Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai hadi leo. Kwangu mimi ni faida kubwa sana kuongeza kila siku moja katika maisha yangu. Nayaona mengi na bado mapya kabisa katika maisha yangu, kiufupi kila uchao unakuchwa na jambo jipya ambalo nimejifunza katika maisha yangu.

Duniani tunapaswa kujifunza kila siku, na mafunzo siku zote ni lazima tukubali kujifunza jambo jema au jambo baya, katika mafunzo tunayopitia ni lazima kujifunza namna ya kukwepa mambo mabaya na namna ya kutumia mambo mema katika kuhitimisha ngwe yetu ya maisha ili siku moja katika kumbukizi waweze kusema fulani aliwahi kusema hivi au kufanya hivi. 

Leo nimeamka nikiwa na fikra tofauti kabisa na nimejiuliza kuhusu nafasi ya maisha haya baada ya miaka kadhaa huko mbele mimi nikiwa katika kiti cha hukumu, nimejiuliza maswali ambayo labda ni kwa sababu ya uzuzu wangu ndiyo maana najifikiria bila sababu, nimefikiria tofauti ya maisha yetu na maisha haya, taifa letu na mataifa yale. 

Nimeamka nikiwaza mambo mengi juu ya matukio mbalimbali yanayoitwa ya kisasa na hasa yanayoibuliwa na vijana wa kisasa, kwa kuwa yananiumiza sana na kuifanya akili yangu iwe inabadilika siku hadi siku, kichwa kinaniuma na sijui hatima yake itakuwaje. 

 

Busara kwa kijana ni jambo ambalo huwa halionekani, unaweza ukamuona kijana mwenye hekima na hali kadhalika mtu mzima mwenye hekima, lakini busara huwa ni kama kipawa ambacho hutokana na kuabudu na kuwa na hofu ya Mungu, sasa hivi inaonekana vijana wetu wametekwa na wimbi la shetani na kukosa vijana wenye kipawa hicho, ni suala la kumuomba sana Mola. 

Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya ajabu ambayo enzi zetu yalikuwa ni nadra sana kuyaona, si kwamba kulikuwa hakuna vijana, la hasha, walikuwepo na walikuwa na maadili ambayo nadhani yaliwafanya wakaheshimu baadhi ya mambo ambayo leo yametamalaki kutokana na usasa.

Kwa mfano, umalaya na ukahaba unaofanywa kwa uwazi wa ajabu na hasa kwa vijana, unataka kutuonyesha nini kwa dunia ambayo itakuja kesho yetu? Hiki kizazi ambacho tunakifundisha kwa kufanya umalaya hadharani tunataka wao waje wafanye vipi? Inawezekana ni ugumu wa maisha, lakini siamini kama hilo ndilo suluhisho, na sitaki kurejea maandiko yanasema nini juu ya umalaya na ukahaba huu.

 

Tumekuwa na tabia ya uongo ulioota mizizi na tunaufanya hadharani bila kuona haya, sina hakika kama ndio usasa au maendeleo, ninapata shida sana kwenda na kasi hiyo na kuibadilisha akili yangu kukubaliana na uongo katika kila kona, iwe miadi, mapenzi, fedha na kila kitu kinachohusishwa na shetani kubebwa kwa uongo. 

Zamani na enzi za busara za vijana na wazee ilikuwa hauwezi kuona picha za vifo, watu waliheshimu maiti na kuzihifadhi kwa heshima yake, ilikuwa ni busara tu ambayo ilikuwa ikitumika, inawezekana ilikuwa ni uzamani, lakini tujiulize, huu usasa wa kuanika picha za maiti hadharani katika mitandao ya jamii ni busara gani mpya ambayo tunajifunza na tunataka tuiache kama amana kwa kizazi kijacho? 

Kuna picha nyingi za ngono ambazo zinatembezwa katika mitandao ya kijamii na simu, pia kuuzwa katika santuri na jamii hii imekubali kupokea kama jambo muhimu sana, sina hakika kama kuna chembe ya busara inayotumika, tukiombee kizazi hiki na sisi tuombe akili zetu zisikubali kupokea mambo ya mapokeo. 

 

Maendeleo huja na matukio ya kipumbavu, wapo ambao wanadhani wanaweza kupata fedha kutoka kwa mtu mwingine bila kufanya kazi, jambo pekee walilobaki nalo ni utekaji wa watoto na watu wazima ili waweze kujinufaisha na malipo hayo, mipango yote hii naamini kwamba ipo kwa vijana ambao hawana busara, njia pekee ni vijana kuwa na chembe ya busara kuwashauri vijana wenzao ambao tayari wamekwisha kupotea katika ulimwengu wa imani.

Yapo mengi sana; kuna ubakaji, kutoa taarifa za uongo, kushitua jamii na kadhalika, lakini pia kuna utangazaji na uandishi wa ‘online’ ambao umekuwa na upotoshaji mkubwa, naamini kama kundi la vijana wakiamua kubadilika na kuwa na busara, mambo haya hatutayabariki na kuwa laana kwa vizazi vinne kutoka kwetu. Inakera sana na nina imani kuna vijana wana vipawa vya  busara, ninaomba wawasaidie wajinga wachache waliomo katika jamii yetu. 

 

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo. 

By Jamhuri