Wizi wa kutisha

>>Bima feki za magari zatamalaki kila kona Dar
>>Mtandao wajipenyeza Bandari, TRA, SUMATRA
>>Yanayopata ajali, kuua wananchi yatelekezwa
>>Kamanda wa Polisi aeleza mchongo wote ulivyo

 
DAR ES SALAAM

NA MANYERERE JACKTON

Mtandao wa utapeli unaowahusisha wafanyabiashara na watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za serikali umebainika kuwapo kwenye biashara ya usafirishaji wa magari nje ya nchi (IT).
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa miezi mitatu umebaini mtandao huo unaowahusisha baadhi ya watendaji waandamizi katika Bandari ya Dar es Salaam, Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na kampuni za bima.
Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) Kanda ya Kaskazini, Joe Simwanza, amezungumza na JAMHURI ofisini kwake mpakani Nakonde, Zambia na kusema utapeli huo unatishia kuua biashara ya usafirishaji wa magari yanayokwenda nchini humo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Anasema yamekuwapo malalamiko mengi na ya muda mrefu ya Wazambia kuhusu utapeli huo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na mamlaka upande wa Tanzania kumaliza kero hiyo.
Kwa sasa Serikali ya Msumbiji iko kwenye upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Beira, na kukamilika kwake kunaelezwa kuwa huenda kukadhoofisha usafirishaji wa magari na shehena nyingine kupitia Dar es Salaam.
Uchunguzi umebaini kuwa karibu magari 300 yanasafirishwa kwenda nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam kila siku, ambapo wenye magari hayo wanauziwa bima za kitapeli.
Bima hizo hazina viwango maalumu vya malipo, badala yake kinachofanywa ni makubaliano kati ya muuzaji na mnunuzi.

JAMHURI tumenunua baadhi ya bima hizo kwa kiwango cha Sh 15,000; Sh 20,000 na Sh 25,000 kwa kila stika. Pia tumenunua bima ya COMESA (Umoja wa Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika) kwa Sh 40,000. Tanzania ilijitoa katika umoja huo mwaka 1999.
Nchi wanachama wa COMESA ni Burundi, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Djibouti, Misri, Eswatini (Swaziland), Eritrea, Ethiopia, Kenya,  Libya, Madagascar, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Tunisia, Uganda na Zambia.
Shirika la Bima la Taifa (NIC) ndilo lililokabidhiwa dhima ya kuuza stika za COMESA; lakini kwa sasa zinauzwa mitaani kama njugu zikiwa zimerudufiwa.
Msimamizi wa uuzaji wa stika hizo kutoka NIC aliyejulikana kwa jina la Holo, amekataa kuzungumza kwa masharti kuwa hadi apate kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Samwel Kamanga. Hata hivyo, Kamanga hakuweza kupatikana kutoa kibali kwa kile kilichoelezwa kwamba alikuwa kwenye mkutano wa wadau wa bima mkoani Tanga.

Stika za kampuni za bima zinazouzwa kwa wanaosafirisha magari ya IT zinapatikana hadharani, lakini wakati mwingine kwa kificho pale polisi wanapokuwa wakiendesha msako wa kuwakamata wahusika.
Zimezagaa katika maeneo yote yanayozungumza Bandari ya Dar es Salaam na katika vibanda vilivyopo Mnara wa Saa, Water Front, Gate No. 2, Dawasa, Mnazi Mmoja na Kariakoo.
Hapo Kariakoo, yupo mtaalamu wa kurudufisha stika hizo anayejulikana kwa jina maarufu la Mjaluo. Kwa Mjaluo, kitabu cha stika huuzwa kuanzia Sh 250,000 hadi Sh 400,000 na mteja anapata stika za kampuni yoyote ya bima anayohitaji.
Kutoka kwake, walanguzi ndipo hupata stika wanazokwenda kuuza rejareja. Kwa kufanya hivyo, ndiyo maana bei ya stika hubadilika kulingana na muuzaji anavyomwona mnunuzi alivyo.
Wanauza kuanzia Sh 15,000 alimradi kuhakikisha wanapata faida kutoka kwenye kiwango walichonunua kitabu kutoka kwa Mjaluo.

JAMHURI limetumia nyaraka za magari ya IT yaliyokwisha kusafirishwa nje ya nchi kununua stika mpya za bima. Limetumia nyaraka hizo kununua stika za bima kutoka kwa kampuni tano tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, bila hata wahusika kuona magari.
Namba za stika zilipoingizwa kwenye mtandao wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), zilisomeka kuwa zimeshatumika. Hata hivyo, bado stika hizo feki zinaweza kutumiwa kwa kubandikwa kwenye gari lolote la IT. Kwa kawaida, namba za magari ya IT huwa ni tarakimu nne za mwisho za chesesi ya gari husika.

Mtandao wa fedha

Waagizaji wa magari kutoka mataifa ya Zambia, Malawi, DRC, Rwanda, Burundi na Uganda hutakiwa kulipa dola 200 (wastani wa Sh 450,000) za bima kwa gari. Fedha hizo hulipwa ili pamoja na mambo mengine, zigharimie bima ya gari kuanzia linakotoka hadi kwa mmiliki. Kiasi hicho pia huhusisha malipo ya dereva wa kulipeleka hadi mpakani.

Bima hizo zimebainika kuwa si lolote, wala chochote, kwani magari mengi ya IT yanapopata ajali madereva kwa kuwa ni sehemu ya mchongo huo huzibandua na kutoweka.
Licha ya wanunuzi wa magari kutozwa fedha za kutosha kuwalipa madereva wanaopeleka magari hayo mipakani, imebainika kuwa baadhi ya kampuni za uwakala huwalipa madereva wao Sh 300,000 kwa mwezi, na Sh 100,000 kwa kila gari wanalopeleka mpakani.
Kiwango hicho kidogo cha fedha kinaelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya madereva hao wawe kwenye mwendo kasi muda wote, hivyo kupata ajali mara kwa mara.
“Dereva analipwa Sh 100,000. Humo anatakiwa ale, na ikiwezekana alale nyumba ya wageni, akifanya yote hayo habaki na kitu,” kimesema chanzo chetu.

Kwa kukabiliana na hilo, magari hayo yamekuwa yakisafirishwa usiku, tena yakiwa yamepakiwa abiria ingawa sheria za usalama barabarani zinazuia.
Madereva wanapoendesha usiku uhakikisha wanawasili Tunduma mapema alfajiri na hapo hukabidhi gari kwa wahusika kabla ya kupanda mabasi ya alfajiri hiyo hiyo kurejea Dar es Salaam.
“Tunafanya hivyo kukwepa kulala gesti. Ukilala gesti utakosa nauli ya kurudi Dar es Salaam,” amesema dereva mmoja.

Wanaofaidi fedha za bima

Imeelezwa kuwa fedha zinazotokana na utapeli kwenye stika za bima ni mapato ya mtandao mahususi wenye nguvu na ushawishi.
Baadhi ya wahusika tuna majina na vyeo vyao, lakini kwa sababu za kitaaluma tunaendelea kuwahifadhi hadi hapo tutakapozungumza nao. Baadhi yao wameulizwa na kuahidi kutoa majibu baadaye.
Miongoni mwao ni baadhi ya watendaji waandamizi katika Bandari ya Dar es Salaam, SUMATRA na mfanyakazi mmoja mwanamke katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mwanamke huyo ana watoto wake wawili wanaofanya kazi ya uwakala wa kununua na kuuza magari ughaibuni.
Uchunguzi umebaini kuwa kigogo wa Bandari ya Dar es Salaam ni mbia kwenye mpango wa kuajiri madereva wanaosafirisha magari ya IT pamoja na uuzaji wa stika hizo za bima.

Ajali za magari

Mwandishi wa habari hizi amesafiri hadi Mbala, Zambia na kushuhudia magari mengi yaliyopata ajali upande wa Tanzania yakiwa yametelekezwa njiani – katika vituo vya polisi na kwenye yadi nchini Zambia.
Magari yanayopata ajali mbali na Tunduma yamehifadhiwa katika vituo vya polisi, lakini yaliyopata ajali kuanzia Mbeya na kuendelea, hukokotwa na kampuni ya uwakala [jina tunalo] na kuyavusha hadi kwenye yadi nchini Zambia.
Baadhi ya maeneo ambako kuna magari ya IT yaliyopata ajali ni Kituo cha Polisi Mikumi, Iringa, Ifunda na Makambako nchini Tanzania. Kwa upande wa Zambia, magari hayo yako kwenye eneo linaloitwa “Yard ya Mzungu”, Barabara ya Mbala, kilometa kadhaa kutoka mpakani Nakonde.

Magari hayo kabla ya kuhamishiwa “Kwa Mzungu” yalikuwa kwenye yadi ya Inland Investment Limited, iliyopo Nakonde. Yadi hiyo kwa sasa inakarabatiwa.
Baada ya ajali madereva huyaletekeza, hivyo walioyanunua hukosa vyote – gari na fidia. Kule yanakohifadhiwa, imebainika kuwa vifaa vingi huibwa na waliopewa dhamana ya kuyalinda.
“Tunapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi (Zambia), gari linapoharibika kabisa hawana namna ya kulipwa fidia licha ya kuyakatia bima, hii inasikitisha sana,” anasema Naibu Kamishna Simwanza wa ZRA.
Kituo cha Polisi Ifunda kumetunzwa magari kadhaa ya IT yaliyopata ajali na kuua waenda kwa miguu na abiria, lakini hakuna maelezo ya madereva wala wamiliki wake.

Polisi aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina anasema ajali zaidi ya asilimia 90 hutokea alfajiri au asubuhi, muda ambao madereva huwa wamechoka. Pamoja na kuutumia usiku kusafiri ili wawahi kurejea Dar es Salaam kwa mabasi ya asubuhi, sababu nyingine ya kusafiri kwao usiku ni kutokana na kuwakwepa polisi kutokana na mwendokasi na kupakia abiria.
Katika mji wa Mbala, mabaki ya magari ya IT zaidi ya 30 yameonekana, na kama ilivyo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ZRA huuza mabaki hayo baada ya muda uliopangwa wa miezi mitatu kupita bila wenyewe kujitokeza kuyachukua.

Je, bima ni halali?

Sheria ya Usalama Barabarani inaagiza kuwa chombo cha moto kilichosajiliwa nchini lazima kiwe na bima. Gari lenye namba za chesesi, kwa mujibu wa sheria, halijasajiliwa nchini.
Sheria inatoa mwanya kwa gari kutolewa bandarini hadi nyumbani au karakana likiwa na kibao maalumu cha kuonyesha kuwa halijasajiliwa. Malipo kwa kibao hicho ni Sh 5,000.
Magari ya IT, kwa kuzingatia sheria hiyo, hayana usajili hapa nchini, badala yake namba (tarakimu nne) zinazoonekana kwenye kibao cha utambulisho wa gari ni za kwenye chesesi. Wataalamu wa usalama barabarani wanasema kwa kuzingatia sheria hiyo, ni makosa kulikatia gari bima kwa kutumia namba za chesesi.
“Mfano mzuri ni bima ya nyumba. Huwezi kukatia bima matofali au mifuko ya saruji iliyoko dukani. Hata nyumba ikijengwa lazima kiwanja kiwe na hati ndipo ukikatie bima. Sasa kukatia bima magari kwa kutumia chesesi ni sawa na kukatia bima nyumba kwa kutumia matofali,” amesema mtaalamu huyo.

Msimamo wa TIRA

Ofisa Mawasiliano wa TIRA, Oyuke Filemon, anasema bima za magari ya IT (yellow card) zinatolewa na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Anasema ingawa Tanzania si mwanachama wa COMESA, mizigo mingi ya nchi wanachama zilizo Kusini, Mashariki na Kati mwa Afrika inapitia Tanzania.
“Kama kuna kampuni tofauti zinazotoa yellow card, inapaswa wapate kibali kutoka NIC,” anasema.
Oyuke anasema bima zinazotambulika kwa magari ni mbili –Third Part na Comprehensive kwa magari yaliyosajiliwa nchini. Third part, pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni Sh 118,000; ilhali comprehensive hutegemeana na thamani ya chombo kinachokatiwa bima, thamani ya chini ikiwa ni asilimia 5 ya thamani ya gari.

Anakiri kuwa mara kadhaa maofisa wa TIRA wameshirikiana na polisi kuwakamata wanaojihusisha na uuzaji wa stika feki za bima.
“Tuna kikosi chetu cha udhibiti dhidi ya wanaokiuka sheria za bima, tunajua pale nyuma ya TPA (Mamlaka ya Bandari) ndiyo wanauzia hapo,” anasema Filemon.
Wakati Oyuke akisema hivyo, Meneja wa Mifumo wa TIRA, Aron Mlaki, anasema bima za muda mfupi (short cover) zinatambulika na ni mahsusi kwa ajili ya kuwalipa watu wanaopata ajali au madhara.
Kamishna Mkuu wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware, amezungumza na JAMHURI ofisini kwake Dar es Salaam na kusema suala la magari ya IT ni changamoto kubwa.
Anasema kumekuwapo magenge ya wanaouza stika feki za bima na TIRA imejitahidi kukabiliana nao.

Anasema Mamlaka inaangalia namna ya kuingiza yellow card za COMESA kwenye mfumo wa TIRA wa utambuzi ili kukabiliana na wimbi hilo.
“Tunashindwa kuingilia moja kwa moja hili suala kwa sababu ni la kikanda, kuna mikataba iliyosainiwa kwa ajili hiyo kwa hiyo tunapaswa kufuata taratibu,” anasema Dk. Saqware.
Anasema kwenye mabadiliko ya kisheria yaliyofanywa, mizigo inayoingia nchini kwa maji, barabara na anga sasa inakatiwa bima hapa hapa nchini.

Kauli ya Polisi Usalama Barabarani

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Fortunatus Musilimu, anasema chombo cha moto hakiwezi kukatiwa bima kama hakijasajiliwa.
“Kama gari linatolewa bandarini kwenda nyumbani, na likiwa halina bima, kinachofanywa ni wakala kukata kibao cha gereji. Hizo namba sheria inataka gari litembee mwisho saa 12 jioni. Baada ya hapo halitakiwi kutembea.
“Na iwe kweli hilo gari linatolewa bandarini kwenda nyumbani likisubiri bima, au kwenda gereji; na si kinyume cha hivyo. Likikutwa nje ya hapo linatembea litakamatwa kwa mujibu wa sheria. Siku hizi mambo mengine ni online [mtandao], kwa hiyo gari linaweza kulipiwa bima online na likatolewa bandarini likiwa na bima. Hiyo ni kwa magari yanayosajiliwa hapa nchini.

“Hizo bima za kwenye IT hapo ni ubabaishaji. Najua zipo bima za COMESA ambazo ni halali kisheria. Lakini hizi nyingine ni uhuni tu, pale kuna uhuni, lakini uhakika wa haya utaupata TIRA,” anasema.
Anasema magari ya IT yana namba yanazopewa Bandari, na kwamba mfumo uliopo unawezesha zisomwe pia TIRA.
“Kuna ubabaishaji mwingi kwenye IT maana hata madereva wakipata ajali wanabandua hizo bima halafu wanakimbia. Kama bima ni halali kwanini wabandue bima na wakimbie? Kuna matapeli wengi sana,” anasema.
Kamanda Musilimu anasema bima za COMESA zinapigwa vita, na sababu kuu ya kuwapo vita hiyo ni masilahi ya makundi yanayojitafutia fedha.

“Wanapigwa vita, ni vita kweli kweli wala siyo ndogo,” anasema Kamanda Musilimu.
Usikose matoleo yajayo kusikia kauli ya Bandari, TRA na SUMATRA.
Uchunguzi huu umefanywa kwa ushirikiano kati ya Gazeti la JAMHURI na Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).