Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele ametoa taarifa kwa umma kuhusu udanganyifu unaofanywa na kampuni ya uchimbaji ndhahabu ya Aureus Limited ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Minextech. Ifuatayo ni taarifa hiyo neno kwa neno…

 

Utangulizi

Kampuni ya Aureus Limited (zamani ilikuwa ikiitwa Mineral Extraction Technologies Ltd (Minextech) ni kampuni inayojishughulisha na uchenjuaji wa marudio ya dhahabu ya wachimbaji wadogo (gold tailings) kwa kutumia teknolojia ya kemikali ya sayanaidi (vat leaching).

Kampuni hiyo inamiliki leseni ya uchimbaji madini ML 384/2009. Mitambo ya uchenjuaji ya kampuni hiyo ipo katika maeneo mawili, mtambo wa kwanza upo katika Kijiji cha Nyarugusu wilayani Geita na mtambo wa pili upo Nyakato jijini Mwanza.

Agosti hadi Septemba 2011, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulifanya ukaguzi wa hesabu za fedha na kodi kwa kampuni ya Minextech (ambayo sasa inaitwa Aureus Limited). Ukaguzi huo uligundua kasoro kadhaa zilizoikosesha Serikali mapato. Baadhi ya kasoro hizo ni:


Kampuni ya Minextech kuficha taarifa zake za mauzo ya dhahabu kiasi cha kilo 63.27 yenye thamani ya Shilingi 2,763,426,787 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010. Udanganyifu huo ulibainika baada ya kulinganisha takwimu za uzalishaji zinazotunzwa na kampuni hiyo na kulinganisha na taarifa za mauzo ya dhahabu zilizowasilishwa Serikalini na kampuni hiyo katika kipindi husika.


Kampuni ya Minextech kutolipa kiasi cha Shilingi 9,085,031,656 kama VAT ya mauzo ya dhahabu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.

Kampuni ya Minextech kutolipa kiasi cha Shilingi 252,683,678 kama PAYE katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.


Kampuni ya Minextech kutolipa kiasi cha Shilingi 371,026,716 kama mrabaha katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.Hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha malipo hayo yanafanyika.


Tuhuma za Utoroshaji Madini ya Dhahabu

Kumekuwpo tuhuma mbalimbali kuwa Kampuni ya Aureus Limited imekuwa ikizalisha dhahabu nyingi na kuitorosha nje ya nchi na hivyo kukwepa kulipa kodi za Serikali. Kwa mfano, Juni, 2012 iliripotiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba kampuni ya Aureus Limited imekuwa ikizalisha wastani wa kilo 15 kwa wiki na kuzitorosha nje ya nchi bila kulipa kodi za Serikali. Kufuatia tuhuma hizo, Wizara kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ilichukua hatua za haraka kwa kuweka usimamizi makini wa shughuli za uzalishaji za kampuni hiyo ili kubaini ukweli.


TMAA ilianza rasmi kukagua uzalishaji na mauzo ya dhahabu ya kampuni ya Aureus Limited kuanzia Juni 16, 2012 ambapo Wakala uliweka Mkaguzi katika mtambo wa kampuni hiyo uliopo katika Kijiji cha Nyarugusu. Pia, Juni 27, 2012 Wakala uliweka Mkaguzi katika mtambo wa uchenjuaji wa kampuni hiyo uliopo huko Nyakato Jijini Mwanza. Ukaguzi unaofanywa na Wakala ulilenga kupata taarifa sahihi na za kina za uzalishaji wa kampuni hiyo na kuhakikisha kuwa Serikali inapata kodi na mrabaha stahiki.

Matokeo ya Uchunguzi wa Awali

Mapitio ya taarifa za uzalishaji wa kampuni hiyo zilizowasilishwa Serikalini kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 zilionesha kwamba kwa wastani, kampuni hiyo ilikuwa ikitoa taarifa ya kuzalisha kilo 4 za dhahabu kila mwezi.


Tathmini ya awali iliyofanywa na TMAA kuangalia uwezo halisi wa kuzalisha dhahabu katika mitambo ya kampuni hiyo ulionesha kuwa, mtambo una uwezo wa kuchenjua tani za marudio 3,500 kila mwezi. Matokeo ya uchunguzi wa sampuli za kimaabara kwa marudio (gold tailings) yalikuwa na wastani wa kiasi cha gramu 4 ya dhahabu kwa tani moja, na makapi yalikuwa na wastani wa gramu 1 ya dhahabu kwa tani moja, hivyo kuwepo kwa uwezo wa kuzalisha kilo 10 za dhahabu kwa mwezi.


Ukaguzi wa Uzalishaji wa Dhahabu Mgodini

Ukaguzi uliofanywa na TMAA kuanzia tarehe 26 Juni, 2012 hadi tarehe 3 Septemba, 2012 unaonesha kuwa, uzalishaji wa dhahabu katika kipindi ambacho Wakala umekagua shughuli za uzalishaji wa kampuni hiyo ni mkubwa kuliko uliokuwepo katika kipindi kabla ya kuanza kwa ukaguzi. Kwa mfano, jumla ya kilo 8.72 za dhahabu zilizalishwa katika kipindi cha mwezi Julai 2012.


Ikumbukwe kuwa, marudio (gold tailings) yanayopembuliwa hivi sasa na kampuni hiyo yana dhahabu kidogo ukilinganisha na marudio yaliyokuwa yanapembuliwa miaka iliyopita (kuanzia mwaka 2006 hadi 2010). Hivyo, huu ni ushahidi wa wazi kuwa kampuni hiyo ilikuwa haitoi taarifa sahihi Serikalini za uzalishaji na mauzo ya dhahabu.


TMAA ilikubaliana na kampuni ya Aureus Limited kuwa, wakati kazi katika mtambo wa elution zinapofanyika, Mkaguzi wa Wakala atakuwa na ruhusa ya kuingia katika eneo la mtambo na kuchukua taarifa za uzalishaji wa dhahabu bila kizuizi chochote. Pia, lakiri zitakazotumika kudhibiti uzalishaji kwenye mtambo huo haziwezi kuondolewa bila kuwepo kwa Mkaguzi wa Wakala. Baada ya kuafikiana kuhusu utaratibu wa ukaguzi na udhibiti wa uzalishaji, Wakala umeendelea na kazi ya ukaguzi kama kawaida.

TUKIO LA KUKIUKA MAKUBALIANO NA KUKATA LAKIRI ZA SERIKALI

Mnamo tarehe 9/9/2012 Mkaguzi wa TMAA alipangiwa kufanya ukaguzi katika mtambo wa kuchenjulia dhahabu (elution) wa kampuni ya Aureus Limited uliopo huko Nyakato – Mwanza.


Ratiba ya kazi iliyopangwa awali na uongozi wa kampuni hiyo ilikuwa, Mkaguzi afike katika eneo la mtambo saa moja asubuhi. Mkaguzi huyo alifika mahali hapo muda wa saa 12 na dakika 55 asubuhi. Hata hivyo, Walinzi wa kampuni hiyo hawakumruhusu kuingia ndani ya jengo la uzalishaji na walimfahamisha kuwa uzalishaji wa dhahabu usingekuwepo siku hiyo, na badala yake ungefanyika siku inayofuata, yaani Jumatatu ya tarehe 10 Septemba 2012.


Kufuatia maelekezo hayo, Mkaguzi aliondoka na kurejea ofisini kuendelea na kazi nyingine.Tarehe 10/9/2012 siku ya Jumatatu saa moja kamili asubuhi, Mkaguzi alifika tena kwenye mtambo wa kampuni hiyo huko Nyakato – Mwanza. Alipowasili katika eneo hilo, alijulishwa na Wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa, walifanya kazi tarehe 9/9/2012.


Mkaguzi aliambiwa kwamba, lakiri zilikatwa na uzalishaji ulifanyika. Lakiri zilizoondolewa kwenye mapipa yanayohifadhi loaded carbon ni zenye namba MEM-TMAA 133570-81 na zile zilizotolewa kwenye mitungi ya kuchenjulia dhahabu ni zenye namba MEM-TMAA 132691-4. Kitendo cha kampuni hiyo kufanya kazi ya uchenjuaji wa dhahabu bila kuwepo Mkaguzi wa Serikali ni kukiuka makubaliano kati yake na Serikali na ni dharau kwa Serikali.


Hivyo, Mkaguzi wa TMAA alitoa taarifa kwa Uongozi wa Wakala ambao nao ulizifikisha taarifa hizo Wizarani kwa hatua zaidi. Kufuatia tukio hilo, Serikali imechukua hatua za awali za kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa na kufunguliwa mashitaka. Tayari viongozi wawili wakuu wa kampuni hiyo wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi na uchunguzi zaidi unaendelea kabla ya Serikali kuchukua hatua zaidi zinazostahili.


Tukio hili linadhihirisha wazi kuwa, kampuni ya Aureus Limited ilikuwa imekusudia kuficha kiasi halisi cha uzalishaji wake kwa lengo la kukwepa kulipa mrabaha na kodi stahiki. Vilevile, kupitia tukio hili, ni ishara kuwa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinaelekezwa kwa kampuni hii kuhusu udanganyifu wa takwimu zake za uzalishaji wa dhahabu zinaweza kuwa na ukweli ndani yake.

Hitimisho

Serikali imejipanga vizuri kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha na udanganyifu katika shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini. Nitoe wito kwa wadau wote wa sekta ya madini kufanya kazi zao pasipo udanganyifu. Wote watakaopatikana kutenda kosa hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao na kuzuiwa kujihusisha na shughuli za madini hapa nchini.

By Jamhuri