Jamani, maisha yanaendelea baada ya uchaguzi. Tanzania imekuwa nchi ya kuangaliwa na mataifa mengi duniani hasa kutokana na sifa kubwa ya kuwa kisiwa cha amani.

Tanzania inatazamwa na wenye dhamira mbaya ya kutaka tuingie katika machafuko ili waweze kuchota kilicho chetu.

Kwanza tupongezane kwa amani iliyopo nchini hata kama kuna makandokando ambayo huenda yakawa ni sehemu ya wawekezaji wa uvunjifu wa amani hapa kwetu, kilichonikera sana ni pale ninapoona majirani zetu wakishabikia uvunjifu wa amani nchini Tanzania.

Kiukweli sijaipenda kauli ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akisema anataka kuona mfano wa demokrasia kutoka katika uchaguzi huu. Nimthibitishie Tanzania ni yetu na itaendelea kuwa yetu na yeye hana hisa na amani yetu kwa sasa ajikite zaidi katika amani ya Rwanda na kuihifadhi katiba ya nchi yao.

Leo bado muda mfupi kutangazwa na kuapishwa kwa rais wa nchi yetu, mheshimiwa rais nakujua kwamba wewe ndiye utakayeapishwa, kuna ahadi nyingi nyuma ya urais wako, rais anayetoka madarakani amechoka sana kwa kazi kubwa aliyoifanya mpaka leo, sasa hivi kwa mujibu wa kauli yake, yupo tayari kukabidhi nchi muda wowote, hii ndiyo demokrasia ya kweli iliyopo Tanzania tu katika nchi hizi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa rais, kazi kubwa ya kuomba kura haikuwa rahisi, kuna sehemu ulipita watu wakakukejeli, wakakuzomea, wakakutafutia matusi katika mitandao ya kijamii na hata katika mabango, walihadaa vitendo vyako kama watani zako lakini mwisho wa siku sisi tumebaki kama Watanzania na Taifa la Tanzania lazima liwepo kwa gharama yoyote.

Sasa unaapa kuwatumikia Watanzania, jambo la msingi kabisa ninalokusudia kusema leo ni kwamba sahau matusi na kejeli zote kwa kuwa huo ndiyo mchezo wa siasa na stadi za ushindi kwa mpinzani wako, sahau hayo na kumbuka ahadi zaidi ambazo umewapa wapigakura wako.

Utakapokuwa unaapa kumbuka miradi yote ambayo ulisema utafanya kwa mujibu wa ilani yako ya uchaguzi, utakapokuwa unaapa kumbuka kuwa kuna watu walisema huwezi na wamekupa ili kukupima kama unaweza, kumbuka pia ni kishindo hichohicho utarudi nacho tena kwa wapiga kura baada ya miaka mitano.

Kama hakuna kitu ulichokamilisha, nakutahadharisha anza kufikiria jambo jipya la kufanya, hawa Watanzania wa sasa nadhani wamekunywa maji yote ya hasira dhidi ya kiongozi ambaye anawahadaa na kuwaona kama njia ya kuingilia Ikulu.

Watanzania wa leo waligeuka kuwa wanasiasa wazuri kuliko mliopanda majukwaani, Watanzania hawa wamenishangaza kwa mtindo wao wa kusema ‘liwalo na liwe’. Hili ni fundisho kwamba hata wewe unayeapa leo  baada ya miaka mitano watasema bora tulipigie kura jiwe lakini siyo wewe tena.

Watanzania wa leo wamegeuka kuwa wale wa miaka ya ubarobaro wetu ambao tulikuwa tunajua kuwa siasa ni kazi na siyo blabla za majukwaani, siasa ni kuwajibika kwa wananchi unaowaongoza, siasa ni mapatano yasiyo na shaka ya uongo, siasa ni ahadi za kweli, siasa si vita ni ushindani wa hoja zinazowezekanika.

Mheshimiwa rais, utakapoapishwa kumbuka kuna watu nyuma yako ambao wapo kwa ajili ya kukuangusha, wapo kwa ajili ya kutotekeleza wajibu wako, wapo wengi ambao hawako na wewe katika utekelezaji wa majukumu yako, wapo na bado watakuwapo tu kukushangilia wakikuona unaingia shimoni kwa kushindwa kutekeleza ahadi na sera zako, hao ni wengi, ishike katiba lakini kumbuka wapo nyuma yako.

Najua unaapa kwa moyo mkunjufu kabisa, lakini kumbuka urais ni taasisi ambayo wengi wao watafikiria matumbo zaidi na kuleta ukiritimba katika serikali yako, najua unajua lakini si vibaya nikakukumbusha kwamba pale uliposhangiliwa sana katika hotuba zako ndipo penye kero kubwa kwa wapiga kura hawa unaoapa mbele yao.

Mheshimiwa rais, nisingependa nikuchoshe kwa barua ndefu lakini naomba nikusihi kama Mtanzania mwingine yeyote, punguza jazba, acha kulipa kisasi, wote waliopiga kura wapo chini ya himaya yako, wewe ndiye rais wa nchi bila kujali nani alimpigia nani, anza kazi mara moja, miaka mitano siyo mingi katika kuonesha mbichi na mbivu.

Mheshimiwa rais, baada ya miaka mitano, Watanzania watataka kusikia nimefanya hiki na kile na siyo tutafanya tupeni muda, hawa Watanzania wa leo nadhani wamechoka wanataka mtu na siyo chama, ukiona kuna mtu anakukwamisha kichama anza kumtupa kabla hujatupwa.

Nikutakie kazi njema na hongera kwa kuwa rais wa awamu ya tano, kuongoza watu karibu milioni hamsini ni baraka hata mbele ya Mwenyezi Mungu.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri