Tumefunga mkataba wa mabadiliko

Juzi Jumapili Oktoba 25, mwaka huu, Watanzania tulifunga mkataba wa mabadiliko kati yetu (wapigakura) na wagombea uongozi nchini (madiwani, wabunge na rais) kutuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo; 2015-2020.

Mkataba huo muhimu unabeba dhana ya mabadiliko yenye kusudio la kujenga ‘Tanzania Mpya’ kwa maana ya kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta za uchumi, siasa na huduma za jamii na kutokomeza maadui ujinga, umaskini, maradhi na rushwa nchini.

Dhana hiyo ya mabadiliko imeleta mshawasha mkubwa kuanzia kwa vijana hadi kwa wazee baada ya kuchoshwa na rushwa, ufisadi na maisha yasiyo na afya huku wakiwaangalia baadhi ya Watanzania wenzao wachache wakitakata na kunawiri.

Watanzania tumeamua kuleta mabadiliko ya kweli. Ukweli huo unawezekana umepotoshwa au haukupotoshwa Jumapili iliyopita. Hivi sasa tunasubiri tu kuona kama kweli tumefanya mabadiliko ya dhati kupitia sanduku la kura ambako kila mtu alitumia haki yake kujiandalia maisha bora ya baadaye.

Iwapo hatukufanya uamuzi makini na wa busara, tusitarajie kupata hayo mabadiliko ya kweli. Hapo tutakuwa tumecheka na ngedere na mahindi kuliwa. Mabua ya mahindi hayatatusaidia kuoka mkate wala kujenga nyumba.

Tayari tangu juzi hadi leo, tunaporejea matokeo ya kura tulizopiga katika vituo mbalimbali nchini, huku tukisubiri kauli  thabiti na ya mwisho kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  kututangazia rasmi nani ni mshindi wa udiwani, ubunge na urais.

Inawezekana nafsi yako ima inakusuta kwa kuzima mabadiliko ya kweli na kuwasaliti Watanzania wenzio, au nafsi hiyo inafurahi kuona umefungua mlango wa mabadiliko na kuungana na Watanzania wenzio wenye huba na nchi yetu.

Kampeni zimepita, vijembe na kejeli zimetoweka na uchaguzi umefanyika. Kilichopo ni kupokea matokeo ya uamuzi wetu. Uamuzi wenye sura mbili; kushinda na kushindwa kwa mgombea na chama chake

Ukweli sura hizo zina asili ya malezi, elimu na vitendo vya chama cha siasa na mgombea mwenyewe kabla ya uchaguzi alijiwekaje mbele ya Watanzania kwa kauli na vitendo. Watanzania wanahitaji mtu mwadilifu na mwenye uwezo wa kuongoza.

Uamuzi wa Watanzania makini ni msumeno unaokata mbele na nyuma bila kujali unaokatwa ni mti wa mvule, mkongo au mpingo. Cha msingi mti unakatwa na kutoa vigogo au mbao ambazo ni muamala kwa mpasua mbao ambaye ni Mtanzania.

Kauli thabiti na vitendo mwanana vya mtu yeyote anayetaka kuwa kiongozi hunakishiwa na mapenzi, huba, nyonda na hukamilishwa na mahaba. Mahaba yanaposhamiri kiongozi huwa ni muhibu kwa watu anaowaongoza.

Mahaba hayo huwa yanachuja endapo mmoja kati ya hao wawili anapolea ulaghai, ufisadi hata uasherati. Na hapo pendo kama asali hukosekana. Hata kama mtu atajitahidi kutia sukari na maji ya zamzam kamwe pendo halitakuwa la mahaba.

Watanzania makini na wazalendo wana mahaba makubwa kwa mama yao, Tanzania kwa sababu ya mapenzi wayapatayo katika malezi ya kweli na salama. Hifadhi ya mali zao aina aina ardhini, majini na hewani. Hayo ndiyo mahaba kati ya Mtanzania na mama Tanzania.

Kwa hiyo, fadhila ya Watanzania kwa mama yao ni kumpatia kiranja mzalendo na muadilifu akisaidiwa na fumbi la mbele na fumbi la nyuma. Natarajia kuona viongozi tuliowachagua ni chaguo letu baada ya kupima uwezo na uadilifu wao.

Matokeo ya uchaguzi yasitufanye tufarakane, tushindwe kusalimiana, kuzikana na kuanzisha vita ya wenyewe kwa wenyewe! Majirani zetu watatushangaa na kutupuuza. Tukumbuke msemo wetu kuwa baada ya uchaguzi kuna maisha. Asanteni Watanzania.