Kwanza nianze kwa kupongeza juhudi kubwa inayofanywa na viongozi wachache wenye moyo wa uzalendo na Taifa hili, pili niwapongeze Watanzania wengi ambao mnaunga mkono juhudi hizo pasi na kununuliwa na watu wachache, ambao wao walidhani nchi hii ni yao na kwamba walio nje ya mrija wa pesa ni wadandiaji katika nchi yao.

Watanzania wachache ni mambumbumbu na makada wa mafisadi katika kuundeleza juhudi za wachache ambao wangelipenda maisha yaendelee kuwa yaleyale ya kuliwa Pato la Taifa, kwa ukiritimba wa kujiwekea mazingira mazuri ya kuvuna bila jasho, na wengine wakiishi kwa mlo mmoja na kuwasindikiza katika maisha bora wanayoishi wao.

Bado wapo Watanzania ambao hawajaamka na kukubali mabadiliko ya kisiasa ambayo yanageuza tabaka la wahujumu uchumi na waliohodhi madaraka kuwa mali yao kuhojiwa, wapo ambao walizoea maisha ya upambe kwa wale wenye uchu ya mali na wao kujiona ni maskini jeuri kwa fedha ndogo wanayolipwa kwa kazi ya kutetea dhambi ya wizi, tunawajua.

Bado kuna dhana zilizojengeka kwa baadhi ya Watanzania wakiamini katika kupinga kila kitu hata kilicho chema kwa faida ya wengi ili waonekane nao wanatoa mchango wa mawazo, lakini ukweli wanaujua wao na roho zao kuwa ni unafiki na uzandiki kwa kile wanachokifanya.

Sitaki kuamini kama baadhi ya wanaopinga yote yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano wana dhamira ya kweli katika kuliletea maendeleo Taifa letu, wapo wasomi uchwara wanaotoa hoja zao kana kwamba hawakupata fursa ya kuongeza maarifa ya uchambuzi wa mambo ya kitaifa na mfumo wa uendeshaji kiuchumi.

Napata taabu kidogo pale ninapobaini msomi anashindwa kutofautisha kati ya hasi na chanya, na ndipo ninapotaka kujua nafasi ya uteuzi inaangalia idadi ya vyeti au uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo. Niliwahi kuandika hapa kwamba ni vema hata Rais wetu akajipa muda wa kuangalia viongozi wasomi wenye kukabiliana na changamoto badala ya wasomi wenye vyeti vingi.

Kama ni mfuatiliaji wa mambo ya kisiasa na kiuchumi, utabaini mambo mengi yanayokinzana na dhana ya usomi na utatuzi wa migogoro ndani ya Taifa letu, utakubaliana nami kwamba jukwaa la kisiasa halitumiki na wasomi wa changamoto bali linatumika na wasomi wa kukariri na ambao hawawezi kufikiri kwa siku moja mbele zaidi.

Siku za hivi karibuni, kumeibuka sakata la sukari. Wanasiasa wamelibeba suala la sukari kuwa ajenda kubwa sana ambayo kimsingi ilitakiwa ifanywe na vyombo vya dola, kwao hao wasomi wa siasa na uchumi wamelivalia njuga kama vile nchi ina mgogoro mmoja tu wa sukari, wameviona vyombo vya dola vinavyoshughulika na sukari kama ni kambi nyingine ya siasa badala ya uwajibikaji wao.

Sikatai katika kutoa mawazo lakini nakataa katika kusimamia jambo dogo na kuliona kama ni la msingi, ambalo linapaswa kujadiliwa na kuikosoa Serikali iliyopo madarakani kwa kutumia vyombo vyake vya dola katika kudhibiti uhuni unaotokana na watu wachache kutengeneza mazingira ya maisha ya kisanii.

Wapambe wameshika mabango kulalamika utendaji wa Serikali badala ya kushika bango kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali, wapo wanasiasa wanaodhani siasa ni ubishi wa kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali, wengine siyo wanasiasa ni makanjanja wa uchambuzi wa masuala ya uchumi. Wanajaribu kupinga mambo kwa mtazamo wao na matatizo yanayowakabili sanjari na njaa zao.

Wapo wanaohoji ujenzi wa barabara kama vile siyo jambo muhimu, wapo wanaohoji kwanini Rais hasafiri kwenda nje ya nchi, wapo wanaohoji juu ya rushwa na kudai hadharani kwamba haiwezekani Tanzania ikawepo bila rushwa.

Wapo wanaotaka Rais wa nchi yetu awe anawasikiliza wafanyabiashara ili Taifa liweze kununulika kiurahisi, wapo wanaohoji utumishi wa umma kuingiliwa kana kwamba waliopo ni wafalme wa kurithishwa, nahofu mageuzi ya kimabadiliko ambayo yalikuwa yakitafutwa yalikuwa ni yepi ama kuliangamiza Taifa letu ni kutafuta madaraka.

Nina kila sababu ya kuamini kuwa kila anayesema juu ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni mbovu, basi ana tatizo katika mfumo wake wa kufikiria mambo kwa kina, vinginevyo muda mfupi heshima itarudi. Wanaoweweseka ni wale wachache, wezi, sisi tunaunga mkono juhudi zote.

 

Wassalaam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

921 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!