Home Sitanii Ya Sabaya, tuandike majina yetu vizuri

Ya Sabaya, tuandike majina yetu vizuri

by Jamhuri

Na Deodatus Balile

Kwanza, naomba kabla sijaingia katika undani wa mada nichukue fursa hii adhimu kuwashukuru wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kunichagua kuwa Mwenyekiti wa TEF kwa kishindo.

Sitanii, ushindi wa asilimia 72 walionipa wahariri hawa ni imani kubwa isiyostahili kubezwa kamwe. Wana matumaini makubwa na uongozi wangu na hapana shaka wanatarajia niwalipe imani kwa kutekeleza ahadi yangu ya Maendeleo ya Taaluma, Kujenga Mifumo na TEF imara.

Nampongeza mshindani wangu, Neville Meena, ambaye wapiga kura walimpa asilimia 27 ya kura zote zilizopigwa. Nampongeza Makamu Mwenyekiti, Bakari Machumu, aliyeshinda kwa kishindo pia na wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji ya TEF (KUT). Kwa pamoja tunayo kazi kubwa ya kufanya ili kuendeleza taaluma ya habari nchini.

Namshukuru Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, aliyetupa heshima kubwa ya kuja Morogoro kufungua mkutano mkuu wa mwaka, uliokwenda sambamba na mkutano wa uchaguzi ulionipa ushindi.

Waziri Mkuu na serikali kwa ujumla wametuonyesha imani kubwa ambayo tangu TEF ianzishwe mwaka 2008, haijawahi kupata heshima hii. 

Nasema asante sana Mhe. Majaliwa na nikuahidi kuwa TEF na tasnia ya habari kwa ujumla itafanya kazi kwa karibu na serikali kujenga taifa la uwazi, uwajibikaji na lenye kujali haki na maendeleo ya watu.

Niliahidi kwenye mkutano wa Morogoro kuwa TEF ni chama cha kitaaluma na kitafanya kazi ya kitaaluma bila ubaguzi wala upendeleo. Tutafanya kazi na serikali, CCM, CHADEMA, CUF, ACT, NCCR na vyama vyote vya siasa bila kujali ni chama tawala au cha upinzani. 

Tutafanya kazi pia na jamii kwa ujumla kwa maana ya mtu mmoja mmoja na taasisi zilizomo katika taifa letu. Nawashukuru Watanzania wote waliopata fursa ya kunipongeza na ninawaahidi sitawaangusha.

Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema: ‘Ya Sabaya, tuandike majina yetu vizuri.’ Nafahamu kesi ya Sabaya iko mahakamani na ninaheshimu Kifungu cha 114(1)(d) cha Kanuni ya Adhabu Sura 16 ya Sheria za Tanzania kinachozuia kujadili suala lililoko mahakamani kwa nia ya kuathiri mwenendo wa kesi.

Kwa mantiki hiyo, sitayajadili makosa anayoshitakiwa nayo Sabaya, bali nitagusia haja ya kusafisha mapito yetu tunapokuwa na madaraka.

Njia za kupata madaraka zinatofautiana. Wapo wanaoyasotea, wapo wanaoyapata ‘kishikaji’, wapo yanaowadondokea kama ‘zali la mentali’ na wengine Mungu anajua, kwani akina ‘sangoma’ wanahusika.

Sitanii, bila kujali umepataje madaraka, jambo la kwanza binadamu unapaswa kujiepusha na ibilisi la ‘roho mtakavitu’, bali kwa neema za Mungu akujalie uwe na ‘Roho Mtakatifu.’

Ubahatike kuwa na mapaji angalau ya ucha Mungu, utii, adabu, hekima na heshima. Tukiwa viongozi hakika sisi ni watumishi. Tunastahili kuwa wanyenyekevu. 

Maisha yetu ya uongozi tuyawekeze katika uhusiano mwema na watu, tutatue shida za watu na kuwawezesha kutimiza malengo yao, kwa kuwasogezea fursa wanazostahili hata kama zitakuondoa wewe katika nafasi unayoishika, bali akaingia mwingine na kufanya vizuri zaidi kazi yako.

Ninaposema utumishi wa umma, maana yake ni utumishi wa watu. Ukiona unatamani vitu, kwa maana ya mali na kuwaonyesha watu upeo wa madaraka yako kwa kuwaburuza wengine na kukanyaga haki zao, hakika ujue wewe unaliandika vibaya jina lako.

Tukiandika vizuri majina yetu hatutalazimika kuacha mafungu ya kulipa watu wa kututetea kipindi tupo magerezani au makaburini, bali mema tuliyoyatenda yatatusemea, yatatutetea, bila chembe ya kumlazimisha awaye.

Sitanii, ndiyo maana katika nchi hii kuna vijana wengi wanaitwa Julius, si kwa uzuri wa jina, bali wazazi waliupenda ufanisi wa Julius Nyerere, hivyo wakaona familia zijinasibu kwa angalau kuwa na ‘Nyerere wao’ katika familia wakimwita kwa jina la kwanza la Mwalimu; Julius.

Sina uhakika kama Uganda leo kuna familia yenye hamu ya kumpa mtoto wao jina la Idd Amin. Nimesikia Ujeruman ni marufuku mtoto kupewa jina la Adolf au Hitler.

Sitanii, majina yanatolewa kwa kazi iliyotukuka. Hata ukifa jina lako linadumu milele kwa kazi uliyoifanya. Msiniulize kama leo kuna Mtanzania ana hamu ya kumbatiza mtoto wake jina Sabaya au wengine ninaosikia wanatajwa kuwa si muda wataitwa Upanga kusaidia upelelezi. Tuandike majina yetu vizuri.

Kwa sisi tuliobahatika kuishi angalau nusu karne, walau tumeona mengi. Natamani vijana wanaopewa madaraka wangekuwa na fursa ya kunisikiliza. 

Nawaona wengi, wakiwa wakuu wa wilaya, mikoa, manaibu waziri au mawaziri na wakati mwingine wakurugenzi au maofisa waandamizi wanavyopandisha mabega.

Sitanii, leo unainua simu unawapigia mawaziri wazee kama akina mzee William Lukuvi, George Simbachawene, Balozi Liberatha Mulamula… wanapokea simu na wanakujibu unalouliza, ila unawapigia mawaziri ‘Yoso’, hata ukituma meseji, hawajibu. Mabega yako juu.

Kuna kijana mmoja, huyu ni muungwana. Ni Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo. Akiwa DC Kinondoni, kuna RC alimkemea hadharani, yeye aliyameza machungu, lakini hadi leo humkuti Chongolo akidharau rika lolote.

Sitanii, ninapowasema vijana, simaanishi waliomo serikalini peke yao. Hata vyama vya upinzani wapo ambao ni tabu. Walipopata ubunge, ilikuwa unawapigia simu hawapokei, ubunge sasa umeisha, tukikutana anakwambia: “Kaka shikamoo!!” Ukaka ulipotea akiwa mbunge. Ubunge umeyeyuka, ukaka umerejea. Ni shida.

Bahati mbaya vijana hawa wanasahau kuwa hatuwapigii simu kuwaomba chochote, bali kuwasaidia katika utendaji wao, kwa kuwaeleza wapi wanaharibu.

Ikitokea akakujibu, anakwambia: “Kwa hiyo unataka kufanyaje?” Unaona, heeee, huyu kajipanga kwa mapambano, si mazungumzo. Unachukua busara ya ‘aliye juu, mngoje chini.’

Sitanii, makala hii inaweza kuwa ndefu, ila niwashauri vijana waliopewa uongozi mambo kadhaa. Mosi, wanapaswa kufahamu kuwa wao ni binadamu na Watanzania kwanza, suala la madaraka ya uongozi au cheo ambacho ni dhamana ni nyongeza. 

Cheo kinaweza kuondoka wakati wowote, ukashushwa kwenye V8, ukaishia kuchuchumaa mahakamani ukiwa na pingu mikononi. Mifano ipo.

Pili, hakuna mtu aliyepata kuheshimika kwa kufanya uongozi usioheshimu utawala wa sheria. Unapopewa madaraka, ukifika ofisini, kwanza waheshimu uliowakuta, omba mwongozo wao, soma sheria na kanuni zinazotawala eneo unaloongoza. 

Utafahamu nini unaruhusiwa kufanya kisheria na nini si eneo lako. Bahati mbaya baadhi ya vijana wanatoa maelekezo hata kabla ya kuingia ofisini mara tu wanapoteuliwa. Hii si sawa.

Nisikuchoshe msomaji wangu, viongozi wetu wakiheshimu utu, wakasimamia haki za watu kwa mujibu wa sheria, watakuwa wamesuka mkeka wa utawala bora na wala hatutawaona mahakamani, na hata wakifariki dunia watabaki mioyoni mwetu. Tutayatetea majina yao bila ndugu kulazimika kukodisha watu wa kuyatetea. Mungu ibariki Tanzania.

You may also like