Kwa kawaida, Mtanzania ninayemjua mimi, kalelewa katika mazingira ya kuhoji kila kitu hata ambacho jibu lipo wazi, atahoji ili apate jibu la pili ambalo halina tofauti na jibu la kwanza, Mtanzania anaitumia vizuri demokrasia hata kama anajua wazi kuwa inamaliza na kumpotezea muda. Huyu ndiye Mtanzania anayeweza kuuliza mvua wakati wingu analiona.

Siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la sheria mbalimbali  zinazotumika hapa nchini, zipo zilizopitwa na wakati na zipo  zilizofufuliwa na zipo zilizoongeza makali yake lakini pia zipo zilizokuwapo lakini hazikuwa zikitumika kwa sababu ya ubinadamu tu, ubinadamu wa kiongozi husika au upungufu wa watendaji.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, sheria zinatungwa na Bunge la nchi yetu, ikishatungwa inatiwa saini na kiongozi mkuu wa nchi na kisha kuchapishwa katika Gazeti la Serikali, hili Gazeti la Serikali lipo na linagawanywa kwa gharama kidogo na kuonekana katika mitandao ya kijamii, wengi wetu hatujawahi kuliona na hasa vijijini.

Kwa umri wangu, nimewahi kuliona Gazeti la Serikali mara chache, lakini pia sikulisoma ipasavyo ili nizijue sheria chache ambazo zipo katika gazeti hilo, huu ndiyo utaratibu wetu wa Kitanzania kujua sana bila kusoma kabisa, desturi ya kubisha tusichokijua vizuri, utamaduni wa kuwa wajuaji mbele ya upofu wa jambo tunalojua tunalijua.

Nimeshika kalamu leo kwa kuwa naona kuna wingu kubwa baina ya watumiaji wa sheria hizo na waliokabidhiwa jukumu la kuzifanyia kazi, wapo wananchi ambao bado wanatumia sheria ambazo labda zilifutwa au kufanyiwa marekebisho makubwa, sheria mpya ni changamoto kubwa kwa kizazi hiki kisicho na utamaduni wa kupitia nyaraka mbalimbali.

Lililonisibu kuandika ni suala la wingi wa sheria ambazo hazijulikani au sheria ambazo hazijaandikwa katika Gazeti la Serikali kuwa sheria mama na mwongozo kwa wananchi, kwa ufupi kuna mkanganyiko mkubwa wa sheria kutokana na mahali ulipo, siku hizi nasikia zinaitwa sheria ndogo za mahali.

Sioni sababu kwanini kuwepo na sheria ndogondogo iwapo sheria kubwakubwa zinavunjwa kiurahisi, sheria kubwakubwa ziliachwa katika makabati na kuwafanya Watanzania wazowee maisha ya kuvunja sheria na sheria inaposhika mkondo waanze kulalamika kuwa wanaonewa.

Najua umuhimu wa kuwepo kwa sheria, moja ya sababu kubwa ni haki baina ya wananchi, lakini sheria inaposhindwa kukidhi matakwa inageuka kuwa kero kubwa kwa wananchi ambao kimsingi ni kama unavunja utaratibu wa kuishi kwa haki na amani.

Haya ndiyo mambo ambayo yamewafanya Watanzania wengi wawe wanahoji hata mahali wasipostahili kuhoji, ni kama wanatafuta namna ya kufuta sheria yenyewe wanayoona kimsingi haikustahili kuwapo ili kuleta haki na amani.

Kuna maswali mengi ambayo tunapaswa kujiuliza juu ya sheria za mahali fulani zinapoibuka na kuwa kero kwa wananchi, hizi sheria za halmashauri au kijiji ni lazima zipitiwe upya na ikibidi zipigwe marufuku ili wananchi tuishi maisha ambayo yapo sawia kisheria kila mahali.

Hizi sheria, mathalani, sheria ya kupitisha gari mahali fulani au kosa la kusimamisha gari mahali katika manispaa moja kuwa tofauti na sheria ya manispaa nyingine, kutafanya wananchi wawe wajinga miaka yote ya kujua sheria mama inasemaje; matokeo yake itakuwa vurugu nchini kwa kosa la kutoelimisha jamii.

Kusiwe na sheria za halmashauri, majimbo, vijiji na pengine mtaa, tuone sheria kuu inasemaje, mimi siyo mwanasheria au mtunga sheria, lakini sina hakika kama ni sawia kuwa na sheria inayovunjwa ndani ya sheria ya msingi, vinginevyo sheria tutaigeuza siasa ya kujadili kila wakati na huu ni wakati wa kazi.

 

Wasaalamu, 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri