejengwa kwenye maeneo ya wazi na viwanja vilivyovyamiwa na watu wasio wamiliki halali wa viwanja hivyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alfayo Kidata, amesema watu wote waliovamia maeneo hayo nchi nzima watabomolewa bila kujali mhusika ni nani.

Amesema kazi hiyo ya kubomoa majengo hayo yaliyojengwa kinyume cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, itakuwa ya kudumu na itafanyika kwa awamu tofauti na kwamba imeanza jiji la Dar es Salaam ikiwa ni awamu ya tatu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita nyumba nne zilizojengwa katika maeneo yaliyovamiwa na watu ambao si wamiliki halali wa viwanja hivyo, zimebomolewa kwa usimamizi wa maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na ofisi ya Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni.

Nyumba mbili zilizobomolewa ni namba 507/2/1 na namba 507/2/2 zilizopo Mikocheni ‘B’ ambako kati ya nyumba zilizovunjwa, moja ilijengwa katika kiwanja kinachomilikiwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daud Balali.

Na nyumba nyingine ni namba 67 Block C na 1330 Block G, zote zikiwa eneo la Tegeta. Nyumba hizo zote ni miongoni mwa nyumba zilizojengwa kinyume na kifungu namba 175 (1) cha sheria hiyo.

Wavamizi wengi wa maeneo ya wazi wamekuwa wakitumia uwezo wao wa kifedha kupora ardhi inayomilikiwa kihalali na wananchi wengine, na pia kuvamia maeneo ya fukwe za bahari kinyume na sheria ya ardhi.

Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa zaidi ya viwanja 100 vya wazi vimevamiwa hapa jijini, na kuwataka wavamizi hao kubomoa majengo yao na kuyarejesha maeneo hayo. Lakini hadi sasa wavamizi wa maeneo hayo ya wazi, kwa kutumia jeuri ya fedha waliyonayo ama urafiki wao na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wamekaidi agizo hilo lililotolewa na wizara hiyo.

Mapema Januari mwaka huu aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, alisimamia ubomoaji wa jengo la mgahawa lililojengwa kinyume cha sheria ndani ya eneo la wazi la bustani ya Samora na Kampuni ya Easy Payment Limited.

Jengo hilo lililokuwa likijengwa bila vibali vya ujenzi nyakati za usiku na siku za mapumziko tu lilikuwa na baraka zote za uongozi wa Manispaa hiyo huku viongozi hao kila siku wakipita jirani na eneo hilo.

Sisi JAMHURI tunasema operesheni hii ya kuyakomboa maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa kinyume na Sheria za Ardhi ikiwamo Sheria namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007, iwe ya kudumu kwa lengo la kukomesha uhuni huu.

Sheria imefafanua vizuri kwamba maeneo yote ya wazi ni kwa ajili ya matumizi ya umma, na suala la kujenga majengo ya biashara au makazi ndani ya maeneo hayo hairuhusiwi.

Tunasema migogoro mingi ya ardhi nchini chanzo chake ni rushwa iliyokithiri kwa baadhi ya watumishi wa Wizara ya Ardhi na wale walioko katika Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.

Watumishi hawa kwa tamaa ya fedha wamejiingiza katika uhuni wa kutisha kwa kugawa kiwanja kimoja kwa watu watano tofauti na wote wanapewa barua ya toleo au hatimiliki na kuwaingiza wananchi kwenye migogoro ya ardhi.

Pia baadhi yao wamethubutu kuuza maeneo ya wazi kwa kutumia mikataba ‘feki’ inayopewa majina ya uwekezaji kwa madai ya kuyaendeleza, jambo linaloonekana halina ukweli wowote ule.

Wanaoendekeza uhuni huu ni baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali na halmashauri. Mfano hai ni kama walivyofanya viongozi wa Manispaa ya Ilala jijini hapa, kuuza eneo la wazi kwa kampuni ‘hewa’.

Tunasema kazi ya kuyakomboa maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa hapa nchini haipaswi kuambatana na ubabaishaji ambao umedumu kwa kipindi kirefu na kuzidisha machungu kwa wananchi, huku baadhi yao wakipoteza maisha kwa migogoro isiyokuwa na ulazima wa kuwapo.