Mwaka 1946  nilipangiwa na mkoloni kuwa Afisa Kata mashuhuri iliyojulikana kama Liwale, wakati huo ilikuwa na watu wapatao kama elfu mbili tu na kwa kweli walikuwa wengi kiasi cha kunifanya nigawe maeneo mengine yatawaliwe na vijana wenzangu niliowaamini.

Wakati huo nilikuwa natoa ripoti kwa Area Commission (Mkuu wa Wilaya) aliyekuwa akikaa na kuishi  Kilwa, ilitakiwa kila baada ya miezi mitatu nimpelekee taarifa za makazi na maendeleo. Nilikuwa natembea kwa miguu kuipeleka ripoti, mara chache nilikuwa nanyeshewa mvua na ripoti kuloa lakini nillihakikisha kila baada ya miezi mitatu anapata ripoti.


Bado nina kumbukumbu kuwa tulikuwa hatulipwi kitu chochote kutokana na kazi hiyo, wala tulikuwa hatuna posho yoyote ya safari au kujikimu zaidi ya kufanya kwa mgongo wa utumwa ambao baadaye tulifikia hatua ya kusema inatosha tunahitaji kupata uhuru na kujitegemea sisi wenyewe.


Kwa wale wasiojua urefu wa safari hiyo wanaweza kuuliza kwa watu wa Kusini mwa Tanzania na hasa wakazi wa Mkoa wa Lindi, wala hamna sababu ya kuwa na shaka ukweli unajidhihirisha kwa afya nilionayo leo kwa kuishi miongo kadhaa kutokana na mazoezi hayo.


Miaka kadhaa baada ya uhuru bado maeneo mengi yalikuwa ni magumu kutawalika kutokana na taarifa za uhuru kutofika haraka na wengine kuzoea hali ya kutawaliwa, hivyo wengi wao walikuwa bado katika kasumba ileile ya ndio bwana, hiyo ilitokana na tatizo la mawasiliano tuliyokuwa nayo wakati ule. Ikumbukwe kuwa redio pekee ilikuwa Redio Dar es Salaam na makao yake yalikuwa hapo Karume jijini Dar es Salaam, karibu na kiwanda cha bia.


Maisha ni safari ndefu, tunaoweza kujua ni wachache na wale wanaopenda kufuatilia historia ya zamani kama wapo, ambao wanajua na kuthamini tulikuwa wapi, tuko wapi leo na tunakwenda wapi kesho na hatima ya taifa hili ambalo kwa uhakika ni kubwa kuliko taifa lolote afrika mashariki kwa upendeleo wa mipaka ya wakoloni lakini yenye faida kwa taifa letu.


Wanangu leo nimeanza kutoa taarifa hii ambayo siyo muhimu sana kwenu lakini nimeona ni vema nikaanza hivyo ili mpate kujua na kuelewa ninachotaka kuzungumzia kwa maana ya masikitiko makubwa niliyonayo moyoni kwa kuona jinsi ambavyo tunachezea rasilimali tulionayo kwa faida ya wachache waliotukuka kupata nafasi ya kucheza na mali ya taifa hili.

 

Wanangu kwa bahati mbaya sana nasema teknolojia imewafikia katika kipindi ambacho unaweza kufanya jambo lolote ukiwa umeketi nyumbani kwako tofauti na enzi zetu ambapo ulibidi kutumia nguvu kutembea au kuwasiliana kwa njia yoyote na umbali usiomithilika.

 

Kumbukeni enzi zetu tulikuwa hatuna usafiri wa magari kama sasa, tulikuwa hatuna mawasiliano ya simu kiurahisi kama sasa, tulikuwa hatuna simu za viganjani kama ambavyo sasa mna mitandao mingi kwa gharama nafuu na vilevile tulikuwa na mikongo michache ya masafa ya redio na siyo televisheni kufanya watu wengi wapate taarifa kwa wakati mwafaka, lakini pia tulikuwa hatuna hayo mawasiliano ya intaneti kama ilivyo leo.


Wanangu nasikia kuna namna nyingi zaidi za mawasiliano lakini vema nikakiri wazi kuwa sitaki kuendelea kusikia mawasiliano hayo kwa kuwa yanazidi kuninyong’onyesha nguvu kutokana na mateso niliyopata wakati wa ujana wangu.


Wanangu kama mmebahatika kutembea nchi hii kama mimi, hongereni na tutakuwa pamoja na hiki ambacho nataka kusema lakini kama bahati hiyo hujaipata basi naomba tushirikiane nami katika malalamiko yangu ambayo nataka leo niwaambie hao viongozi wetu.


Nchi hii ni kubwa sana, tofauti na unavyoingalia katika ramani ambayo labda unayo sebuleni kwenu au kama unasimuliwa. Nchi hii ina mbuga za wanyama na mbuga za wazi, ina sehemu ambazo huwezi kujua ni za wilaya gani hata tukidanganyana kwamba si kweli, kwangu mimi sitakubaliana kamwe labda iwe kwa sababu za kisiasa.


Nchi hii ina maeneo ambayo hayajawahi kutumika kwa shughuli yoyote ya kimaendeleo iwe ufugaji au kilimo, ni maeneo ambayo yapo lakini hayafanyiwi kazi yoyote ya kufikiriwa kwamba yanaweza yakaliingizia pato kubwa taifa letu maskini kwa kujitakia.


Wakati wa uhuru tulikuwa na sera ya kilimo cha kufa na kupona. Katika sera ile tulibainisha wazi kuwa kila raia mwenye umri wa miaka kumi na minane anapaswa kuwa na shamba la ekari moja kwa ajili ya lishe yake, vilevile ekari moja kwa ajili ya zao la biashara lakini hatukuishia hapo, tulisema kila kijiji lazima kiwe na shamba la ushirika ambalo wote tulilima na mazao yalikuwa ni mali ya kijiji. Ukitaka kuamini angalia mabohari ya ushirika karibu vijiji vingi vya zamani.


Sera hii haikutenganisha mwenye madaraka na asiye na madaraka hivyo kiongozi bora ni yule aliyetoa mfano wa shamba lake na mifugo yake, huo ndio ulikuwa ufahari wa kiongozi bora na hakuajiri mtu zaidi ya kufanya mwenyewe kazi hizo siku za mapumziko kama siyo kila siku baada ya kazi za taifa.


Julius alikuwa na shamba lake alilolima kwa mkono wake huko Mwitongo Butiama Musoma, kila mtu analijua hilo, alikuwa na shamba la miti aliyopanda yeye mwenyewe kwa kuwashirikisha wanaye ambao walikuwa hawajafikisha miaka kumi na minane. Alifanya hivyo kama kiongozi wa kuigwa na majirani zake wengi walijifunza kutoka kwake, halikadhalika Rashid pia hadi uzee wake unamkuta alikuwa akilima uyoga.


Tulikuwa na maafisa kilimo wengi waliohitimu kule Ilonga na Uyole na waligawiwa karibu kila kata ili watoe mafunzo kwa wakulima wengine. Walifanya kazi hiyo kwa moyo mkunjufu kabisa, nakumbuka miaka kadhaa iliyopita wakati huo nikiwa Ilula mkoani Iringa tulikuwa tukifundishwa jioni chini ya mti matumizi ya vifaa na mbolea ili tupate mazao ya kutosha.


Sina hakika ni kitu gani kimetokea hadi tumesahau kilimo na kubaki na biashara, sera ya kilimo imekufa na imekuja sera mpya ya kila aliyefikisha miaka kumi na minane lazima awe mfanyabiashara, mbali na hiyo sera sasa mikopo inatolewa kwa wafanyabiashara tu na siyo wakulima.

Wanangu siku za hivi karibuni tumekuja na sera ya kilimo kwanza ambayo inazungumzwa katika mafaili na maofisa wengi ambao pia nina wasiwasi kama wanajua hata bei ya jembe ama mbolea. Kilimo kwanza kimekuwa ni ufahari kuuzungumzia mjini badala ya kuonyesha mifano kwa wananchi wengi walioko vijijini kwenye aridhi ambayo ingeweza kutumika ipasavyo.


Vinafanyika vikao vya kilimo kwanza kwa miposho mikubwa lakini hatuna shamba la mfano na hakuna anayejua adha ya kushika jembe miongoni mwa hao wateuliwa wa kujadili mikakati na mipango madhubuti ya kilimo kwanza na wasiojua shamba linafananaje na mvua zinanyesha lini. Mimi nilitembea umbali wa ajabu kwa siku kadhaa bila posho wala fedha ya kujikimu.


Nasikitika kwa sababu kama tungeamua kwa dhati ya moyo wa kweli kilimo kisingejadiliwa mijini badala yake tungewapa fursa wale wanaoishi katika mapori makubwa yanayoweza kufumuliwa na kuwa mashamba ya chakula, tungewakopesha vitendea kazi na matokeo yake tungezalisha ajira za kutosha kwa hao waliojifanya wafanyabiashara wakati wana nguvu za kuingia shambani.


Wanangu naomba muangalie mbuga zilivyo mtembeapo, anza Kusini hadi Kaskazini Mashariki ya mbali na Dar es Salaam hadi Magharibi halafu jiulize kwanini taifa hili linaendelea kuwa na njaa, kwanini maskini, kwanini tumeacha sera ya kilimo cha kufa na kupona, kwanini viongozi wetu siyo wa mifano, kwanini tugeuze ajira ni siasa na biashara na nini hatima ya taifa linalofuga wavivu na watunga sera mezani.


Sipati jibu leo lakini nasikia kuna bomu linaloweza kulipuka wakati wowote la vijana na ajira, kumbe tungeweza kuzuia kwa kutoa mikopo na kuwapeleka katika mapori yale niliyokuwa napita enzi zile nikiwa kule Liwale kwenda Kilwa.

Kidumu chama chenu na sera mlizonazo.

Wasalaam.

Mzee Zuzu

Kipatimo.


By Jamhuri