TOKYO, JAPAN

Japan imetangaza hatua za tahadhari baada ya kuibuka wimbi jingine la maambukizi ya virusi vya corona. Nchi hiyo imetangaza kutenga kiasi cha yen trilioni moja (dola bilioni 9.1 za Marekai) kukabiliana na wimbi hilo.

Hatua hiyo ya serikali imeliweka Jiji la Tokyo, ambao ndio mji mkuu wa nchi hiyo katika hali ya tahadhari kwa mara ya nne.

Aidha, hali ya tahadhari imetangazwa pia katika kisiwa kilichopo kusini mwa nchi hiyo cha Okinawa. 

Hatua hizo zilizotangazwa na serikali zitashusha matumizi kwa kiasi cha yen trilioni 1.2, kwa mujibu wa Toshihiro Nagahama, mchumi mkuu wa taasisi ya Dai-ichi Life Research Institute.

“Ni dhahiri kuwa kutokana na hatua zinazochukuliwa sasa na serikali kutakuwa na makatazo katika shughuli za uchumi,” Nagahama anasema katika taarifa yake ya utabiri wa nini kinaweza kutokea chini ya hali hiyo.

Aidha, alibainisha kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha zaidi ya watu 55,000 kupoteza ajira zao katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Hatua hizo za tahadhari kwa Tokyo na Okinawa zilianza kutumika juzi Jumatatu na zinatarajiwa kudumu hadi Agosti 22, mwaka huu. Hatua zilizotangazwa pia zitaathiri michezo ya Olympic ambayo imepangwa kuanza Julai 23 jijini Tokyo.

Chini ya hatua hizo za tahadhari, migahawa na baa zitazuiliwa kuuza pombe wakati zikitakiwa kupunguza muda wake wa kuwa wazi.

Nagahama anasema hatua hizo zitashusha pato la taifa kwa yen triloni moja, ikiwa ni sawa na anguko la uchumi la asilimia 0.7 kati ya Julai na Septemba, takriban anguko la asilimia tatu kwa kipimo cha mwaka.

Tathmini hiyo haikuhusisha thamani ya bidhaa zitakazoingizwa nchini humo.

Kutangazwa kwa hali hiyo ya tahadhari kunafuatia kuibuka kwa wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona baada ya kuondolewa kwa hatua za tahadhari zilizotangazwa Juni 20, mwaka huu.

Takahide Kiuchi, mchumi wa Nomura Research Institute, alitoa makadirio kama hayo akisema uchumi utasinyaa kwa yen trilioni 1.03.

Aidha, alikadiria hasara nyingine ya yen bilioni 146.8 iwapo michezo ya Olympic itafanyika bila mashabiki kuhudhuria.


Mabango makubwa ya matangazo jijini Tokyo yakimuonyesha Waziri Mkuu wa Japan, Yoshihide Suga, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza uamuzi wa serikali kutenga yen trilioni moja kukabiliana na maambukizi ya corona nchini humo.
541 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!