Na Deodatus Balile

Alhamisi, Aprili 10, 2021 Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 

Kwanza kabla sijaijadili bajeti hii, naomba nimshukuru Mheshimiwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kulialika Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa mwaliko maalumu kuwapo bungeni wakati bajeti inasomwa. Nasema asante sana, na heshima hii uliyotupa naamini itakuwa endelevu.

Nimefurahia utaratibu uliotumiwa kuwapokea wageni bungeni. Sisi sote ni Watanzania. Zamu hii tumeruhusiwa kuingia bungeni na simu zetu za mkononi, kalamu na viandikishi, kwa maana ya notebook

Utaratibu huu mzuri ulikamilishwa kwa hotuba ya bajeti kuingizwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango, kisha waalikwa wote tukapewa vitabu vya bajeti tukafuatilia. 

Kimsingi utaratibu huu ni mzuri na udumishwe. Hongera Mhe. Spika Ndugai kwa maboresho haya, maana zamani wageni hawakuruhusiwa kuingia hata na kalamu!

Sitanii, ninafahamu watu wengi wamejadili bajeti ya Serikali. Bajeti hiyo Waziri Mwigulu hakupata fursa ya kusoma kila kitu kilichopendekezwa na serikali. 

Hakika sisi tumeichapisha yote katika gazeti la Jumanne, Juni 15 – 21, 2021 toleo No. 507 kutokana na umuhimu wake. Hii ni bajeti ya kihistoria. Kwa muda mrefu tumekuwa tukisema tunataka bajeti ya kukuza viwanda, lakini hili limekuwa halitokei.

Bajeti ya mwaka huu imefungua mlango wa kutengeneza vifungashio, magunia, mazao ya kilimo, viwanda vya pikipiki, mabati na chochote kiwacho kutokana na kodi nyingi kufutwa. 

Naomba msomaji ujipe muda uisome bajeti hii. Gazeti letu JAMHURI ni la wiki, hivyo hata kama hautamaliza kuisoma ndani ya saa 2 unaweza kuihifadhi baadaye ukipata muda umalizie. Ni muhimu uone mabadiliko makubwa yaliyowasilishwa.

Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema: “Kodi ya simu za mkononi haiepukiki.” Nafahamu yapo maeneo matatu ndiyo yanajadiliwa kwa kina katika bajeti ya mwaka huu. 

Maeneo haya ni kodi ya Sh 1,000 kwa mita ya umeme kwa nyumba za kawaida na Sh 5,000 kwa nyumba ya ghorofa na zile za biashara. Mimi naona hii imeondoa kero. Ni mfumo unaoondoa hatari ya kuuza nyumba za watu. 

Kama haukununua umeme hautadaiwa kodi hii na nyumba yako itabaki salama. Naamini kila Mtanzania ana hamu ya kuishi maisha bora, ambapo umeme ni kichocheo cha maisha bora. Na hakika, kodi hii inalipika. Siasa laini za kudhani mtu atapata huruma ya wapangaji nilizoanza kuziona, tuzipuuze.

Nimeona malalamiko ya watu kadhaa kwenye mitandao, hasa katika eneo la gharama za miamala ya simu ambayo inaanzia Sh 10 hadi 10,000 na kodi ya simu za mkononi ambayo ni kati ya Sh 10 hadi 200 kwa siku. 

Pia kuna tozo ya Sh 100 kwa kila lita ya mafuta inaanzishwa. Kodi hizi tatu zimeleta kilio kikubwa mno kwa wananchi.

Sitanii, naziona kodi hizi mpya zikileta wastani wa Sh trilioni 3 kwa mwaka hapa nchini. Najua inauma ukisikia hii kodi mpya imeanzishwa. 

Lakini kuna jambo nataka niwaambie Watanzania, tunapaswa kufahamu kuwa nchi yetu haiwezi kuendelea kamwe kwa kutegemea misaada na mikopo. Misaada na mikopo ni sawa na kumwekea mgonjwa ‘drip’. Mgonjwa ataishi, ila ‘drip’ haiwezi kuwa mbadala wa chakula kamwe.

Leo wala sitatumia mifano ya ughaibuni. Mwaka 2006 nilifanya mahojiano na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Akaniambia: “Hakuna jinsi tunavyoweza kusambaza umeme bila watumiaji wa umeme kugharamia usambazaji. Ni lazima nitahakikisha serikali inaanzisha chombo cha kusimamia hili na tutaweka utaratibu wa kupata na kuzitumia fedha kutoka kwa watumiaji wa umeme.” Mwaka mmoja baadaye, yaani 2007 ikaanzishwa REA (Wakala wa Umeme Vijijini).

REA tunakatwa asilimia 3 ya gharama ya umeme unaonunuliwa. Fedha hizi tunazitumia kununua nguzo, vifaa kama nyaya na vingine. Leo kila kijiji kinasambaziwa umeme. Nguzo zimemwagwa vijijini pembezoni mwa barabara za miti na zege. Tumeweza kusambaza umeme kwa kutumia fedha zetu za ndani.

Sitanii, uamuzi huu wa kuanzisha kodi ya simu mahususi kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijijini ninauunga mkono asilimia 100. 

Hata kodi ya Sh 100 kwa kila lita ya mafuta nayo naiunga mkono asilimia 100. Kama tulivyojenga mfumo wa umeme kupitia asilimia 3 ya ununuzi wa umeme wa REA, naiona kodi hii mpya ya simu ikijenga barabara za nchi hii.

Nawahakikishia sisi Watanzania tunapaswa kusimama kwa miguu yetu. Tukitegemea mikopo, misaada na wafadhili, ukiacha kuwa haiji kwa wakati, kuna mikopo inakuja na masharti. 

Wapo wenye hamu ya kutwambia turasimishe ushoga ndipo watupatie mikopo. Binafsi ninasema hapana. Tuepuke kutaka kula vya watu, tutaliwa!

Mwisho, ninalo jambo la mikopo ya elimu ya juu. Niseme kwa ufupi tu kuwa tunahitaji kuanzisha kodi ya huduma ya asilimia 2 kwa kila huduma inayotolewa na hii iende moja kwa moja kwenye elimu. China walianzisha kodi ya elimu asilimia mbili kwa kila huduma inayotolewa mwaka 1980. Leo wanatoa misaada ya kusomesha watoto wa nchi za kigeni, ikiwamo Tanzania kutokana na kukusanya fedha nyingi. Naamini tukiamua tunaliweza hili na tutasomesha kila mtoto wa Tanzania bila kuwapa mikopo.

Tukianzisha hiyo, tutafuta utaratibu wa kuwapa wanafunzi fedha mkononi. Wanafunzi kazi yao ibaki kuwa ni kusoma, kula, kuoga na kulala. Tutapunguza kasi ya watoto wetu kwenda kwenye majumba ya starehe, watapata fursa ya kuishika elimu isiwaponyoke. Vyuo vitakuwa na mabwalo ya kulia chakula, ila tutaweka viwango kuepuka maharage yaliyobunguliwa.

Kwa mfumo wa sasa wa kuwapa fedha mkononi wanafunzi wetu kwa njia ya mkopo, si tu tunawaharibu kwa kuwanyima fursa ya kusoma wakaenda kwenye starehe kwa sababu wana fedha, bali pia wakihitimu hatuna uhakika wataajiriwa wapi, hivyo mkopo wa sasa kulipika kwake ni shaka tupu. 

Zimejengwa baa nyingi na nyumba za starehe karibu na vyuo usipime. Leo ukienda kwenye kumbi, kama Dodoma utasikia ma-DJ wanasema: “UDOM piga keleleeeeee,” kisha wanaitikia: “Yooooooooo…” Ma-DJ wanaendelea: “CBE mpooooo?” Wanaitikia: “Yoooooooo”.

Nasema hapana. Muda wa wanafunzi wetu kuwa maktaba wanakuwa kwenye kumbi za starehe. Muda wa kulala, wapo kwenye madangulo. Vyumbani wanashindania simu bora, redio na televisheni. 

Ukiingia mabwenini utafikiri umeingia kwenye shamba la wanyama (Animal Farm). Aliyewasha redio haya, wa TV sawa… hakuna utulivu mabwenini siku hizi sawa na ilivyokuwa enzi zetu tuliosoma miaka ya 1980 na 1990. 

Watoto wetu kwa kuwapa fedha mkononi kama mkopo tumewaweka katika mazingira hatarishi, halafu tunasema elimu imeshuka!

Nahitimisha safu yangu kwa angalizo. Tunao Mfuko wa Barabara (Road Fund). Unapokea mabilioni kutoka kwenye kila lita ya mafuta. Je, mfuko huu huwa unakaguliwa? Hakuna panya wanaouguguna? 

Je, tumejiandaa kuziba matundu kama yapo yasihamie Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA)? Fedha hizi ni nyingi, ikiwa hazitasimamiwa vilivyo, tutawakatisha Watanzania tamaa ya kulipa kodi kwa uadilifu. 

Hongera Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukataa kodi za damu. Hongera Dk. Mwigulu Nchemba kwa kuanzisha vyanzo hivi vipya, ila Watanzania wanataka kuhakikishiwa usalama wa fedha hizi zikiisha kulipwa. Mungu ibariki Tanzania.

1377 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!