Miaka mitatu iliyopita, kuanzia Juni 11, 2013 niliandika makala iliyohusu “Haki, Ukweli ni Nguzo ya Amani.” Katika makala yale nilielezea na kufafanua hadharani maana ya HAKI na UKWELI yanavyojenga nguzo ya AMANI katika jamii yoyote duniani.

Leo tena nimeona ipo haja ya kuzungumzia neno UKWELI ikiwa ni sifa kuu ya uadilifu. Msukumo huu umenijia baada ya kufuatilia hali ya mgogoro wa kisiasa uliyopo sasa ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba

Ukweli, kiasili visiwa hivyo tangu zama kuna migongano ya kimaslahi, kinasaba, kimila na kitamaduni. Huo ndiyo ukweli wenyewe. Hata kama visiwa hivyo vilikuwa chini ya tawala za kienyeji, baadaye za kisultani na hatimaye za wananchi, ukweli bado amani yake haijawa asilimia mia moja kwa sababu HAKI na UKWELI havijapewa udhahiri wake.

Sipendi kuelezea historia na mwenendo wa visiwa hivyo kwa mujibu wa simulizi zilizomo vitabuni, ndani ya vifua vya Waunguja na Wapemba na Watanzania wa Zanzabar wa tangu mwaka 1964 hadi leo. Kwa sababu wote wanadai wana HAKI na wanasema UKWELI juu ya Zanzibar yao. (Unguja na Pemba).

Tangu Oktoba 28, 2015 ndani ya wiki ya Uchaguzi Mkuu ulioanza Oktoba 25, 2015, masikio ya Wananchi wa Jamhuri ya Muungano  waTanzania yalianza kusikia kauli ya aliyekuwa mgombea urais  wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad akitangaza yeye ndiye anayestahili kutangazwa na  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa mshindi; ili hali TUME hiyo halali ilikuwa bado imo katika mchakato wa kupokea  na kuhesabu kura zilizopigwa vituoni Unguja na Pemba.

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha alisikika ndani ya saa 24 hivi, akitangaza na kuikana kauli ya Maalim Seif akisema ni batili na wala hana mamlaka na madaraka ya kujitangaza. Hiyo si kazi yake ni kazi ya TUME – ZEC kutangaza mshindi wa urais wa Zanzibar.

Tayari kauli mbili hizo zinagongana na dhana HAKI na UKWELI na kuleta mtetemeko ndani ya watu wa Zanzibar na kujiuliza kulikoni? Mtetemeko huo umekuwa na kupanuka na kuleta mtikisiko ndani na nje ya visiwa hivyo pale Mwenyekiti Jecha alipotangaza kufuta matokeo na kuagiza kufanya uchaguzi tena ndani ya miezi mitatu ijayo.

Kuanzia hapo kila mtu mwenye filimbi, nzumari, baragumu alijitahidi kuvimbisha mashavu kujaza pumzi-hewa kupuliza ala yake isikike hadi ndani ya handaki. Kazi hiyo bado inaendelea kufanywa na viongozi na wanasiasa wao, wanasheria, wanadiplomasia, wanaharakati na waandishi wa vyombo vya habari. Ngoma imeiva na Watanzania wanaicheza !!.

Nyimbo tatu zinanogesha ngoma hiyo. Ya kwanza, kumtaka Mwenyekiti wa ZEC amtangaze mshindi aliyejinadi. Ya pili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aingilie kati na amtaje aliyejinadi awe mshindi. Na wimbo wa tatu hakuna mshindi na uchaguzi unarudiwa Machi 20, 2016. Patamu na pachungu hapo.

Yote niliyoyagusia ukweli pande mbili hizo zilizomo kwenye mvutano yaani Maalim Seif na Mwenyekiti Jecha walistahiki kuwapo kwenye kilinge kimoja na kila mmoja kutoa uthibitisho wa madai yake ili wachezaji, Watazamaji na wasikilizaji waweze kutoa msimamo wao  baada ya UKWELI kuwekwa dhahiri shahiri.

Kwa mantiki hiyo, ile nguzo ya amani ingekuwapo Unguja na Pemba badala ya hivi sasa Watanzania wanavyoendelea kusikia mivumo ya ala, vigelele, vifijo na midundo ya ngoma ikitia tafrani ndani ya mioyo yao. Hivi kulikuwa na hofu gani tangu awali kwa Maalimu Seif na Mwenyekiti Jesha kutuweka wazi kwa kilichotokea siku ya uchaguzi Oktoba 25, 2015?

Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari nchini na hasa vya huko Zanzibar, kupitia kipindi maalum kilichorushwa na Televisheni ya Zanzibar (ZBC) mjini Unguja alisikika Jecha na kukaririwa akitoa ushahidi wake uliomlazimisha kuufuta uchaguzi ule ulitokana na kasoro zilizojaa udanganyifu wa wazi.

Alisema alibaini kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa kanuni na sheria za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, zilizofanywa na baadhi ya wasimamizi walioajiriwa na taasisi hiyo. Alisema kuwa wasimamizi walijaribu kuharibu uchaguzi wakitumia baadhi ya fomu ambazo hazitokani na Tume na kujaza matokeo.

Alisema kasoro nyinginezo ni pamoja na kuwapo mihuri feki ya ZEC, karatasi kujazwa namba za ziada tofauti na idadi ya wapiga kura 300 na kuwa na idadi ya 330 katika kituo kimoja husika. Namba za fomu zilifanana katika fomu tofauti na majina ya wasimamizi kujirudia katika vituo mbalimbali; badala ya kutakiwa kuwapo katika kituo kimoja tu husika.

Fomu za vituo vitatu tofauti zilisainiwa na msimamizi mmoja jambo ambalo si sahihi. Kila kituo kina msimamizi wake. Baadhi ya wananchi walitishwa kwenda kupiga kura vituo vya Pemba. Waangalizi wa kimataifa kushindwa kwenda Pemba na walionekana  walikuwa na azma yao maalum. Mengi alieleza Mwenyekiti Jecha.

Binafsi bado najiuliza kwanini Jecha hakueleza “MADUDU” hayo na mengineyo tangu awali? Laiti angeeleza hayo mwanzoni na Maalim angejibu kilingeni,  leo nguzo ya amani ya Unguja na Pemba isingekwenda fyongo. Hata hivyo Watanzania tuna muda wa kutafakari kabla ya Machi 20, 2016.  Kwaheri ya majaliwa.

By Jamhuri