Lugola amevuna alichopanda, asimlaumu mtu

Wakati Rais Dk. John Magufuli anatangaza kumtumbua Kangi Lugola kutoka kwenye uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisisitiza sana neno unafiki. Kwamba yeye si mnafiki. 

Akasema kwamba Lugola ni mwanafunzi wake na rafiki yake, lakini alichokifanya kwenye kazi ya umma hakikufaa, akamtumbua kwa kuyajali zaidi masilahi ya umma akiwa ameyaweka pembeni masuala mengine yaliyobaki. Hakutaka kuwa mnafiki.

Nataka hapa tulitazame hilo la unafiki aliousema rais. Unafiki ni tabia chafu sana inayosemwa hata kwenye vitabu vitakatifu. Unafiki ndio uliomponza Samson aliyekuwa na nguvu za ajabu akaishia kukamatwa kama kuku aliyeugua mdondo na kuangamizwa. Samson angeweza kuukwepa unafiki pengine angeendelea kusumbua kwa nguvu zake.

Kwa hiyo rais kujitenga na unafiki ni kitu bora sana. Tulimzoea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na mpaka sasa mifano mingi tunaitolea kwake. Mwalimu alikuwa mtu muadilifu sana na mkali kupindukia kwenye masuala ya kazi, hakutaka masihala kwa upande huo.

Ila alipochukizwa na kitu tulizoea kuona anabadilisha tu safu ya wasaidizi wake bila kuwaeleza wananchi ni kipi kimemuudhi, hakuwa na mazoea ya kutaja kosa la mtu. Huo ndio uliokuwa mtindo wa Mwalimu.

Hata mzee Edwin Mtei, rafiki yake wa karibu sana, alilieleza hilo kwenye kitabu cha maisha yake ‘From Goatherd to Governor’, jinsi alivyopeleka mgeni kutoka Benki ya Dunia kwenda nyumbani kwa Mwalimu Msasani. Anasema Mwalimu alichokifanya ni kuwaacha Mtei na mgeni wake sebuleni na kwenda zake kwenye bustani kusoma kitabu!

Eti Mtei alipomfuata Mwalimu aliishia kuambiwa na mzee huyo wa Kizanaki kwamba yeye ni kiongozi wa nchi na kamwe hawezi kuongoza nchi yake kwa maelekezo ya Washington. Kilichofuatia ni mzee Mtei kwenda ofisini kuandika barua ya kujiuzulu!

Lakini Rais Magufuli analiweka wazi kosa la mtu ili kila mwananchi alipime kosa husika na kuona kama kuna aina yoyote ya uonevu. Magufuli ni muwazi katika hilo, hataki unafiki.

Bahati mbaya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekumbwa na unafiki mkubwa.

Watu wanataka kujionyesha ni wazuri na wazalendo, kumbe wengi wao wanauma wakipuliza mithiri ya panya. Ukimuondoa mzee Mwinyi, aliyeng’atuka mwenyewe kwa kukiona kilichotokea chini yake kuwa kilikuwa hakifai ijapokuwa hakukishiriki, nafasi hiyo ikafuatia kukaliwa na watu wanaoonekana kuwa na tabia za kinafiki.

Kwa mfano, kuvaa Bendera ya Taifa kwa kutaka kuwaadaa wananchi kuwa wenyewe wana uchungu na taifa lao au kwamba wanalipenda sana, lakini wakiishia kufanya madudu ya hatari kwa nchi.

Lugola ni mtu wa pili mwenye tabia hiyo kukalia wizara hiyo katika kipindi kisichozidi miaka mitatu. Wa kwanza alikuwa Mwigulu Nchemba, akivaa skafu za bendera ya taifa kwa lengo la kuwapotosha wananchi wamuone kama mzalendo mkereketwa wakati kumbe ndani ya moyo wake hamna kitu! Huo ni unafiki.

Kwa mambo kama alivyoyaeleza rais kuhusu kosa la Lugola, kuna uzalendo wowote unaojionyesha hapo? Kuna mtu anayeweza kusema kwamba rais amefanya vibaya kumtumbua Lugola kwa aliyoyafanya kwa nchi eti kwa vile alikuwa anavaa mashati yenye bendera ya taifa?

Anafanya mpango wa kupoteza fedha nyingi yeye peke yake na rais amuache? Kisa anavaa bendera ya taifa! Hongera Magufuli kwa kujipambanua na unafiki.

Alianza Kitwanga na kutaka kuugeuza uwaziri mali binafsi ya Magufuli na kutumia ukaribu wake kwa rais kufanya mambo ya ajabu ya kuligeuza Bunge klabu cha pombe! Magufuli kwa kutaka kujitenga na unafiki akasema hapana ndugu yangu, hapo hapakufai, wapishe wengine.

Nadhani kwa kufanya hivyo ametumia kauli ya Baba wa Taifa aliyesema ukipewa kazi ya nchi ni lazima ujiheshimu, kwamba ukitaka kufanya uhuni barabara ziko nyingi, kafanyie uhuni wako kule. Narudia kumpongeza Rais Magufuli kwa kuliona hilo.

Magufuli angekuwa mtu mnafiki mambo yangeishia ndani kwa ndani bila kujua kilichoendelea, fedha Sh trilioni moja zingepotea bila kujulikana zilikopotelea! Wakati tunasumbuka na fedha za kufanyia mambo mbalimbali kumbe Lugola na wenzake wamekwisha kuweka mfukoni fedha zote hizo!

Tena eti wamefunga na mikataba minene ya kwamba hata ikitokea mkataba ukashtukiwa kilichoanza kufanyika lazima kiendelee mpaka kwisha! Kumbe walijua kuwa kuna uwezekano wa kutenguliwa mkataba husika, hivyo wakaamua waufunge kwa nyenzo ngumu kwelikweli!

Hivi kweli tusiyaangalie hayo tubaki kuangalia tu alama za bendera ya taifa kwenye mashati!

Watu wameyasema mengi, lakini na mimi naona ni bora niongeze ya kwangu. Kumuondoa tu Lugola kwenye uwaziri bado hakutoshi, ni lazima aeleze fedha zote hizo zimefanya kitu gani ili ikiwezekana tofauti iliyobakia irudishwe Hazina. Kwa sababu hata kama ni fedha za mkopo wanaozilipa ni Watanzania, walipe wanachokielewa kuliko kulipa hewa.

[email protected]

0654031701