Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, aliwahi kusema: “Asilimia 98 ya Watanzania hawaheshimu sheria.” Alinukuliwa na mojawapo ya vyombo vya habari.

Ukitafakari matamshi haya kwa haraka haraka unaweza kusema kuwa ni taarifa ambayo haishabihiani na hali halisi, lakini upo uwezekano kuwa aliyosema hayapishani sana na ukweli.

Sina hakika kama Kamanda Tibaigana alitamka hayo kutokana na utafiti aliyoufanya au aliyasema hayo kutokana na uzoefu wake kama afisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi. Lakini hata kama matamshi yake hayatokani na utafiti rasmi, tunaweza kuamini kuwa uzoefu wake wa kazi unampa sifa za kuweza kutabiri kwa karibu sana hali halisi inayohusisha Watanzania na utiifu wa sheria.

Lakini pamoja na kuzingatia uzoefu wake, au tuseme hasa kwa sababu ya uzoefu wake huo ni muhimu pia tuweke tahadhari kwenye kutafakari ujumbe mzito kama huu.

Mazingira ya kazi yake yanampa fursa ya kukutana na wahalifu kila wakati na hiyo peke yake inampa jicho la kuona kuwa karibu kila mtu ni mtuhumiwa. Hata hivyo, kamanda wa polisi hafanyi kazi kwa saa 24 kila siku na bila shaka hujikuta kwenye mazingira mengine ambayo yanamruhusu kutathmini jamii anayoishi nayo nje ya mazingira ya kazi yake.

Kutoheshimu sheria kunajitokeza kwa aina nyingi. Vipo vitendo ambavyo mtu akifanya au kutofanya vinaweza kusababisha yeye kupatikana na kosa la jinai au ambalo si la jinai.

Bila shaka ni sehemu ndogo ya watu katika nchi ambao hukutwa na makosa ya jinai, lakini tukijumlisha makosa ambayo si ya jinai basi ni wengi tutaingizwa kwenye kundi la wasioheshimu sheria.

Kwa mfano, ni vigumu kwa dereva wa gari kuwapo barabarani kwa miaka mingi bila kukiuka kwa makusudi mojawapo ya sheria za usalama barabarani. Miaka ya hivi karibuni mapolisi wa usalama barabarani wamevalia njuga madereva ambao wanaendesha kwa mwendo unaozidi ule ulioruhusiwa kwenye sehemu ya barabara.

Kinachofanyika kwa madereva wengi ni kuwa anapokaribia sehemu ambayo anafahamu wapo polisi wanaopima kasi ya mwendo, atapunguza mwendo na mara atakapowapita mapolisi atarudia kuendesha kwa kasi ambayo yeye ataichagua.

Upo utafiti ambao hupima hali ya uhalifu kwenye nchi mbalimbali duniani. Matokeo ya baadhi ya utafiti yanabainisha kuwa hali si mbaya kama Kamanda Tibaigana alivyotamka, lakini si nzuri.

Mojawapo ya utafiti ambao hutokana na majibu ya maswali ya watu wa nchi mbalimbali ambao hushirikishwa kwa njia za mtandao ili kupata maoni yao juu ya hali ya uhalifu kwenye nchi zao umefanywa na tovuti inayojulikana kama Numbeo.

Matokeo yanabainisha kuwa Tanzania, katika kipimo cha 0 hadi 100 (100 ikiwa ndiyo kiwango cha juu kabisa cha uhalifu kinachoonekana kwa wale waliojibu maswali ya utafiti) ina kiwango cha uhalifu wa zaidi ya 61. Kwa vigezo vya utafiti, kati ya 60 na 80 ni kiwango cha juu cha uhalifu. Bado haifikii kiwango cha Kamanda Mstaafu Tibaigana, lakini inashabihiana na matamshi yake.

Zipo sababu kadhaa zinazoweza kuathiri usahihi wa matokeo ya utafiti kama huu. Ukizingatia kuwa taarifa zinazotumika kufanya utafiti zinategemea ukamilifu wa taarifa ambazo wanazo wanaojibu maswali, basi ni dhahiri kuwa hali halisi ya uhalifu inaweza kuwa kubwa kuliko inayopatikana kwenye utafiti.

Vyombo vya habari hutoa taarifa za uhalifu ambazo hupatikana kutoka Jeshi la Polisi, lakini yapo matukio mengi ya uvunjifu wa sheria ambayo polisi hawayafahamu, au ambayo hayajaripotiwi polisi. Kwa hiyo ufahamu wangu wa hali halisi ya uhalifu itaakisi taarifa zile tu ambazo polisi wanazo na ambazo wametoa kwa vyombo vya habari, na matukio yale ambayo mimi mwenyewe nitayashuhudia.

Ukiongeza wale ambao huamua kuadhibu watuhumiwa wa wizi bila kuwafikisha polisi na ambao mara nyingi hawafikishwi kwenye vyombo vya sheria au kwa kukosa ushahidi au kwa sababu nyingine, utaona yanajitokeza matukio mengi ambayo hayawezi kubainika kwenye matokeo ya utafiti.

Aidha, kwenye nchi ambazo Jeshi la Polisi lina uwezo mdogo wa kubaini uhalifu, nchi hizo zitaonekana kuwa na uhalifu wa hali ya chini kuliko hali halisi ilivyo wakati ukweli unaweza kuwa kwamba matukio mengi ya uhalifu hayabainiki. Hali hii inaweza kusababishwa na ukosefu wa mafunzo mazuri au vitendea kazi kwa polisi.

Kwa hiyo kutokana na hizi sababu zilizotajwa na ambazo zitasababisha kutofahamika kwa matukio mengi ya uvunjifu wa sheria, hali halisi ya uhalifu nchini inaweza kuwa iko juu na inakaribiana na ile iliyotajwa na Kamanda Tibaigana.

Wapo wabeuzi wanaosema kuwa sheria zipo ili zivunjwe, na kwao inaweza kuwa jambo rahisi kutoheshimu sheria. Wapo watu wanaosema kuwa ni vigumu kuishi kwa kuheshimu sheria wakati wote labda kutokana na ukweli kuwa hujikuta, mara kwa mara, wamefanya kosa moja au jingine la kisheria. Wapo wanasiasa wanaosema kuwa zipo sheria ambazo hazifai kuwapo, na wakati mwingine huhimiza wafuasi wao kuzipuuza.

Kwa ujumla, hali ya kutoheshimu sheria ipo na itaendelea kuwapo. Kinachoweza kupunguza hali hiyo ni kukua kwa kizazi kipya cha watu wanaoona umuhimu wa kuheshimu sheria. Lakini hali hii pia ni vigumu kufikiwa.

Watoto wanajifunza kwa wazazi. Sasa iwapo karibia sisi watu wazima wote tunayo hulka ya kuwa vibaka, wezi, matapeli, mafisadi, majambazi, wauaji, wabakaji, na washiriki wa kila aina ya uhalifu, tutawezaje kufundisha watoto wetu umuhimu wa kuheshimu sheria?

1425 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!