Yah: Kama mimi ningelikuwa Manumba ama wasaidizi wake?

Sasa hivi napenda nikiri wazi kwamba kama kuna mtu ama wana wakati mgumu wa kuingalia rediocall ama kusikilizi simu zao za mikononi za kikazi na siyo kindugu ama urafiki hawana muda wa kuangalia televisheni na kusikiliza redio basi ni kundi zima la Manumba mwenyewe na hao RCO wake wote, poleni lakini ndio kazi mliochagua kutokana na masomo yenu.

Tanzania ni moja kati ya nchi maskini ambazo sasa zinaitwa  zinazoendelea, tunaendelea kwa mambo mengi sana lakini mambo ya mkato ni zaidi kuliko uhalisia wenyewe na hii inatokana na ukweli kwamba sisi wengi ni maskini ki-mali bali ni matajiri wa  kufikirika na kumiliki dili nyingi ambazo baadhi yake kwa wastani wa asilimia tisini na tano ni tofauti na malengo ya akina Manumba  maRCO na OC-CID  na wasaidizi wao.

 

Nawapa pole lakini pia nawapa lawama na bado nasisitiza waongeze juhudi na kundi la vijana ili kuweza kufikia malengo yao kama ilivyokuwa katika kaulimbiu ya “ TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA”  na iwe “ TANZANIA BILA UHALIFU INAWEZEKANA”  Tanzania bila ukimwi iliwezekana kwa sababu tuliwekeza katika uraghibishi, mafunzo kwa wanaongoneka, kuchukua tahadhari kabla ya hatari, nidhamu, ulevi wa aina zote, na mwisho tukasambaza vitendea kazi kwa juhudi kubwa sana, kila mwananchi alipata silaha ya kutumia katika kupambana na Ukimwi. Kwa ufupi tuliwekeza kiasi cha kutosha.


Suala la ujambazi ni kubwa na hasa katika jamii ambayo ni wavivu mawazo yao ni kutajirika katika kipindi kifupi, kundi hili huwa na mawazo ya kuondokana na umaskini katika kipindi cha robo, nusu ama saa kadhaa na siyo kipindi kifupi cha serikali miaka mitano. Hili ndilo kundi ambalo tumemkabidhi Manumba aweze kutoa ushauri nasaha na kupambana nao ili Tanzania bila uhalifu iwezekane.


Mimi ni mmoja kati ya watu wachache ninayekerwa sana na wahalifu, nakerwa na wahalifu kwa sababu nyingi kwanza siamini katika maisha ya utajiri wa haraka lakini pia malezi yangu yanapingana na tendo la uhalifu, hivyo kila ninapoona uhalifu lawama zangu nazipeleka kwa Manumba na wenzake wote.


Naweza nikaulizwa kwanini Manumba na siyo IGP, ukweli uko palepale kwamba kuna usalama wa raia na vitisho na uhalifu dhidi ya raia na mali zao katika hali ya uficho, haya mambo mawili tofauti ambayo wengi wetu hatuyaoni kiurahisi tunadhani kila jambo ni la kundi zima la polisi, polisi kwa ujumla wao wana mgawanyo wa majukumu ya nje na ndani.


Zamani tukiwa vijana tulikuwa na amani sana, Tanzania  hatukuona umuhimu wa polisi, tulijengewa mazingira ya uzalendo uliofanya hata mimi nifanye kazi ya akina Manumba bila kuajiriwa, na polisi walitoa  msaada na kufanikisha kutokomeza uhalifu kiurahisi sana, Tanzania ya leo siyo yetu ni Tanzania nyingine ya kila mtu afe kivyake katika kufanikiwa maisha ama kujitetea dhidi ya uhalifu na hatujawekeza katika hilo bado tunabungua bongo na kufanya utafiti wa kisiasa ili tuamue kuwekeza katika amani kwa kuwawezesha hao akina Manumba.


Tumeona jinsi ambavyo hali ilivyo hivi sasa, kuna vikundi vingi  vya majambazi ambavyo vinaweza vikawachanganya tuliowapa dhamana ya kupambana na ujambazi, mara leo wako huku na dili hili na kesho kule na dili nyingine, akina Manumba wanapofikiria ubomoaji wa mabohari wao wako katika utekaji nyara, akina Manumba watakaporudi na kujipanga na utekaji nyara wenyewe wako West Gate Mall, watakapoenda West Gate kwa kasi watawakosa kwa kuwa wao watakuwa wako benki wakichukua hela kama zao, lazima uwe kichaa, na ili uende na wakati lazima rediocall ikae mbele unasikiliza huku ukiitazama.


Nawapa lawama kwa kuwa hawajawahi kulalamika ili waweze kuwezeshwa kama tulivyowezesha mambo mengine ambayo yameamriwa kisiasa tu kwa manufaa ya watu wachache, Manumba  mimi kama mzee nakulaumu kwa kuwa umekubali kupokea jukumu ambalo unapigana nalo kwa nguvu yako ya Mwenyezi Mungu lakini si kuwezeshwa kitekinolojia kama ilivyo katika nchi zingine.


Hakuna taifa lolote duniani lililoendelea huku likiwa halina amani ndani na siyo mipakani, kwa hali tuliyonayo ni mbaya ujambazi na uhalifu mpya wa kitekinolojia umekithiri, msaada wa mafunzo na kifedha unatakiwa tuwekeze katika jeshi letu, Ukimwi ulikuwa unauwa taratibu lakini majambazi, magaidi, mateja, waporaji ni sekunde, hebu serikali angalieni upya vipaumbele.


Nawaonea huruma sana hao ma RCO, OC-CID na vijana wao kwa kazi nzito isiyo na msaada kutoka kwa raia, nawaonea huruma kwa kukaa na hayo marediocall mbele yenu mkisikiliza nini kipya ambacho hamkujipanga kinatokea na jinsi gani mkabiliane nacho.


Kwa ufupi WestGate yetu bado, kidnap inanukia, ugaidi huo waja na mkwaja wake lakini nyie ndio walewale na nguvu ya Mwenyezi Mungu. Naomba nikemee shetani huyo kwa majina yote yenye nguvu ili mshinde vinginevyo mambo siyo mambo, muziki mkubwa wanangu unakuja, tujipange kucheza uhalifu ni ajira mpya inayokuwa kila siku.

Wasalaam

Mzee Zuzu

Kipatimo.