Inawezekana wengi wetu tulikuwa hatukuelewi wakati wa kampeni zako za kuutaka urais. Kuna wakati ulisema kabisa unataka kulala mbele na wapiga dili, sisi kwa umbumbumbu wetu tulidhani ni dili za mafisadi na siyo sisi wapiga dili ndogondogo.

Baada ya kuapishwa, tulianza kuona mabadiliko ya uongozi katika ngazi mbalimbali. Ulianza kuwabadilisha mabosi wetu wengi ambao sisi tulikuwa tukiwategemea kwa kipato cha hapana pale, tulikuwa tunafanya kazi nje ya ofisi nyingi lakini kama waajiriwa.

Mabosi wetu uliwaita majipu ukawatumbua na wengine ukawahamisha na kuziba mianya, bila wewe kujua ukaanza kutufukuzisha kazi za ajira ya nje, tuliokuwa madereva wa michepuko tukapaki magari, tuliokuwa madalali wa mambo ya wakubwa tukakaa vijiweni bila kazi, na kila jioni mabosi walikuwa hawatoki tena kuvinjari na sisi na kutuachia posho kama zamani.

Majiko mengi ya wapambe huko mitaani yakaanza kununa. Hali za familia zikaanza kutetereka, wake zao wakaanza kuondoka na michepuko ikaingia mitini, hela za dili zikapotea na msururu wa wapambe na familia, hotuba zako zikaanza kujirudia vichwani ukinadi sera za kiuchumi na kufanya kazi, ‘hapa kazi tu’.

Mheshimiwa Rais, kama ungetuambia mapema kwamba unataka tufanye kazi halali, naamini wachache sana tusingekuchagua, ungechaguliwa na wengi wapenda hakina wachapa kazi, kwa kukuchagua umeua ajira yetu na wategemezi wetu wanakula kwa macho, hali ya uchumi kwa sisi wapiga dili imedorora sana kiasi cha kutia aibu kwa jamii inayotuzunguka.

Ukiwauliza majirani zetu leo, wale majirani ambao walikuwa wanatuona tukifaidi maisha miaka ya nyuma wanaweza kuwa wanatucheka, hatuendi tena katika yale maduka makubwa na kujaza bidhaa katika matoroli, leo tunasifia mabasi ya mwendo wa haraka kuliko magari yetu tuliyopaki nje ya majumba yetu ya kifahari.

Leo tunagombana na wauza mkaa huku mtaani, hawaweki lumbesa ambacho tunadhani ndicho kipimo halali, leo umeme nao tunahisi unaisha upesi tunagombana na watoto, kwa hiyo tunaamua kununua wenyewe kubana matumizi lakini bado unaisha upesi, kwa hiyo tumeamua kuzima taa za nje na kuilalamikia Serikali kupunguza bei ya nishati hiyo.

Maisha yamekuwa magumu, madeni yameongezeka, dili zote zimepotea, sasa hivi kila kitu ni lazima atoke jasho, wapo wengi ambao wanaona maisha ni mazuri sasa hivi kwa kuwa walikuwa wanaishi kwa hali hiyo miaka yote ya nyuma, walikuwa na kipato kiduchu na waliweza kukitumia kwa ufasaha wakati huo.

Hawa ndiyo wale ambao walikuwa wakitupita baa na kutupungia mikono tukipiga mambo yetu, hawa ndiyo waliokuwa wakipita katika mapipa ya takataka na kuokota masalia ya vyakula na vinywaji tulivyosaza, hawa ndiyo ambao walikuwa wakiomba misaada mbalimbali ya kijamii mitaani, hawa ndiyo tuliokuwa tukiwafanya sungusungu wakati sisi tukiwa tumelala.

Sasa hivi hali ni mbaya, tunafuatilia bei za bidhaa bila shuruti, tunafuatilia chenji zetu na kudai risiti, hali ni mbaya tumepunguza matumizi yasiyo ya lazima, hali ni mbaya tumeamua kufanya mazoezi kila jioni, hali ni mbaya tunadhibiti vyakula vya makopo na tunatumia zaidi vyakula vya asili.

Hali ni mbaya kwa Serikali kuamua kudhibiti matumizi na kuifanya Serikali kukuza uchumi wake vizuri, mambo ya mtu kati yamekatwa sasa ni mtu kwa mtu, hoteli zilizozowea kulisha watu wa Serikali na tukapata asilimia kumi hazifanyi kazi tena.

Hivi tutaishije kama siyo kuamua kwenda kulima kijijini ambako tumetanguliza familia zetu? Napenda kushauri tu kama inawezeka na tuachiwe japo mlango mmoja wa kupiga dili kwa kuwa nchi hii pia ni yetu wapiga dili si ya hao wenye umasikini wao. 

Mheshimiwa Rais Magufuli, acha kutukatia mipenyo yote ya hela za dili, tutakufa njaa maana wizi tutachomwa moto.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri