Mhariri, kwanza nakupongeza kwa uzalendo wa kuichapa barua hii.
Sababu kubwa ya kuandika andiko hili ni kumuomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, afike huku kwetu Zanzibar kujionea makosa ya barabarani yanayofanywa kwa makusudi bila kuchukuliwa hatua.
Sitanii. Ukiwa barabarani kila dakika utaona daladala au gari la abiria lililozidisha abiria kupita idadi iliyoandikwa ubavuni kwa dereva. Huo ni upakiaji hatarishi usioruhusiwa hata iwe ni kwa wanafunzi.
Tumekuwa tukishuhudia wapanda Vespa (pikipiki) wakiendesha bila ‘helmet’. Makosa mengine ni kutoheshimu taa za kuongozea magari, kutoheshimu alama za barabarani na kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa kasi.
Pia yapo magari mabovu lakini yapo barabarani, magari ya kusafirisha abiria yanajaza mafuta vituoni huku yakiwa na abiria, jambo ambalo ni hatari. Madumu ya kuchotea maji kufanywa kuwa vikalio vya abiria n.k.
Makosa hayo huku kwetu ni ya kawaida, wala hayachukuliwi hatua zozote na wahusika. Kwa makosa hayo wahusika walitakiwa kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kutozwa faini, lakini askari wetu huku wamekuwa kimya huku wakiikosesha serikali mapato kwa makusudi.
Makosa ya barabarani yanayohatarisha maisha yetu yamekuwa yakifanywa makusudi. Tunajiuliza, serikali iko wapi kuchukua hatua? Waliopewa dhamana wako wapi? Au wana masilahi na yanayotokea?
Mheshimiwa waziri, iwapo mtu akiibiwa Vespa akatoa ripoti katika kituo chochote cha Polisi kilichopo Mkoa wa Mjini Magharibi, akitaja tu eneo chombo kilipoibwa, polisi huomba wapatiwe Sh. 200,000. Baada ya kutoa malipo hayo chombo hupatikana.
Polisi wetu wamekuwa wakishirikiana na wahalifu. Askari wetu wana mtandao wa wezi na matapeli maarufu. Hivi sasa wizi wa mifugo umeshika kasi, wizi wa mazao tumeanza kuuzoea, unyang’¡¯anyi, udhalilishaji pamoja na ubakaji huku mbakaji akiuawa yamekuwa ni maisha yetu.
Haya yote yanafanyika kwa sababu kesi nyingi zinaishia vituoni kwa njia ya rushwa. Askari hawatimizi majukumu yao, inasikitisha gari la abiria linatoka shamba hadi mjini likiwa limezidisha abiria, linapita vituo vitatu vya Polisi na zaidi halikamatwi wala hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Huku mambo yote humalizwa kwa siri.
Juni 28, mwaka huu Makamu wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, aliliagiza Jeshi la Polisi Zanzibar na taasisi zinazohusika na usalama barabarani kuwadhibiti wanaovuruga sheria za barabarani. Agizo hilo halijatekelezwa na madereva wanatamba wakijua askari watamalizana nao kwa rushwa, kwa sababu umekuwa ndio mradi wao.
Kwa maelezo haya, naamini mheshimiwa waziri utakuwa umefahamu ni kiasi gani askari wetu walivyo tatizo. Nyumba za askari wa usalama barabarani zimejaa vitabu vyenye namba za vyombo vya moto ambavyo kesi husika zimeishia hewani.
Wako katika ujenzi wa taifa,
Omar Mikate,
Mwanakwerekwe, Zanzibar.

Mwisho

998 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!