150827102252-donald-trump-july-10-2015-super-169Uchaguzi umemalizika nchini Marekani; na Donald Trump ametangazwa kuwa mshindi. Huu ni uchaguzi ambao ulisusiwa na asilimia 43 ya wananchi ambao inaelekea hawakuwa na muda au hawakutaka kupoteza muda wao.

Trump ametangazwa kushinda ingawa amepata kura  61,166,063; wakati mpinzani wake, Hillary Clinton alipata kura 62,318,079. Ni  kwa sababu katika nchi hii ushindi hautegemei wingi wa kura za wananchi, bali unategemea wingi wa kura za majimbo.

Yaani wananchi katika majimbo wanachagua wawakilishi wao ambao ndio wanaoamua nani ameshinda. Hawa ni wawakilishi wa majimbo (Electoral College) ambao wamempa Trump kura 290 wakati Clinton amepata 232. Huu ni mfumo kwa mujibu wa katiba yao. Wengi wanaona ni vizuri wakaachana na mtindo huu na badala yake wategemee kura za wananchi.

Hata Trump wakati wa kampeni aliulaani mtindo huu akisema si wa haki, lakini mara tu aliposhinda akaandika katika mtandao kuwa ni njia bora ya kumpata rais kwa vile inatoa haki hata kwa majimbo madogo!

Kushindwa kwa Clinton kuliwashangaza wengi. Kampeni ilikuwa haijawahi kutokea, jinsi wagombea walivyoparurana na hata kutukanana. Tafiti nyingi zilitabiri kuwa Clinton angeshinda.

Mshangao mwingine ni maandamano yaliyoibuka ghafla nchini kote. Maelfu ya vijana wamejitokeza kumlaani Trump na kumkataa kama rais wao.

Wanafunzi na vijana walimiminika mitaani.  Zaidi ya 260 walikamatwa na polisi ambao walitumia risasi baridi, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha. Jijini New York watu zaidi ya 10,000 waliandamana hadi makazi ya Trump wakalizingira jengo lake (Trump Tower). Wengi wao walibeba mabango yakisema “Trump si rais wetu”. Wengine wakachoma moto sanamu yake.

Wakati huohuo, watu zaidi ya milioni mbili nchini Marekani wamesaini risala wakiitaka Electoral College kutomtangaza Trump kama rais na badala yake wamtangaze Clinton. Jopo hilo linatarajiwa kukutana Desemba 19 kutaangaza matokeo ya mwisho.  Trump aliwalaani waandamanaji na kusema walilipwa fedha ili kuandamana na pia walichochewa na vyombo vya habari.  Yaelekea washauri wake walimuonya. Ndio maana siku ya pili Trump akageuka na kuwasifu waandamanaji akisema yeye yuko pamoja nao.

Inasemekana alishauriwa kuwa ni lazima abadilishe lugha kali aliyokuwa akitumia wakati wa kampeni. Ndio maana akaanza kuwasifu Obama na Clinton ambao nao wakamsifu Trump.

Mwishowe Trump akasema amejifunza mengi mazuri kutoka kwa Obama. Naye Obama akasema: “Ni vizuri tukakumbuka kuwa sote tuko katika jahazi moja.”

Nikakumbuka ule usemi “Waarabu wa Pemba…” Ukweli ni kuwa hakuna tofauti za kimsingi baina ya Republican na Democrat.

Hata hivyo, ni vigumu kusahau kuwa Trump amechaguliwa na watu ambao wamekuwa na msimamo wa kikaburu. Wamempata rais ambaye anazungumza lugha yao.

Kwani Trump aliwahi kutoa matangazo katika magazeti akipendekeza kunyongwa kwa vijana watano weusi ambao waliwekwa gerezani miaka mingi bila ya kushtakiwa. Walishukiwa kwa ubakaji na hata kabla kufikishwa mahakamani, Trump alitaka wanyongwe. Baadaye iligundulikana kuwa hawakuwa na hatia, lakini Trump hakuomba radhi.

Wamempata Trump ambaye wakati wa kampeni yake aliahidi kuwa atapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani, kuwa atawasajili Waislamu wote wanaoishi Marekani ili kuwachunguza mienendo yao, na pia atabomoa misikiti yao nchini humo. 

Makaburu hawa sasa inaelekea wamepata nguvu mpya na ari mpya. Ndio maana kikundi cha kikaburu kiitwacho Ku Klux Klan (KKK) kimetangaza kuwa kitaandamana huko North Carolina ili kusheherekea ushindi wa Trump.

Hawa ni weupe ambao wanaamini kuwa wao wana hati miliki ya Marekani na ndio wenye haki ya kutawala. Wamekuwa wakiwashambulia siyo tu Weusi, bali pamoja na Wayahudi na Wakatoliki. Baadhi yao wamediriki hata kuwachoma moto. Kiongozi wao, David Duke ameandika katika mtandao akimpongeza Trump.

Inasemekana kuwa hata mshauri mkuu aliyeteuliwa na Trump amewahi kuwa mwanachama wa KKK. Na ndipo unakuta baada ya ushindi wa Trump mwalimu wa sekondari katika Georgia anaandikiwa barua na wanafunzi wake wakimwambia atumie hijabu yake kujitundika.

Mwalimu huyo, Bi Mairah Teli, amesema: “Mimi ni Mwalimu. Nimesikitishwa sana na barua hii niliyoikuta darasani. Nikiwa Mwislamu navaa hijabu kwa mujibu wa imani yangu. Nataka wote wajue kuwa haya ni mazingira ya nchi yetu leo. Kueneza chuki kama hii hakutaifanya Marekani kuwa taifa kubwa ulimwenguni (kama anavyokusudia Trump).”

Pia wanawake kadha walivuliwa hijab wakiwa barabarani, huku wakiambiwa; “Hili si vazi la Marekani, nanyi si Wamarekani.”

Halafu kuna matukio ya raia wenye asili ya Kiafrika na Mexico ambao pia wameshambuliwa, wametukanwa na wamedhalilishwa.  Katika shule ya sekondari iliyopo Pennsylvania wanafunzi weupe wamekuwa wakiwaita wanafunzi Weusi “wavuna pamba” wakikumbusha kazi waliyokuwa wakifanyishwa mababu na mabibi zao wakati wa utumwa.

Mwanafunzi wa miaka 10 alidhalilishwa kijinsia kwa kushikwa sehemu zake za siri. Mtoto aliyefanya kitendo hicho alisema “iwapo rais wangu anaweza kufanya hivyo, nami pia naweza.”

Katika vyuo vikuu yalichorwa maneno “Marekani ni nchi ya weupe tu” pamoja na nembo ya Hitler (swastika). Katika chuo kikuu cha New York jina la Trump liliandikwa kwenye mlango wa chumba wanakoswali Waislamu.

Tangu kutangazwa kwa Trump nchini kote Marekani kumekuwako na matukio ya aina hii zaidi ya 440. Yamekuwako tangu zamani, lakini sasa yameongezeka.

Haya ni mambo ya ndani ya Marekani. Ni muhimu pia tukaangalia jinsi “ushindi” wa Trump utakavyoathiri ulimwengu mzima, na hasa bara letu la Afrika.

Trump ametamka kuwa ana nia ya kujitoa kutoka makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Mikutano mikubwa ilifanyika mjini Copenhagen na Durban. Ndipo mwaka 2015 jijini Paris wakuu wa mataifa 195 walitiliana saini makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa kaboni (hewa ukaa) ili kuinusuru dunia kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Sote tunaelewa kuwa barafu juu ya Mlima Kilimanjaro inayeyuka. Halikadhalika milima ya Rwenzori huko Uganda. Kutokana na ukame unaoongezeka kila mwaka wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) wamesema ifikapo mwaka 2100 wakulima tisa kati ya 10 hapa Afrika watashindwa kulima kwa sababu ardhi itageuka jangwa.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti ya Christian Aid, wananchi milioni 180 watakufa katika bara letu kutokana na mabadiliko haya iwapo hayatadhibitiwa kwa hatua za makusudi.

Sasa Trump amesema hakubaliani na wanasayansi kuhusu mazingira. Hivyo ataitoa Marekani kutoka makubaliano ya Paris 2015 kama George W. Bush alivyojitoa kutoka protakali ya Kyoto. Hii ni hatari kubwa kwetu sote. Hivi ndivyo tunavyohusika moja kwa moja na sera ya Trump.

Tunahusika pia kwa sababu Marekani imetawanya majeshi yake katika bara letu. Hivyo ni vizuri tukajiuliza iwapo Trump ataendeleza sera ya kibeberu duniani, au ataamua kuokoa fedha ili kuinua maisha ya wananchi wake.

Kwa mfano, utawala wa Obama umekuwa na mpango wa siri wa kupanua kituo cha ndege zisizo na rubani (drone) nchini Niger. Bajeti ya kwanza ya mradi huu ni dola milioni 100 na lengo ni kuendesha shughuli za kijasusi na mashambulizi barani Afrika kwa kutumia ndege za drone. Obama ameidhinisha mradi huu.

Niger ni nchi pekee katika kanda ya magharibi iliyokubali kuruhusu kituo hicho cha kijeshi cha Marekani. Tuone kama Trump atauendeleza mradi huu, au la!

Tangu mwaka 2002 Marekani imekuwa ikiendesha kile wanachoita ushirikiano wa kupambana na ugaidi barani Afrika (TSCTP). Wanadai wanasaidia majeshi ya Chad, Mali, Mauritania na Niger. Kati ya mwaka 2009 na mwaka 2013 wametumia dola milioni 288.

Wanadai kuwa wanapambana na ugaidi. Lakini wanajeshi waliofunzwa na Marekani wamekuwa wakipindua serikali zao za kiraia. Hii imefanyika katika Niger, Chad (mara mbili), Mauritania (mara mbili) na Mali. Halafu wanadai eti wanalinda usalama wetu.

Ni usalama upi, wakati tangu kumimina majeshi yao katika bara letu makundi takriban 50 ya kigaidi yameibuka?  Haya yalisemwa na Brigadia Jenerali Donald Bolduc, ambaye ni Mkuu wa Oparesheni ya Majeshi ya Marekani barani Afrika.

Hii si ajabu, kwani mwaka 2002 afisa mwandamizi katika makao makuu ya majeshi Marekani (Pentagon) alitabiri kuwa “baada ya Marekani kuishambulia Afghanistan magaidi watatoka huko na kukimbilia Afrika ambako watahatarisha maslahi yetu.”

Ilipofika mwaka 2008 Marekani ikaanzisha Africom katika bara letu ili kulinda hayo maslahi yao. Lakini hali ilizidi kuwa mbaya, kwani mwaka 2014 majeshi ya Marekani yaliendesha oparesheni 674 katika Bara la Afrika. Leo hii Africom imeeneza makucha yake katika nchi 23 za Kiafrika. Je, Trump ataunga mkono ubeberu huu?

Ripoti moja ya siri iliyovujishwa inasema katika kambi ya kijeshi ya Lemonnier iliyoko Djibouti kuna ndege za drone zinazotumika kuwaua watu wanaoshukiwa kuwa magaidi. Kambi hii ilipanuliwa kutoka ekari 88 mwaka 2002 hadi ekari 600 hii leo. Tayari wametumia dola milioni 600 na siku za baadaye wanapanga kutumia dola bilioni 1.2. Je, Trump ataendeleza sera hii?

Kwani yeye amewahi kutamka kuwa si kazi ya Marekani kueneza demokrasia katika nchi za kusini. Amesema “Inatuhusu nini sisi kuwafundisha Waafrika jinsi ya kuendesha nchi zao?”

Tusubiri kuona kama atatekeleza aliyoyasema au ni danganya toto tu.

By Jamhuri