Albert Einstein, mmoja wa binadamu wenye akili za kiwango cha juu katika karne ya 20, alipata kusema: “We cannot solve our problems with the same thinking we used when we created them.” [Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kutumia mawazo yale yale tuliyotumia kuyatenda].

Kila nikiwatazama Waziri na Naibu Waziri wa Afya, ninakumbuka maneno haya ya Einstein. Taarifa za serikali zinaonyesha kuwa chanjo milioni moja za UVIKO-19 zimeletwa nchini.

Awali, ulitolewa mwongozo wa watu watakaochanjwa wawe wenye umri wa kuanzia miaka 50 na wenye magonjwa sugu. Kweli ikawa hivyo. Vijana na wasio na maradhi sugu waliofika kwenye vituo walinyimwa chanjo. Matarajio ya viongozi yalikuwa makubwa. Walidhani watakaojitokeza kuchanjwa wangekuwa wengi. Mambo yamekuwa tofauti. Hadi ninaandika makala hii, takwimu za serikali zilionyesha waliopata chanjo wamevuka kidogo watu laki tatu.

Ni kwa uchache huo, haikushangaza kuona serikali ikitoa ruksa kwa yeyote anayekubali kuchanjwa afike kituoni apate huduma hiyo. Hakuna tena maswali ya umri au magonjwa sugu. Kwa wataalamu wa tathmini, idadi hii ni kielelezo cha kufeli kwa mpango wa chanjo.

Kwanini tunafeli? Kunaweza kutolewa sababu nyingi. Mathalani, tunaweza kusema elimu ya chanjo bado haijawaingia wananchi. Tunaweza kusema kwa kuwa ni hiari kuchanja, ndiyo maana waliojitokeza ni wachache. 

Tunaweza kudai kuwa wananchi bado wanaamini watapona kwa nguvu za nyungu na maombezi. Tunaweza kutafuta na hata kuumba majibu mengi sana alimradi tu tuhalalishe mkwamo huu.

Lakini kuna jambo moja lisilosemwa wazi. Tumebaki tukimung’unya mung’unya maneno. Kunatakiwa atokee mtu mwenye upungufu wa akili aseme bila kuwaondoa Waziri na Naibu Waziri wa Afya, si chanjo ya UVIKO-19 pekee, bali mambo mengi katika wizara hii yatakwama. Historia ya wawili hawa inajenga uhalali wa wananchi kutowaamini. Binadamu ni wepesi kubadilishwa kwa masuala ya kisiasa na mengine mepesi, lakini linapokuja suala la afya wanakuwa wagumu mno kubadilika. Elimu ya ‘hatari za chanjo’ waliyopewa na hawa mawaziri iliwaingia, kwa hiyo si jambo jepesi kuwabadili.

Wakati wa Rais John Magufuli walishiriki kuwaaminisha Watanzania kuwa chanjo ni mbaya. Hazifai. Waliweka kando akili za usomi wao wa udaktari na kukubali kwenda na mdundo wa bosi hata kama kitaaluma nafsi ziliwasuta. Hawakuwa na ujasiri kama wa Ndugulile ambaye alizungumza kitaaluma, akatumbuliwa, lakini baadaye akarejeshwa japo katika wizara nyingine. Tafsiri yake ni kuwa aliyemteua alijua amefanya kosa kumtumbua.

Waziri wa Afya wa sasa na naibu wake waliwaaminisha Watanzania kuwa chanjo ni kitu kibaya, isipokuwa dawa za kujifukiza na za lishe. Sayansi wakaiweka kando, na mbaya zaidi wananchi wakaamini chanjo ni mpango wa mabeberu kutuua ili wafaidi rasilimali zetu.

Baada ya kufariki dunia kwa Rais Magufuli, viongozi hao hao waliohubiri ubaya wa chanjo ghafla wakabadilika na kuendana na msimamo wa Rais Samia Suluhu Hassan. Wamejitahidi kujitetea na kueleza sababu za kupinga na hatimaye kubadilika, lakini akili za watu wengi bado zimegoma kukubaliana nao.

Wakristo wanaosoma Agano Jipya wanajua namna Mtume Paulo (Sauli), aliyejulikana kwa kuwaua wafuasi wa Yesu, alivyopata shida baada ya kutokewa (na Yesu) na kumtaka awe mfuasi wake. 

Watu walioamini Paulo alikuwa muuaji, iliwachukua muda mrefu kuamini kama kweli mtu huyo alikuwa amebadilika na kuwa mfuasi wa Yesu.

Hili linaweza kutokea kwa Gwajima na Mollel, lakini huenda hadi tukashuhudia utii huo wa wananchi, vifo vinavyotokana na UVIKO-19 vitakuwa vimetupukutisha. 

Shaka yangu ni kwa hizo chanjo milioni 17 zinazoletwa! Kama kwa hizi milioni 1 tumesuasua, lazima tujipange kwa huo mzigo unaoletwa. Japo mwitikio ni mdogo, hiyo haiondoi ukweli kuwa chanjo hizi zinaokoa maisha.

Mamlaka ya uteuzi haipangiwi. Inashauriwa. Nadhani wakati umefika kwa mamlaka ya uteuzi kuwapata wapambanaji wapya wanaoaminika kwenye vita hii. 

Hali ilivyo ni kuwa hawa wawili hahawezi kubadili fikra za watu hata wakawaamini wao na chanjo. Ili kupata matokeo chanya, kuwabadili hawa wawili ni jambo lenye afya.

Tunajifunza nini? Tunachojifunza kwenye sakata hili la chanjo kinatupeleka kwenye mambo mengine mazito ya kitaifa. Mara kadhaa tumekosa consistence kwenye mambo mazito. Hatupaswi kubadilikabadilika. Tumeona tunavyobadilika kwenye vikokotoo, kwenye uteuzi wa ma-DED na ma-RC. 

Tumebadilika kwenye bei za mafuta, tunabadilika kwenye tozo za miamala, na kadhalika. Kubadilikabadilika japo kunatafsiriwa kuwa ni jawabu la ‘usikivu wa serikali’, kunawafanya wananchi wakose hakika ya mambo yanayoamuliwa na serikali.

Mathalani, haiwezekani watumishi wa serikali leo waseme chanjo ni hatari, lakini kesho hao hao wabadilike na kusema chanjo ni nzuri. Mara nyingi watu huchukua kauli ya awali wakiamini serikali mara zote hutangaza jambo ikishapata uhakika. Serikali haina taratibu za ramli. Ramli ni za watu au taasisi zisizo makini.

Nihitimishe kwa kushauri kuwa ili tufanikiwe kwenye vita hii ya UVIKO-19, na ili chanjo zikubaliwe na wengi, hatuna budi kuwa na sura mpya katika Wizara ya Afya. Tukiendelea na hawa hawa, kuna wakati tutaingia gharama ya kuteketeza chanjo zilizokwisha muda wa matumizi.

By Jamhuri