Nakumbuka mwaka 1995 niliingia katika kinyang’anyiro cha ubunge, lakini katu sitataja jimbo husika kwa sababu za kiusalama, na nimeamua kugombea tena mwaka 2015 insha’allah Mwenyezi Mungu akinipa uhai na afya njema.

Nilibwagwa vibaya sana kwa sababu kubwa mbili za kisiasa – sababu ambazo hazitambuliwi mahala popote katika ulimwengu wa siasa, zaidi ya jimboni kwangu ambako nilikuwa nagombea.

 

Sababu ya kwanza ilikuwa sina fedha za kuwagawia wajumbe ambao ndiyo wanaopendekeza jina langu ili liende katika orodha ya wagombea ili niingie katika mchakato. Sababu ya pili nilivishwa madhambi mengi ambayo sikuweza kuyakataa kwa sababu walionivisha walitumia nguåvu ya fedha katika kuiaminisha jamii inayonizunguka.

 

Mwaka wa uchaguzi ujao nimejiandaa ipasavyo kutokana na uzoefu nilioupata mwaka 1995. Nimejiandaa kwa fedha kidogo za kuwaachia wajumbe baada ya kuuza shamba langu hapa Kipatimo kwa mwekezaji ambaye sijui ametoka wapi na anataka kufanya nini, na nimejiandaa kwa mambo mawili; la kwanza kujisafisha kwa fedha na la pili kuwachafua ipasavyo wagombea wenzangu.

 

Nimefikia hatua hii baada ya kuona huku kunakoitwa Tanzania sasa kunatosha kwa shida zake, nataka niende Tanzania nyingine ya pepo, maana kugaagaa na upwa kumefikia tamati sipati hata dagaa, ni afadhali nitende dhambi kwa kuwaongopea wapiga kura kwa wananchi ili nipate fursa ya kubadilisha maisha yangu kwa sasa ninapoelekea katika kifo changu, maana sina hakika na pepo nyingine.

 

Leo nimeliangalia hili baada ya kusikiliza midahalo mingi ya kujiandaa na kuingia katika uchaguzi ujao wa awamu nyingine, na jinsi wanaotarajia kuwania nafasi hizo wanavyovutana katika vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na pengine kuwauma watu masikio ya unafiki na uchochezi. Si muumini sana wa dini yoyote lakini pia si mpagani kwamba nashindwa kutambua dhambi yoyote. Utambuzi wa dhambi upo moyoni mwangu hasa ninapoona jambo ambalo nahisi haliswihi kwa mtu mwingine, kwa maana ya kumtesa – iwe kwa mawazo au moyoni mwake.

 

Hivi sasa yapo makundi ambayo yanajua kuwa nitagombea ubunge, yanafanya kila linalowezekana usiku na mchana kunichafua kuwa ni mlarushwa, nimejilimbikizia mali, mimi tajiri wa kupindukia, mchawi, natumia majukwaa ya kanisa na misikiti kujinadi, sifai kwa sababu mwaka 1995 nilikataliwa na wajumbe, sina mvuto kwa chama change, na kadhalika.

 

Hizo ni hoja ambazo naziona hazina mashiko na ni hoja za kunichafua na unafiki, pengine zinafanywa hivyo ili wao waonekane wasafi na wapate fursa nyingine ya kuendelea kuongoza hata kama matatizo yao na migogoro yao iko hadharani; na inajulikana isipokuwa inafichwa kwa vigezo vyao vya kujiona watakatifu.

 

Napenda sana msemo wa zamani wa wazee wetu kwamba mke mzuri usimtafute siku ya sikukuu, kwani kila mmoja atajitahidi kuwa msafi na kuongeza manukato, Mtafute siku ya kawaida na ikiwezekana mtafute akiwa shambani akifanya kazi uone umahiri wake, lakini pia ni bora zaidi akiwa hajui kuwa anachunguzwa kwa ajili ya kuposwa. Hilo litamfanya ashindwe kuficha uvivu wake na umbeyaumbeya wake.

 

Naandika barua hii kwenu, ili kwa kina mfanye tafakari bainifu ya kujua mkweli ni yupi. Yupo anayesimama kila siku jimboni kwangu akinichafua kwa hoja zake ambazo katu sizijibu nanyamaza kimya ili wananchi wachambue pumba na mchele, waangalie uwajibikaji wangu wa moja kwa moja katika jamii na hoja zao za kuitwa tajiri, wathibitishe uchawi wangu na yote waliyosema kabla ya uchaguzi kufanyika.

 

Najua yatasemwa mengi, lakini mkweli siku zote atachukiwa mbele ya wanafiki. Mimi sijatangaza nia ya kugombea ubunge lakini sielewi kwanini wananchi wanaambiwa maovu yangu kana kwamba wametumwa wakanisemee. Hakuna aliyethibitisha maovu yangu na kama yupo kuna kila njia ya kunitakasa ama nipelekwe mahakamani nikashitakiwe nifungwe, ama kwa mganga mkubwa nikatolewe uchawi wangu.

 

Swali langu la msingi ni kwanini mtu achukiwe kiuongozi na wachukiaji wawe viongozi wenyewe? Tujiulize sisi wapiga kura kabla ya kuwakubali hao wanaonadi sera zao huku tukijua hawana jipya lolote walilofanya katika kipindi ambacho wameweza kutuongoza katika jimbo letu.

 

Mtu mwenye akili nzuri na malengo mazuri hazungumzii mambo ya watu. Atazungumzia mambo  yanayowakabili watu, hatatafuta sababu za kupendwa kwa kumchafua mwenzake, hatazungumzia majina atazungumzia matatizo ya jimbo letu, hatazungumzia mambo yanayofanywa na mwenzake atazungumzia anayofanya yeye ili tuyaone na mwisho ataingia katika kinyang’anyiro bila hofu ya mtu kwa kuwa tayari amefanya jambo zuri.

 

Nawasihi wanajimbo wajiulize hao wanatafuta nini jimboni wakati uchaguzi bado? Kwanini wasinichukulie hatua za kinidhamu wakati wapo madarakani? Wana wasiwasi gani nikichukua fomu? Lakini bila hofu natangaza rasmi kuwa fomu ya ubunge nitachukua na nitaingia madarakani kwa kazi yangu nzuri, ambayo wanajimbo mnapaswa kujiuliza maswali machache nitakayoyasema kabla ya uchaguzi.


Kidumu chama chetu,

TANU oyeeee!

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


By Jamhuri