Ni kawaida mali za wadhamini kuuzwa pale ambapo wale waliowadhamini wanaposhindwa kurejesha mikopo. Huwa inauma kwa sababu wakati mwingine mdhamini hakufaidika na mkopo, ila tu aliamua kumsaidia ndugu, rafiki, jamaa ili akope, asonge mbele, ila baadaye inakuja kuwa hivyo.

Suala la msingi huwa ni kujua nini la kufanya hasa kama wewe ni mdhamini na hali hii imekutokea au inaelekea kukutokea. Yapo mengi ya kufanya kisheria, ila hapa nitaeleza mojawapo ambalo ni kufidiwa kwa pesa au kile ambacho umepoteza.  

Aina za udhamini

Kwanza, ni udhamini wa kujidhamini mwenyewe na kuchukua mkopo;  pili, udhamini wa kudhaminiwa na mtu ili uchukue mkopo. Udhamini huu wa pili ni ule unakwenda kuomba mkopo unaambiwa mkopo upo ila inahitajika dhamana/rehani ya nyumba, kiwanja, gari nk, na bahati mbaya wewe hauna lolote katika haya, au unalo lakini halifikii kiwango cha mkopo unaohitaji, hivyo kuhitaji ziada ya dhamana.

Unamfuata rafiki yako unamuomba utumie nyumba, kiwanja, gari lake kama dhamana na anakubali kwa makubaliano ambayo mnayajua nyie wenyewe.

La msingi ni kwamba amekubali mali yake itumike kukudhamini uchukue mkopo. Huu huitwa udhamini wa mtu wa tatu (third party mortgage) na ndio udhamini ambao makala hii inauzungumzia.

Kumdhamini mtu kisheria

Sheria haikatazi kumdhamini mtu. Udhamini wa aina hii unaruhusiwa na si vibaya kufanya hivyo ikiwa unaona itafaa. Kifungu cha 78 cha Sura ya 345, Sheria ya Mikataba kimesema mkataba wa udhamini unaruhusiwa na anayetoa dhamana ataitwa mdhamini, anayedhaminiwa ataitwa mdeni mkuu (principal debtor), na anayepokea dhamana ili atoe hela ataitwa mkopeshaji /mtoa mkopo.

Mikataba ya aina tatu kwenye dhamana

Katika mazingira ya aina hii huweza kupatikana mkataba zaidi ya mmoja. Kwanza, mkataba kati ya mdhamini na yule anayetaka kuchukua mkopo. Hawa zaidi hujadili kiasi gani cha fedha kitakachochukuliwa, je, mdhamini atapata chochote ama la, na mustakabali wa mali iliyowekwa rehani isije ikauzwa.

Pili, ni mkataba kati ya mdhaminiwa/mkopaji na taasisi inayotaka kumkopesha, na tatu ni mkataba kati ya mdhamini na taasisi inayotoa hela. Hawa zaidi watajadili kama kweli amekubali kumdhamini mchukua mkopo, na kama yuko tayari mali yake iwekwe rehani kulinda deni la mtu.

Mkopaji kumfidia mdhamini mali ya mdhamini inapouzwa

Kifungu cha 97, Sura ya 345, Sheria ya Mikataba kinasema kuwa mdhamini ana haki na anastashili kufidiwa/kulipwa (indemnify) na mkopaji pale ambapo amelipa chochote katika mkataba wa udhamini.

Ikiwa dhamana iliyowekwa na mdhamini kumdhamini mkopaji imeuzwa ili kulipia deni, basi maana yake aliyelipa deni ni mdhamini na kwa msingi huo anatakiwa kufidiwa hasara hiyo na mkopaji, yaani yule aliyekuwa amechukua mkopo.

Suala la kufidiwa ni ahadi ya asili (implied promise). Maana yake ni kuwa hata kama makubaliano kati ya mdhamini na mdhaminiwa hayakuzungumza au hawakuahidiana lolote kuhusu kufidiwa, bado kufidiwa ni sharti la lazima.

Kwa hiyo mdhaminiwa hawezi kusema hatukukubaliana/hatukuahidiana hivyo. Iwe walikubaliana hivyo au halikuzungumzwa kabisa wakati wa makubaliano yao, bado kufidiwa ni jambo la asili ambalo halitegemei makubaliano.

Kwa maana hii, kama mkopaji anayo mali nyingine, basi inapaswa kukamatwa na mdhamini ili ifidie hasara. Na mali inayoweza kukamatwa ni pamoja na fedha benki. Halikadhalika haki ya kumshtaki na kupata msaada wa mahakama iko wazi ikiwa ataleta ukorofi.

Please follow and like us:
Pin Share