Kuna wakati huwa najiuliza, ni wapi ambapo tulikosea hii nchi yetu? Nchi iliyokuwa ya asali na maziwa katika uzalendo, maadili, uaminifu, utamaduni, mapenzi, upendo na mengineyo mengi tu.

Najiuliza tuko wapi tulio hai mpaka leo na tunaojua ukweli wa asili ya nchi yetu iliyotukuka? Najiuliza tumefikia hapa kwa sababu gani?

Kuna wakati nikiamka asubuhi naona kama dunia inakwenda kasi sana, siamini kama yale ya jana ndiyo ya leo, na inapofika jioni naona ni kama karne ya miaka imepita, kasi hiyo inanifanya nibaki nyuma sana kimaendeleo na kifikra, kasi hiyo inanifanya nijione mfu ninayetembea, najiuliza hiki ni kizazi gani na tunaelekea wapi? 

Wapo watakaoshindwa kunielewa kwa kuwa wana damu changa na uwezo wao wa kufikiri kwa kasi bila kufukia mashimo kunawafanya wajumuike na mbio za dunia yetu, natamani niteremke katika dunia hii lakini kwa kuwa siyo basi au treni inabidi niendelee kuwamo ndani ya safari mpaka kifo kitakaponitenganisha na usafiri huu.

Ninawaza kwa sauti japo najua ni makosa na inawezekana nikatukana kutokana na kuwaza kwa sauti, nawaza hiki kizazi ni kipi? Hakina uhusiano na kile ambacho tulikuwa nacho sisi, au ndiyo kasi ya dunia imewabadilisha hadi wazazi wao, kosa ni la nani? Kutaka kujua kosa la nani ndipo ninapoona naweza nikavunja maadili tena, maana nawaza kwa sauti. 

Hivi kile kizazi cha nidhamu halisi kipo wapi? Ni kweli kwamba wote wamefariki dunia na kupoteza mila na utamaduni ule? Kizazi kile kama bado tupo tumenunuliwa au tumefumbwa macho kimazingara kiasi cha kushindwa kukemea mambo ambayo leo yapo hadharani na yananadiwa waziwazi? 

Sitaki kuamini kabisa kwamba kizazi hiki kimepandikizwa ubongo wa kisasa na sisi tuna ubongo wa kizamani, ambao si ‘hybrid’ kama huu, ubongo wa kupokea mambo ya kijinga badala ya mambo ya maana, ubongo wa kufikiri kiurahisi badala ya kutafakari mambo kwa kina.

Mimi sipendi kujiingiza katika mambo mengi ya kijamii, kiutamaduni na kisiasa, lakini nasikia jinsi ambavyo watu wanachangia na kutoa maoni yao, naona jinsi wanaokwenda kasi na dunia walivyo na mawazo mbadala na yale ya dunia ya polepole.

Nachelea kusema kila kitu ni kama kimepandikizwa katika bongo zetu za kupokea uchafu, hatutaki kufikiri kwa kuumiza bongo zetu, tunapenda mambo mepesi na kuiga mambo ya waliokwenda kasi kuliko sisi, ni kizazi cha kukariri jibu na kuchagua jibu na si kizazi cha kupitia njia ndefu na kuona faida na hasara.

Ni kizazi ambacho kinaishi kwa jambo ambalo limetokea siku hiyo na linapokelewa katika uchanya wake na si uhasi na namna ya kupambana nalo, ni kizazi chenye sababu lukuki chanya za kuhalalisha ubaya kwa kisingizio cha kwenda na wakati, si kizazi cha kukemea tena bali ni kizazi cha mwache na hamsini zake.

Nakumbuka mengi kuanzia katika miziki yetu ya zamani ya waimbaji waliokuwa wakiangalia mazingira tunayoishi, nakumbuka mengi kutoka kwa waigizaji na filamu zetu za miaka ya sitini, nakumbuka mengi kutoka kwa viongozi wetu wa wakati ule, najiuliza, kwani tuliolea taifa hili tulikosea wapi kuacha urithi wetu? Ni kweli tulimpa urithi mtoto wa kambo tusiye na nasaba naye?

Kweli hatusikii hoja za maana kutoka kwa watu wenye weledi zaidi yetu na kuufanyia kazi na badala yake tunatumia fursa hiyo kumfanya mtoa hoja kuwa mpumbavu na sisi kujaza bongo zetu matusi ya nguoni dhidi yake, tunatarajia kweli laana itatuachia kwa ujinga huu? Nachelea kuomba radhi kwa kuwa nawaza kwa sauti tu.

Hivi hiki kizazi cha kuoana watu wa jinsia moja tunapaswa kubaki kimya na kutetea kwamba ni haki? Hiki kizazi cha kubadilisha jinsia tunapaswa kukichekelea? Hiki kizazi cha kushinda katika mitandao na kuchafuana tuna haki ya kukilinda? Hiki kizazi cha ombaomba wenye nguvu na akili timamu tunapaswa kukiheshimu bila kukikemea? Hiki kizazi cha kuongea tu mbele za watu bila haya na kuwachafua watu wengine kwa kigezo cha demokrasia ni cha kukiacha kitutafune?

Nawaza kwa sauti tu, sijui tunakwenda wapi, maana tumekuwa bendera fuata upepo unaovuma kwenye mambo ya kijinga.

Mungu tusamehe tulioacha urithi wa hovyo.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo. 

1778 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!