Nilikuwa nasikia kutoka kwa watu kwamba bajeti ni vilio kila kona, sikuelewa, kwa sababu bajeti si msiba ama majanga lakini nilipoipata baada ya hiyo digitali kunifikia, nimeona huo msiba ni wa aina gani.

Nakumbuka bajeti yetu ya kwanza tukiwa Tanganyika ilikuwa ikisemwa milioni kadhaa na bajeti hiyo ndiyo iliyokuwa ya kuijenga Tanganyika iliyokuwa huru punde ili ifikishe taifa letu katika maendeleo. Bajeti ile haikupata kuzungumzia vileo ama mafuta, isipokuwa nakumbuka ilitaja ongezeko la shilingi mbili kwa chumba cha hoteli yoyote iliyosajiliwa.

 

Bajeti yoyote ya nchi inapotayarishwa, kusudio lake kubwa ni kukusanya mapato kwa ajili ya kuweza kuiendesha serikali katika kuwahudumia wananchi, na inatakiwa kulenga vyanzo ambavyo havitetereki kwa mwaka mzima ili ama kufikia, au kuvuka malengo.

 

Bajeti yetu siku zote inajikita katika vyanzo ambavyo naweza nikaamini kwamba havijawahi kutetereka na ndiyo maana kuna wakati tunafikia malengo kwa msaada wa mikopo na wafadhili kuijalizia pale tunapokwama, lakini pia bajeti hukaa vizuri inapotokea wakapatikana watumishi au wafanyabiashara wanaokubali kukopwa huduma zao na kupelekwa mwaka mwingine wa fedha.

 

Huu ni utaratibu wa nchi mbalimbali duniani lakini katika nchi nyingine suala la kodi lina mtazamo tofauti, ili kukidhi mahitaji ya bajeti yao na kuwa na akiba zaidi ya bajeti waliyojipangia waweze kusaidia nchi zinazoshindwa kufikia malengo ya kukusanya kodi kwa kukosa vyanzo madhubuti vya kodi.

 

Nawashukuru waandaaji wa bajeti yetu lakini naomba nitoe mawazo yangu kwa kusema suala la kuangalia vyanzo vya mapato liwe kama ilivyokuwa katika mchakato wa katiba, wananchi wapate fursa ya kutoa mawazo yao sehemu gani zilengwe zaidi katika kukusanya kodi za serikali.

 

Nimepata kukutana na watu kadhaa kutoka ughaibuni ambako mtu hutambua umuhimu wa kulipa kodi kiasi kwamba anapofanya biashara yoyote hulazimisha taasisi inayokusanya kodi kupokea sehemu ya pato lake kama malipo ya kodi. Hii niliona ni tofauti na hapa kwetu ambako walipakodi ni wale tu ambao sehemu ya malipo yao ina mkono wa serikali. Kwa lugha nyepesi ni wale wanaofanya biashara na serikali, na waajiriwa hawa wa serikali hawana njia ya kukwepa kulipa kodi.

 

Kodi hii iliyopigiwa makofi mengi sana na waheshimiwa wabunge wetu bila kujua kutoka chama gani, inakasoro nyingi zinazojirudia kila wakati, imekuwa kama dozi ya ugonjwa kwa maana ya mgonjwa kuongezewa idadi ya vidonge kila mwaka, imejikita katika makusanyo yaleyale – vileo na mafuta.  Maeneo kama ya madini na utalii hayajaguswa ipasavyo, maeneo haya yangeweza kuguswa  kwa manufaa ya mwananchi huyu anayetegemea mlo mmoja kwa siku na kuacha kugusa mafuta ambayo ndiyo msumari wa kila kitu.

 

Misamaha ya kodi katika madini na uwekezaji inafanya bajeti yetu iwe tegemezi kwa wahisani kila siku, kwa kufanya hivyo maisha ya akina sisi yanazidi kuwa nafuu ya jana, tunasikia jinsi ambavyo kila sekta ambayo inaachwa au kupewa msamaha wa kodi inavyopoteza mabilioni ya shilingi halali ya kodi kwa serikali yetu, lakini pamoja na kusikia huko tunashindwa kuandaa utaratibu wa kukusanya kwa kisingizio ambacho hata wenye nchi hatuelezwi, hivyo tunakuwa na kigugumizi cha kujua kulikoni kwa viongozi wetu tuliowapa dhamana ya kuisimamia serikali yetu.

 

Hainiingii akilini kuacha kukusanya kodi katika bodaboda na matoyo kwa kisingizio cha kuwawezesha wananchi. Hivi aliyewaambia kwamba walalahoi wanamiliki hayo matoyo ni nani? Kwa kuwasaidia ni kwamba hizo ni mali za mafisadi, kuna matajiri wanaomiliki bodaboda zaidi ya 100, kwa hiyo waliosamehewa kodi si walalahoi ni matajiri wenzenu.

 

Kuendelea kutegemea kodi kutoka katika pombe na sigara kuna mwisho, kwani kutokana na ukali wa maisha yaliyopo sasa hivi wengi wetu tunamrudia Mungu na kuokoka, nani atakunywa pombe na kuvuta sigara na, je, mapato ya serikali yatatoka wapi ama tutawaeleza wafadhili wetu wajazie pale ambapo hapajajazwa na walevi?

 

Nilitarajia kwa Sera ya Kilimo Kwanza kutoa kodi  na kutia ruzuku katika zana za kilimo na kutoa mikopo kwa vijana wanaofanya biashara za kubangaiza, ili kuwahamasisha wakalime mazao ya chakula na biashara kuiwezesha serikali kupata mapato kiurahisi na si kuziachia kampuni kubwa za wawekezaji misamaha ya kodi, ambazo si za wazawa, ziweze kuchuma vizuri “shamba la bibi.”

 

Inanitia uchungu mimi binafsi ambaye naikumbuka bajeti yetu ya Tanganyika, iliyokuwa haina kodi ya madini kwa kuwa tulikuwa hatuyachimbi na bado tuliweza kukusanya kodi hadi katika baiskeli na kichwa na kuweza kutoa huduma za afya, elimu, maji na nishati bila wasiwasi.

 

Naomba kurudia kushauri kama wasomi wetu mmefikia ukomo wa kujua vyanzo vya mapato, basi uwe mchakato wa kukusanya maoni kama ilivyo katiba ili nasi tushiriki kuisaidia serikali kupata mapato.

 

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

1048 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!