N

dugu Rais, kumekuwa na mfululizo wa habari zisizoisha kuhusu ujambazi na majambazi katika misitu ya pori la Vikindu. Vikindu kama ilivyo Mkuranga yenyewe ambayo ni wilaya mojawapo katika Mkoa wa Pwani, kwa kweli ni Dar es Salaam. Karibu kabisa na yalipo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini. Pia ni karibu na Makao Makuu ya Jeshi  la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pia makao makuu yapo Dar es Salaam. Tuseme ni kilomita chache sana kutoka Vikindu hadi Ikulu, rais anakoishi na kufanyia kazi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamewakamata wanawake wanne na watoto wanne waliokuwa wamefichwa kwenye kambi maalumu huku wakipatiwa mafunzo ya uhalifu wa kutumia silaha. Aliongeza kusema kuwa waliwakamata eneo la Kilongoni wakiwa wamekusanywa kwenye nyumba ya mtu aliyemtaja kwa jina moja la Suleiman wakiwa wanafundishwa mambo ya dini na harakati za kigaidi. Sambamba na mafunzo ya madrasa, pia walikuwa wakifundishwa ukakamavu katika michezo ya karate, kunfuu na judo pamoja na matumizi ya silaha aina ya SMG na bastola.

Kamanda Sirro aliongeza kusema kuwa watoto hao pia walikuwa wakifundishwa kupiga maeneo tete ya kummaliza mtu pumzi na kufariki haraka, kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe, na kupora au kunyang’anya kwa kutumia silaha

Ndugu Rais, harakati hizi za kigaidi katika misitu ya pori la Vikindu hazikuanza leo. Ni miaka sasa tangu tuanze kuzisikia. Wananchi wana haki ya kujiuliza mpaka hawa magaidi wanaanzisha makambi ya mafunzo walinzi wao kwa maana ya polisi, wanajeshi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama walikuwa wapi? Ni kweli vyombo vyote hivi vilikuwa havijui? Kama ni kweli vilikuwa havijui, basi ulinzi na usalama wa raia na nchi yao uko shakani.

Siku za nyuma wananchi waliambiwa kuwa yaliwahi kutokea mapambano makali kati ya polisi wetu na magaidi hao ambako magaidi walifanikiwa kumuua kamanda wa polisi aliyekuwa anaongoza operesheni hiyo. Polisi waliongeza nguvu kwa kushirikiana na wanajeshi na wakawaambia wananchi kuwa walikuwa wamechakaza kila kitu.

Cha kushangaza ni kwamba matukio ya kigaidi yangali yanaendelea. Sasa Kamanda Sirro anasema wamewakamata wanawake wanne na watoto wanne waliokuwa mafunzoni. Kama waliokamatwa ni wanafunzi waliokuwa mafunzoni, walimu wao wako wapi? Bila kuwakamata walimu wao mafunzo yataendelea. 

Hizo kambi zikishambuliwa huwa zinavunjwa halafu wanajenga tena upya? Kwanini kambi za mafunzo bado zingalipo? Tishio

la ugaidi nchini mwetu ni kubwa. Iko haja walinzi wetu wakajipanga upya kwani kwa mwonekano wa sasa magaidi wanaonekana wanapeta.

Yaonekana Polisi imeelekeza nguvu kubwa sehemu ambako hakuna tishio! Ndugu Rais, ile nguvu kubwa inayotumika kule Arusha kwanini isije kusaidia huku? Arusha kunani? Hawa wana judo, karate na silaha za moto wakati Godbless Lema hana hata kisu cha mfukoni. Yanayotendeka Arusha kwa Lema yanalifedhehesha Taifa. Ni aibu kwetu wenyewe na wenzetu wa nje wanaotufuatilia lazima wataishia kutudharau. Kwanini tunaonesha woga mkubwa kiasi hiki kwa jambo ambalo tunaweza kulimaliza vema kama tukitumia vichwa vyetu kufikiri?

Ndugu Rais haiingii akilini kwa mtu timamu kuona askari sita wakiwakimbiza akina dada waandishi wa habari huku wakiwa wamewashikia bunduki eti kosa kumpiga picha Godbless Lema! Tumefikishwa wapi hapa?

Kwanini baadhi ya askari wachache waendelee kuidhalilisha serikali kwa kiwango hiki? Baba, serikali ni rais! Tumekosa busara, je na fahamu tumepoteza? Ni kweli hakuna wa kuwakemea wahuni wachache walio katika jamii yetu? Tusiwasukume wananchi wamwamini Mzee Mwinyi anaposema nchi inaendeshwa kama gari lililokatika usukani. Tunajidanganya sana kuwaona akina Lema kama wapinzani halisi. Kama ni nyoka hawa ni nyoka wa plastiki. Wanatisha sana kwa fikra nzito wanazozionesha, lakini hawamdhuru mtu! Na sasa wamejengewa imani ya manabii kuwa wanateswa kutokana na kuwatetea Watanzania! Kati yao mwendawazimu ni nani! Hawa nyoka wa plastiki au wale wanayempiga nyoka wa plastiki kwa kutumia gongo kubwa?

Ndugu Rais, kama wale waandishi wa habari waliokuwa wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada wasingekutana na Hakimu mwema Nestory Baro, ingekuwaje? Aliwashika na kisha akawataka askari waache kuidhalilisha Mahakama kwa vitendo vya aina hiyo. Naye Hakimu Mfawidhi Rwezile alisema Mahakama haifanyi kazi kwa siri na kwamba bila kujali mtu mwenye kesi mahakamani hapo, waandishi wa habari na watu wengine wote wanaruhusiwa kuingia mahakamani hapo bila kubughudhiwa alimradi wanafuata taratibu.

Alisema, “Watu wanakuja kutafuta haki zao. Hivyo hatutarajii kuona wala kusikia kama nilichoona leo wakiwafanyia waandishi wa habari. Nimeonya na sitarajii jambo hili lijirudie.”

Baba, hii nguvu kubwa kule Arusha ya nini? Kwanini tusiielekeze Vikindu? Huenda ni kwa amri zetu sasa tumetengeneza Jeshi la Polisi ambalo si rafiki tena kwa raia. Tumeshuhudia polisi wakiuawa baadhi ya raia wanashangilia. Baba, ulijisikiaje uliposikia kuwa kuna mashamba makubwa ya bangi jirani tu ya hapa? Bangi inalimwa kwa kilimo cha umwagiliaji! Inapandwa, inamwagiliwa mpaka inavunwa polisi hawajui?

Tulisema tangu mwanzo, baba tengeneza polisi yako!

By Jamhuri