NA MWANDISHI WETU, DODOMA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano, na kutoa mwito kwa wananchi kuzidi kuunga mkono juhudi za serikali.

Hayo yamo kwenye hotuba yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019, aliyoitoa bungeni wiki iliyopita. Hotuba hiyo imechapishwa katika kurasa za 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17 na 18 za toleo hili.

Amesema, “Tukiwa tunaingia kwenye Bunge la Tatu la Bajeti kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatuwezi kumsahau Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania kwa kujenga nchi yenye uchumi imara.

“Katika kipindi hiki, tumeshuhudia mambo makubwa aliyoyafanya yakiwemo kujenga ari ya uzalendo kwa kuilinda na kuisemea nchi yetu bila woga; kudumisha amani, utulivu na mshikamano; kuimarisha ulinzi na usalama kwa kukomesha vitendo vya mauaji yaliyojitokeza Mwanza, Amboni (Tanga), Mkuranga, Kibiti, Rufiji (Pwani) pamoja na kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.”

Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine kuwa ni kujenga nidhamu ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe; kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma; kuanzisha mahakama ya rushwa na ufisadi; na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi zikiwemo za madini na maliasili.

“Aidha, amefufua Shirika la Ndege la Tanzania; ameanzisha ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR); ameendeleza ujenzi wa barabara zikiwemo barabara za juu (flyovers) na amenunua meli na vivuko.

“Kazi nyingine ni ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme kama vile Stiegler’s Gorge; usambazaji umeme hadi vijijini na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania),” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameyataja mambo mengine makubwa aliyoyafanya kuwa ni kuimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya; kutoa elimumsingi bila malipo kwa watoto wa Kitanzania; ujenzi wa miradi ya maji; na kuimarisha bei za mazao ya kibiashara.

“Mheshimiwa Rais ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma. Haya ni baadhi tu ya mambo aliyoyafanya na yatatolewa ufafanuzi wa kutosha kupitia wizara za kisekta,” amesema.

Kuhusu uchumi, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

“Viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8, kiwango ambacho kilikuwa juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo uchumi wa Kenya ulikuwa kwa asilimia 6.1, Rwanda asilimia 6.0, Uganda asilimia 5.5, Burundi na Sudan Kusini asilimia hasi 6.3.

“Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kwamba katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2017, Pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016.

“Shughuli zilizochangia ukuaji huo  kwa viwango vikubwa ni pamoja na uchimbaji wa madini na mawe asilimia 17.5; huduma za usambazaji maji safi na majitaka asilimia 16.7; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 16.6; habari na mawasiliano asilimia 14.7 na ujenzi asilimia 14.1.  Aidha, sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ilikua kwa asilimia 3.6, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu mwaka 2010,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

By Jamhuri