Hata kama huamini juu ya uchawi na ushirikina, huwezi kuishi ndani ya jamii nyingi za Kiafrika na usisikie taarifa juu ya masuala haya. Miongoni mwa kabila la Wazanaki imani hizi zipo.

Ilikuwa desturi anapougua au kufariki mtu jambo la kwanza jamaa zake wanalofanya ni kwenda kwa mpiga ramli kutafuta mchawi aliyemdhuru jamaa yao. Sina hakika ni kwa kiasi gani hizi imani zipo leo hii, lakini nafahamu kuwa wapiga ramli bado wapo na wanashiriki kutoa maoni yao ya kitaaluma kwa wateja wao kuhusu uchawi na ushirikina.

Miaka kadhaa iliyopita baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Butiama walimtimua mtu, ambaye nitamuita Pepe, akituhumiwa kufuga na kufanya biashara ya misukule. Inaaminika misukule ni binadamu ambao huzikwa wakiaminika wamekufa, lakini hupewa uhai kwa njia za kichawi na hufanyishwa kazi kwenye mashamba na pia kutoa huduma kadhaa za weledi.

Miaka ya nyuma nilisimuliwa kisa na mfanyakazi wa Hospitali ya Butiama ambaye mfanyakazi mwenzake aliyekuwa daktari alifariki wakati huo. Hakuwa amefariki dunia, aliniambia, ila alichukuliwa katika mazingira hayo ya kichawi na wakati huo alikuwa mganga mkuu kwenye hospitali iliyopo kwenye ulimwengu wa misukule. Hospitali hiyo ilikumbwa na upungufu wa wafanyakazi na “mchawi” aliyetimuliwa ndiye alisadikiwa kupeleka watu wa kuziba nafasi zilizo wazi.

Pepe alijijengea desturi ya kufanya shughuli za kawaida katika mida ambayo haikuonekana kuwa ya kawaida kwa wengine. Wanakijiji wenzake walipojiandaa kulala usiku yeye ndiyo kwanza aliwaelekeza mafundi kuendeleza ujenzi wa nyumba yake. Kwa wanaoamini uchawi ni mida ya usiku ndipo wachawi na wale wanaoaminika kuwa wasaidizi wao wakuu, yaani fisi na bundi, wanakuwa na pirikapirika nyingi na mizunguko ya huku na kule.

Kwa tathmini yangu, Pepe, ambaye alikuwa pia mfanyabiashara, alikusudia kusimamia kwa karibu ujenzi wa nyumba yake na kwa vile alikuwa na mizunguko mingi mchana, hakupata muda wa kufanya hivyo mpaka ilipofika usiku.

Nilipata kuzungumza na fundi mmojawapo aliyeshiriki kwa kipindi kifupi kujenga nyumba ya Pepe usiku na alinithibitishia kuwa ni muda bora zaidi kujenga nyumba kuliko mchana kwa sababu wakati huo wale wapiga porojo wa mchana ambao hupunguza kasi ya kazi huwa wamelala na fundi anaweza kuendelea na kazi pasipo kukatishwa na mazungumzo. Huyo fundi aliacha ujenzi wa nyumba ya Pepe baada ya kupata onyo kali kutoka kwa wazee wa kimila (abhanyikura), akakatazwa kushiriki ujenzi ule wa usiku.

Baada ya hapo ‘abhanyikura’ walipeleka mwito kwa Pepe kumtaka aeleze sababu ya kujenga nyumba usiku. Alielekezwa kuendeleza ujenzi wake mchana kama wengine na akafuata kwa muda, lakini baadaye akarudia tena ujenzi wa usiku. Alipata mwito mwingine kuonana na ‘abhanyikura’, lakini safari ya pili badala ya kuitikia mwito, si tu hakuhudhuria kikao kilichoitishwa kwa ajili yake, bali akatuma onyo kwa wazee kuwa wakiendelea kumfuata fuata atawafungulia mashitaka mahakamani na wangeweza kujikuta jela. Kama hii ni kweli, basi alikuwa amefanya kosa kubwa sana. Wazee wa jadi ni taasisi muhimu sana ya kimila. Ni dhahiri kuwatishia huku kuliibua tafrani kubwa zaidi.

‘Abhanyikura’ ni kama serikali, na pengine hata zaidi. Serikali itakuvumilia kuongea na mtuhumiwa – hata wa uhaini, lakini hawa wazee ni tofauti. Pepe alikuwa anachochea moto.

Kwa kulipiza kisasi ‘abhanyikura’ wakaanza kuweka vikwazo. Hakuna aliyeruhusiwa kuongea naye. Yeyote ambaye angekiuka hiyo amri angeweza kutozwa faini, aghalabu ng’ombe mzima, kutegemea na mazingira ya ukiukwaji uliyofanyika. Athari za ukiukwaji wa aina hii kwenye mazingira ya mjini yanaweza kuwa ni madogo sana, lakini kwenye kijiji, ambako ushirikiano na wengine ni muhimu katika kila nyanja, vikwazo huwa na athari kubwa mno. Nilipata taarifa kuwa mmiliki mmoja wa duka alipewa onyo kali na wazee wa kimila baada ya kumuuzia Pepe vocha za simu.

“Angekubali tu amri ya wazee, akakubali kulipa faini, na kuendelea kujenga mchana, angekuwa bado yupo,” alisema fundi. Kusingezuka kisingizio cha kumfukuza. Aliwadharau wazee akawapa mwanya wale waliyokuwa wanamshuku kwa uchawi kufanya njama za kumtimua kijijini.

Ukichukulia kuwa mtu yeyote anayeaminiwa kuwa ni mchawi hadhaniwi kuwa na woga wa aina yoyote na huaminika ni mkatili mmoja ambaye hurandaranda usiku akitafuta binadamu wa kuwadhuru akitumia fisi kama usafiri wake, mimi nilifikia uamuzi kuwa Pepe hakufanana asilani na taswira hii.

Jioni moja, nilikuwa naendesha gari nikitoka Musoma na nilisimamishwa na kundi la watu waliokuwa wamesimama pembeni ya gari nyingine ndogo. Miongoni mwao alikuwa Pepe. Alinijulisha kuwa walikuwa wakielekea Musoma, lakini baada ya kukuta mawe makubwa yameegeshwa katikati ya barabara niliyopita mimi muda ule ule kabla ya kuwafikia, waligeuza gari haraka wakihofu kushambuliwa na majambazi wenye silaha.

Niliwaambia sikuona mawe yoyote barabarani na kuongeza kuwa yawezekana kuwa baada ya wao kugeuza gari na “majambazi” nao wakatawanyika wakihofia nia yao mbaya imegundulika.

Kutokana na maelezo yangu baadhi ya abiria wa ile gari walifarijika na wakaanza jitihada za kumshawishi dereva apite pale pale kwenye eneo la hatari na kuendelea na safari kwenda Musoma. Mtu pekee aliyeamua kuwa kuendelea na safari ya Musoma ni hatari alikuwa mtuhumiwa wa uchawi, Pepe. Aliniomba lifti tukarudi naye Butiama.

Nilivyoona mimi, iwapo Pepe ndiye alikuwa mfano halisi wa mchawi, basi viwango vya uchawi vilikuwa vimeporomoka sana. Iweje aliyetuhumiwa uchawi akawa mwoga kuliko wale waliomtuhumu kuwa mchawi?

2403 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!