Profesa Ibrahim Lipumba alikaa chini akatafakari akaamua kubwaga manyanga, akaandika barua ya kjiuzulu uenyekiti wa CUF. Angebakia na msimamo wake huo huo – ndio kanuni za uungwana – “stick to you words”. Ghafla anasema hee jamani eee mie bado nautaka uenyekiti wangu. Akaandika tena barua ku-‘retrieve’ ile barua yake ya miezi 10 nyuma eti anaona bado anahitajika ndani ya CUF. Ni msimamo gani huo kwa kiongozi mkuu?

Swali la kwanza viongozi na wanachama wanashikwa na mshangao. Profesa kasahau nini kutoka ofisi za CUF? Hiyo ni tabia ya ukigeugeu- leo unaamua hili, kesho unaamua tofauti na ule uamuzi wa kwanza. Tabia namna hii si ya kiongozi wa taifa maana si tabia ya kiungwana.

Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa chama, mtafsiri sahihi wa Katiba ya chama na msimamizi wa imani (IDEOLOGY) ya chama. Kwa nini baada ya kupokea barua ile kutoka kwa Mwenyekiti wake akiomba kujiuzulu hakuitisha kikao husika cha CUF kuijadili na kuitolea uamuzi? Huo ucheleweshaji wa kutoa uamuzi ni udhaifu mkubwa wa uongozi. Tabia ile inaitwa ‘INDECISIVENESS’- kusitasita kutoa uamuzi. Ni kutokujiamini au kutokujua wajibu wake. Dhara kubwa la tabia hii ndiyo kuleta UTATA katika chama. Utata huo (that ambiguity) ndio uliomshawishi au uliomsukuma Profesa Lipumba kuandika barua ya kufuta ule uamuzi wake wa kujiuzulu. Katibu Mkuu wa CUF amejenga mazingira yote ya utata ule. Basi, HATOSHI kuwa Katibu Mkuu-ni goigoi asiyeweza kuamua.

Hapa viongozi wote wawili hawa wana upungufu mkubwa wa kiuongozi. Na ndio wamesababisha msuguano au sintofahamu ndani ya CUF.

Hilo ndilo lililomwongoza Msajili waVyama atoe tafsiri sahihi ya Katiba ya CUF na ni haki kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuata maandiko, katiba na maandishi ya viongozi sahihi ndani ya CUF.

Ukigeugeu wa uamuzi wa viongozi ndani ya vyama vya siasa athari zake ndio hizo. Kutokufuata katiba ya chama. Kutokutafsiri kwa usahihi maana ya demokrasia. Niseme ‘kutokuimanya’ katiba yao maana wametekwa na matukio hata wakasahau katiba yao inasemaje.

Ukiukwaji wa katiba au hata makubaliano yoyote yale kunaleta madhara ndani ya vyama vya siasa. Tabia ya uroho wa madaraka na ubinafsi wa viongozi zimezusha matatizo mengi miongoni mwa viongozi wetu wa siasa.

Wakati wa kujadili rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba bungeni mwaka jana  kuliundwa chombo kinaitwa UKAWA. Kwa uelewa wangu, sijui uhalisia wake, UKAWA siyo taasisi iliyoundwa kikatiba kwa sheria za nchi. Ni makubaliano ya mazungumzo tu (verbal memorandum of understanding). Ni makubaliano ya vyama kadhaa vya upinzani – CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi na NLD. Aidha, UKAWA wamekuwa na makubaliano kadhaa kwa nia na madhumuni ya kuunganisha nguvu zao kuipiku CCM katika jukwaa la uongozi. Kinachonishangazani pale viongozi wa UKAWA kutoa uamuzi wa kigeugeu mara kwa mara ndani ya hiyo UKAWA yao.

Katika kujitafutia ushindi wa viti vya ubunge wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 tuliona tabia yao ya kigeugeu katika kiti cha ubunge cha Masasi na kiti cha ubunge Ukonga. Kule Masasi UKAWA waliamua kumwachia NLD kiti kile. Wakati wa kampeni Mzee wa NLD alishtukia CHADEMA wanasema demokrasia ni kupambanisha wagombea na watu wachague. Maskini mzee wa NLD kashikwa na mshituko wa moyo kwa usaliti ule wa UKAWA. Matokeo yake Mwenyekiti wa NLD akapoteza maisha.

Ukonga, CUF ilijiamini Julius Mtatiro atawakilisha UKAWA katika kiti kile. CHADEMA ikaweka mtu wao pale na CUF wakaonja adha ya USALITI. Mtatiro akafyata mkia kimya kimya akaona kiti cha ubunge cha Ukonga kikiyoyoma, akabaki anakodolea macho na kujutia. Uamuzi ule wa UKAWA ni matokeo ya kauli za kigeugeu ndani ya hiyo UKAWA.

Tabia ya kigeugeu miongoni mwa viongozi wa UKAWA ikaendelea kuonekana. CUF ikamteua Julius Mtatiro Mwenyekiti wa muda wa CUF badala ya Profesa Lipumba. Kiongozi huyu (Julius Mtatiro) sasa ameshamgeuka Profesa na kuhoji; ‘hivi Lipumba anataka kuongoza CUF ipi?’ Mwaka jana tu Mtatiro akimsifia na kumtangaza Profesa Lipumba, leo hii mara moja anaona Profesa si lolote, si chochote.

Kwa mwenendo namna hii vyama vya upinzani watapevuka lini? Inabidi uongozi uache tamaa za unafsi na kusimamia ‘ideology’ ya chama wakati wowote ule. It is the CREED of the PARTY that counts na siyo mimi na wewe tutakuwa akina nani.

Na tukiangalia matokeo ya uchaguzi wetu wa Oktoba 2015 hakuna tofauti kubwa ya matokeo ya miaka ya nyuma.

Kulijitokeza vyama 22 vya siasa vyenye kuweka majina ya wagombea ubunge kwenye majimbo 264. Huo ni utitiri wa kutaka kuonesha demokrasia ya Tanzania. Vyama vyenyewe vilikuwa ni ATC – Wazalendo, ADA – TADEA, ADC, AFP, APPT – Maendeleo, CCM, CCK, CHADEMA, CHAUMMA, CUF, Demokrasia Makini, DC, Jahazi Asilia, NCCR – Mageuzi, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD na mwisho ni UPDP.

Kutokana naulimbukeni wa siasa na kuonesha demokrasia yetu ilivyo, vyama vinane katika vile 22 viliweka wagombea urais katika uchaguzi ule wa mwaka 2015. Vyama vilivyotoa wagombea urais ni ATC- Wazalendo, CCM, CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi, ADC, CHAUMA na TLP.

Matokeo ya uchaguzi ule yaliyotangazwa kwa kiti cha urais yalikuwa hivi:- CCM ilifanikiwa kutetea kiti chake cha urais ikafuatwa na CHADEMA, ATC – Wazalendo, ADC, CHAUMA, TLP, NRA na UPDP wakafunga dimba (wa mwisho kwa kupata kura 7,785 tu za urais).

Kwa viti vya ubunge matokeo bado yalionesha kuwa vyama vingine walikuwa wasindikizaji tu- hata kiti kimoja cha ubunge hawakupata. Basi, matokeo ya viti vya wabunge kwa yale majimbo 264 ya uchaguzi wa kidemokrasia yalikuwa hivi:

 

CCM walikumba viti 195, CHADEMA viti 35, CUF viti 32 huku ndugu zangu akina Mbatia wa NCCR – Mageuzi kiti kimoja tu chake yeye Mwenyekiti wa chama hicho, na askari wangu Zitto Kabwe wa ATC – Wazalendo naye chama chake kikaibuka na kiti kimoja tu chake yeye Mwenyekiti. Jumla ni viti vyote 264.

Hapo sasa, kulitokea nini kwa vyama vile vingine 17 hata vikakosa kiti angalau kimoja katika Bunge? Ndiyo demokrasia aliyosema Aristotle hiyo ya kuwapa uwezo wanyonge? Hata kidogo. Tanzania tumetafsiri vibaya neno hili demokrasia.

Ni lazima kujiuliza huu utitiri wa vyama 22 vya siasa viongozi wake wanaelewa kweli maana ya demokrasia? Mimi nadhani ni msukumo wa uchu wa madaraka tu au vinginevyo ni ulimbukeni wa kutaka kujionesha kuwa hata mimi naweza kuunda chama kikaongoza. Ni silika ya umimi. Hakuna uelewa wa demokrasia hapo. Tutaendelea na majaribio haya ya aina ya demokrasia katika nchi yetu kwa muda gani?

Narudia kauli ya Mwalimu Nyerere pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye kongamano lile la Mei 20, 1974 alipotamka: “Education means liberation of the mind”. Je, mpaka sasa Watanzania hatujakomboka kifikra mpaka tung’ang’anie kuongoza chama cha siasa ingawa chama chenyewe hakichaguliki? Kwa nini tuna upofu wa kutambua demokrasia halisi ni ipi?

Bado najiuliza DEMOKRASIA gani inafuatwa hapa Tanzania? Tangu mwaka 1992 Taifa lilipoamua kurejea kwenye mfumo wa siasa ya vyama vingi, mioyo ya wale wote waliokuwa na mafukuto ya kubinywa demokrasia wakapata nafasi ya kutoa yale mafukuto yao kwa kuanzisha vyama vingine vya siasa na wakajitoa kutoka minyororo ya CCM.

Hapo tunasema wakapumua! (They vented their steam out of their hearts). Ndipo tukaona katika uchaguzi ule wa mwaka 1995 vyama 13 vya siasa vilijitokeza kugombea viti vya ubunge. Katika vyama hivyo 13, basi vyama vinne viliweza kujitokeza kuweka wagombea urais. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1965 chama tawala sasa kikapata UPINZANI. Hii maana yake kwa muda usiopungua miaka 30 chama tawala kimefaidi ukiritimba (monopoly of one party election) wa chama kimoja tu. Nayo haikuwa demokrasia halisi kama ilivyotafsiriwa na Wayunani. Labda ilifaa kuitwa demokrasia ya Kitanzania ya Kibantu.

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri