Sina kasi na viwango, ‘that’s life’

Nalia machozi yanimwagika. Mwili umechoka; umenyong’onyea kuondokewa duniani na Mnyamwezi mmoja msomi, mwanasheria, aliyeendelea na mwenye hadhari na ulimi wake wakati akiwa katika maongezi.

Ni Mnyamwezi mpenda watu, mchapakazi, mvumilivu na mwenye msimamo katika kutetea hoja njema au mbaya. Mjanja na hodari kuruka viunzi hasi au chanya katika hoja inayohusu maendeleo ya nchi. Ni mwenye msimamo na asiyeyumbishwa na mbabe yeyote nchini. Huyu ni Samuel John Sitta, mtoto wa Kitanzania.

Samuel ametoka kwenye mifupa ya watu, nao ni marehemu mzee John Sitta na Hajjat Zuwena bint Saidi Fundikira, wenye asili ya kabila la Kinyamwezi. Alizaliwa Desemba 18, 1942 na kulelewa katika makuzi ya kijijini na mjini. Amefariki dunia Novemba 7, 2016 nchini Ujerumani na kuzikwa Jumamosi, Novemba 12, 2016 kijijini kwake Mwenge, Urambo mkoani Tabora.

Mtani wangu, mkubwa wangu na mheshimiwa kiongozi wangu, amefariki dunia kutokana na maradhi ya saratani ya tezi dume. Hakupenda kuifariki dunia, lakini palikuwa hapana budi kwa sababu kifo ni faradhi. Kimeumbwa. Wewe na mimi tutapita njia hiyo. Hakuna kiumbe chochote kitakachokwepa kifo.

Naungana na Wanyamwezi na Watanzania wote nchini katika maombolezo ya kiongozi wetu shupavu na mwingi wa falsafa yake ya ‘Kasi na Viwango’, ambayo imeacha simulizi nchini na sasa inawashawishi wasanii kuitia katika tungo zao na waandishi kuweka vitabuni.

Bado tukiwa katika siku 40 za maombolezo, natoa mkono wa tanzia kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu Samuel Sitta na kumwomba Mwenyezi Mungu ampokee kiumbe wake na kuiweka roho yake peponi. Samuel ametoka mavumbini na amerudi mavumbini. Ihidimiwe.

Samuel Sitta hakupenda na sisi hatukupenda tufarakane. Alitupenda na tulimpenda. Mwenyezi Mungu amempenda zaidi ya sisi na amemchukua. Aliyoyatenda duniani ndiyo amali yake na itahesabiwa na kupimwa siku ya ufufuo wake mbele ya Muumba wake.

Uliyotenda duniani tumeyaona na kuyazingatia. Dhahiri leo tunazungumzia utu, uungwana na ukarimu wako kuanzia kwa watoto hadi kwa wazee. Sisi hatuna cha kukulipa zaidi ya kusema ‘asante sana.’ Mwenyezi Mungu ndiye mwenye malipo kamili na rehema kwako. Amini.

Nakuthibitishia mtani wangu, kwamba viongozi wenzako, watumishi wa umma, wasomi na wanafunzi, wafanyakazi na wakulima, vijana na wazee walifurahishwa mno na utendaji kazi wako na sasa wana huzuni na masikitiko, na hasa wakulima wa tumbaku wa Urambo ulivyowapaisha kibei.

Ni kweli mzigo mzito mpe Mnyamwezi. Wewe ulikubali kubeba mizigo mizito ya huduma na hisani hata pale ilipokuelemea bado uligangamala kubeba. Kumbuka yalikupata Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kupingana na ufisadi nchini, kulumbana na UKAWA katika kanuni na demokrasia, kupitisha Katiba Pendekezwa, kufyekwa kugombea urais (CCM ) na mengi mengineyo.

Mengi yameandikwa kwenye vyombo vya habari na kusimuliwa mitaani, majumbani na kwenye majumba ya ibada kuhusu utu na imani yako. Sina uhakika kule Urambo kwenye matambiko yenu kukoje! Hata hivyo, nitamtafuta Profesa Juma Athumani Kapuya anipe majibu. Tambua hisani zako bado ni picha vichwani mwetu na  zitadumu.

Hayati Samuel Sitta (74) mwaka 1942 hadi 2016 duniani ni mifupi kinyume na mapana yake katika utu na uungwana wako. Kwa sisi uliotuacha: mama mzazi, mke wako, watoto wako, ndugu, marafiki na watani wako tunashindwa tukuweke daraja gani ili iwe kifu yako na yetu. Je, inatosha kusema ‘that’s life?’

Kwa leo, yatosha kusema niliyosena lakini machozi na kwikwi hazinishi nikikumbuka hisani zako lau kama hisani imepotea duniani. Penye majaaliwa nitasema kwenye arobaini yanayosemwa ya kukuezi kweli wanakuenzi au ndiyo THAT’S LIFE?