Absalom Kibanda, mmoja wa wanahabari mahiri katika Taifa letu, mara zote amekuwa hasiti kunitaja kama “mwalimu” wake.

Naam, mara zote amenipa heshima hiyo bila kujali kuwa ananizidi umri. Ualimu wangu kwa Kibanda unatokana na ukweli kwamba mwaka 1998, wakati huo tukiwa katika Kampuni ya Habari Corporation, na wakati huo nikiwa Naibu Mhariri wa Gazeti la Rai, nilipewa kazi ya wiki mbili ya kuhakikisha nampa mafunzo ya kuripoti habari za Bunge.

 

Tangu wakati huo, Kibanda amenitambua kama mwalimu wake. Lakini si hivyo tu, bali hata alipoingia katika chumba cha habari, bado alihitaji msaada wangu na wanahabari wenzangu, kujua hili na lile ili aweze kutekeleza vema kazi ya uandishi anayoipenda kwa dhati.

 

Kibanda si mnafiki. Hii ni moja ya sifa nzuri za mwanahabari huyu. Pengine ni kutokana na sifa hiyo, tangu tufahamiane karibu miaka 20 iliyopita, tumeendelea kuwa marafiki. Mara zote amekuwa hasiti kuweka bayana kile anachokiamini.

 

Katika jamii hii inayotaka watu wanafiki, waongo, wazandiki na wanaojipendekeza, hii inaweza kuwa moja ya sababu za kujeruhiwa kwake.


Kujeruhiwa kwa Kibanda, kukijumuishwa na matukio mengine ya kuuawa kwa wanahabari akiwamo Daudi Mwangosi na wengine kadhaa, kunaibua hofu kubwa miongoni mwa jamii. Huu ni mwanzo. Bado mengi yanakuja.


Matukio haya yamelenga kupunguza kasi ya waandishi wa habari na wanaharakati waliojiweka mstari wa mbele kuhakikisha tunakuwa na Taifa la watu wanaokosoana.

 

Kuumizwa kwa Kibanda, kukiunganishwa na kuuawa kwa Mwangosi, ni matukio yaliyotawala vyombo vya habari. Kuna kina Mwangosi na kina Kibanda wengi sana ambao wanauawa na kujeruhiwa kila siku, lakini pengine kwa kuwa hawana fursa kwenye vyombo vya habari, ndiyo maana taarifa zao zimekuwa hazivumi.

 

Ndugu zangu, kwa sasa Taifa letu lipo njiapanda, hasa upande huu wa usalama wa raia na mali zao. Matukio ya mauaji na kujeruhiwa, yanaongezeka. Mara kadhaa vyombo vya dola – Polisi na Usalama wa Taifa – wamehusishwa. Kwanini wanahusishwa? Wanahusishwa kwa sababu rekodi za baadhi yao si nzuri.


Mamia ya Watanzania wanauawa au kujeruhiwa kila mwaka kwa staili hii hii ya Mwangosi na Kibanda. Kuna idadi kubwa ya Watanzania waliopata ulemavu kwa njia hii.

 

Taifa letu lilipata sifa kubwa mbele ya jumuiya ya kimataifa kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu miongoni mwa wananchi. Kwa miaka ya karibuni, sifa hiyo inaporomoka kwa kasi mithili ya theluji iliyopashwa moto.


Mauaji ya wanahabari, mauaji ya wananchi wasio na hatia, mauaji ya kidini, mauaji ya albino, mauaji ya vikongwe, ajali za barabarani, ujambazi na matukio mengine mabaya sasa ndiyo yanayoipamba Tanzania.


Kwanini haya mambo yatokee ilhali sote tuliishi kama watoto wa familia moja? Kwanini yatokee kwa watu tulioitana “ndugu”? Je, yanatokea kwa sababu za kisiasa? Kama ndivyo, kwanini tuliridhia kuwa na mfumo wa siasa za ushindani? Ule utu wa binadamu kwa binadamu mwenzake tumeutupa wapi? Kwanini tukose huruma ya kutambua kuwa huyu anayeumizwa au kuuawa ana wategemezi? Binadamu tunakosaje utu kwa binadamu wenzetu ilhali hata simba hawezi kumla simba mwenzake?

 

Watanzania turejeshe upendo uliokuwapo miaka iliyopita. Tutambue na tuheshimu thamani ya maisha ya binadamu wenzetu. Turejee maandiko ya vitabu vyote vitakatifu ambayo yanasisitiza upendo na mshikamano.


Tofauti zetu za kiitikadi, kiimani na kimtazamo sizituondoe kwenye misingi ya utu na upendo. Tushirikiane kuirejesha Tanzania kwenye kundi la mataifa ambayo kila binadamu atapenda kuja kuishi kwa raha mustarehe.

 

Kwa mara nyingine, naungana na wapenda amani wote kumwombea Kibanda. Apone haraka, arejee kwenye dhima yake habari. Tukio hili linatisha, lakini ukweli ni kwamba kujeruhiwa au kuuawa kwa askari vitani si sababu ya kuwafanya wapiganaji na makamanda wengine kurudi nyuma.


Woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote katika mapambano ya kuijenga jamii iliyo huru na inayozingatia haki.

Please follow and like us:
Pin Share