Yah: Dhana ya kujifunza kujiuzulu

Sina hakika kama ningekuwa kiongozi katika maisha yangu iwapo ningeweza kukaa madarakani kwa muda mrefu. Sababu kubwa ni kwamba ninajua maana ya kuwajibika pale ambapo nimekosea au ninayemsimamia amekosea.

Kuna hadithi ndefu mgongoni kwangu ya uwajibikaji katika madaraka ambayo nimepata kuyapitia. Haina maana sana, lakini ni muhimu kuwajulisha wenye dhamana kwamba kuwajibika hakutokani na makosa uliyofanya moja kwa moja, bali labda yaliyofanywa na uliowasimamia kwa kujua au kutokujua.

Nilipokuwa darasa la nne miaka ile, nilipewa dhamana ya kuwa time keeper (mtunza muda) wa shule. Nilikabidhiwa saa ndogo ya mezani na kengele mbele ya shule nzima. Ilikuwa dhamana kubwa sana kwangu, nikijihisi ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuanzisha siku na kuifunga, achilia mbali mgawanyo wa siku katika vipindi na mapumziko.

Baada ya miezi kama sita hivi, na hasa baada ya kuzoea kazi, kuna vijana kadhaa wanafunzi wenzangu waliamua kucheza mpira darasani na matokeo yake ni kuangusha saa ya shule, ikapasuka kioo. Japo ilikuwa bado inafanya kazi vizuri, nilikwenda haraka kwa mwalimu mkuu kutoa taarifa ya uharibifu ule na palepale kumuomba mwalimu anipe adhabu atakayoona inafaa lakini nikiwa nimekwisha kuacha wadhifa wa kuwa time keeper.

Ilipigwa kengele na wanafunzi wakatoka madarasani nikapandishwa kizimbani ili niwataje waliocheza mpira na kuvunja saa ya shule. Niliwataja nikajumuishwa nao kwenye adhabu ya pamoja kuchapwa viboko. Baada ya adhabu nikaitwa peke yangu, tena mbele ya shule nzima kuelezwa makosa yangu na jinsi nilivyotoa taarifa kwa wakati hata kama kosa halikuwa langu, nikaadhibiwa tena.

Siku iliyofuata gari la serikali lilifika shuleni ghafla, ninakumbuka lilikuwa ni Bedford jipya, rangi ya kijani, lililokuwa limeandikwa mlangoni Wizara ya Elimu. Wakati huo mimi sikuwa mtunza muda tena, niliumia sana nilipoona mwenzangu ndiye anapiga kengele kwa mara ya kwanza tangu uteuzi wake ulipofanywa jana yake.

Tulitoka nje wanafunzi wote huku tukimwangalia time keeper atupe japo fununu kuna nini. Ndipo nilipogundua kuwa nimetoka katika mfumo rasmi wa taarifa nyeti ambazo wakati huo alikuwa nazo mwenzangu. 

Kulikuwa hakuna mwalimu yeyote mbele yetu na wala mgeni, mara ghafla mkuu wa shule na ugeni wakajitokeza. Alikuwa ni Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kilwa aliyetuletea madaftari, rula, vitabu na chaki. Kamwe siwezi kuisahau siku hiyo.

Tulipewa taarifa ya kupokea na kutakiwa kuanza kuvishusha vifaa hivyo mara moja kutoka katika gari na kuhifadhi katika bohari yetu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa shule yetu kuletewa vifaa vile na lilikuwa jambo la furaha sana. 

Kabla Ofisa Elimu wa Wilaya hajaondoka ulifanywa uteuzi wa mtunza bohari kubwa ya vitabu vyote kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba, madaftari ya shule nzima na maboksi mengi ya chaki za rangi anuai pamoja na rula nyingi sana.

Zilielezwa sifa za mtunza stoo; lazima awe mwadilifu, mkweli na asiyeweza kuficha siri ya uhalifu, awe mchapakazi na mwenye weledi wa kile anachokifanya, asiwe na kiburi na awe mnyenyekevu kwa wenzake, mwisho lakini si kwa umuhimu, awe na sifa ya kutokuwa na tamaa na mali za shule na mwenye kutoa taarifa kwa walimu mapema iwezekanavyo.

Baada ya maelezo hayo tukasubiri jina kwa dakika kama tano hivi, kisha mwalimu mkuu akataja jina langu, shule nzima iliripuka kwa shangwe na Ofisa Elimu alitaka anione. 

Nikapandishwa katika kizimba kilekile cha jana, kisha kukabidhiwa ufunguo. Siku hiyo sikupata usingizi kwa furaha ya kuaminiwa tena, na kesho yake nikagundua kuwa kumbe hata walimu wengine wanapaswa kuomba vifaa vyao kwangu. Nilijiona mwenye bahati lakini nilijiapiza iwapo kosa litafanyika, nitaomba nipewe adhabu na kujiuzulu wadhifa ule.

Mpaka ninamaliza shule sikupata kuwa na nongwa na bohari yetu, nilikuwa nimejifunza mengi kutoka katika saa ya shule.

Waraka wangu wa leo ni kuwakumbusha wenye kung’ang’ania madaraka hata pale ambapo wanajua kabisa wamekosea. Kung’atuka au kujiuzulu hakuna uhusiano na kushindwa kuongoza bali ni kuonyesha ukomavu katika uongozi. 

Historia inaniambia wote waliojiuzulu walipata kuteuliwa katika nyadhifa zingine na cheo ni dhamana tu, hakina urithi au mwenye nacho.

Tujifunze kujiuzulu kwa uzembe wa walio chini yetu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.