Yah : Mkiamua mnaweza lakini hamuamui Hongereni

Wanangu leo ni siku nyingine ya Jumanne katika wiki hii ambayo ni nadra sana kuifikia, kama hujui kwamba kesho ni mtihani mkubwa kwako kutokana na siri kubwa aliyonayo Mwenyezi Mungu juu yako, ni yule ambaye siyo muumini wa dini yoyote ndiyo anaweza kuwa kichaa asijue hilo.

Nimefarijika sana na demokrasia ambayo inaendelea hapa nchini kwa mambo ambayo kama siyo kigezo yanaweza yakatutoa siku moja hapa tulipo na kutupeleka kule tutakapo kwa nia njema na ya dhati kutoka kwa hao waitwao watawala wenye nia njema ya maendeleo.


Niliwahi kusema kwamba sisi tuliozaliwa zamani tuna matatizo mengi, mosi tuna mawazo ya zamani sana pili hatutaki kubadilika kwenda na wakati wa dotcom, hili tunalijua lakini wakati mwingine tuna maana kubwa ya kutobadilika kutokana na kile tunachokiamini katika ukweli. Tulikuwa na kaulimbiu ya kuwa nitasema kweli uwongo kwangu mwiko kidumu chama chetu.

 

Wanangu naamini  baada ya  kupumzika majumbani na kutafakari maisha yenu ya miaka ijayo na hatima ya kizazi chenu cha dotcom, sina hakika baada ya miaka michache ijayo baada ya dotcom kuzeeka sijui kutakuwa na kizazi gani? Najiuliza ni teknolojia gani mpya itakayokuwepo itakayowafanya nyie kupitwa na wakati, nahisi wakati huo tunaweza tukawa tumebadilishana mavazi, kwamba ya kiume yanavaliwa na wanawake na ya wanawake yanavaliwa na wanaume, e mola naomba nisishuhudie hilo, niwe mahala pema peponi.


Wanangu kuna wakati huwa napata fursa ya kuangalia hizo ziitwazo televisheni, huwa naona sinema za maendeleo, naona mambo ya kufikirika, huwa naona picha za watoto, vita, taarifa za habari zilizojaa mambo ya ajabu ajabu kama ugomvi wa kung’ang’ania  maiti, masuala ya ugomvi wa kidini, ajali za kizembe zilizopoteza mamia ya watu, kufukuzwa kwa wananchi maeneo ambayo wameishi kwa miongo zaidi ya mitano nakadhalika.


Mambo haya huwa yananikera na kunifanya nifikirie mambo yote ya zamani, huwa najidharau kwa kigezo cha uzee lakini bado naamini uzee ni dawa na kwamba inawezekana nayosema yakawa na tija kwenu kizazi cha dotcom.


Haya ni mawazo yangu ya kizee na wala hayahusiani na mpango kazi wa kizazi kipya cha sasa na maendeleo yaliyofikiwa kwa kasi kubwa katika kipindi kifupi cha miaka hamsini ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika ya Ujamaa na Kujitegemea kiukweli, Tanganyika iliyokuwa na kaulimbiu za Uhuru na kazi, uhuru na umoja, zidumu fikra za mwenyekiti, ujamaa oyee!.

 

Nahisi kuzidiwa fikra pevu za kisasa na maendeleo yaliyopo ambayo yanakinzana na fikra zetu za kijinga juu ya Siasa ni Kilimo, Ujamaa na Kujitegemea na kuukataa Unyonyaji, Ubeberu, Ukupe na Ukabaila.


Wanangu naandika barua hii ya leo si kwa sababu nimetoka usingizini na nina mawengewenge, hapana, lakini naamini nanyi huko mliko iwe mjini au karibu na Kipatimo mmeshuhudia wataalamu wenye vipaji vya ajabu waliomo katika jamii yetu iliyogubikwa na matatizo mengi yanayoweza kutatulika kiurahisi na kundi hili lililopo.


Hapa Kipatimo kuna wakazi wengi ambao tulihamishiwa tangu mwaka 1974 wakati wa oparesheni vijiji vya ujamaa, wengi wetu hatukuwahi kupata maradhi ya kutisha, yawezekana ilikuwa hivyo kwa sababu nyingi, ubora wa huduma za jamii kama maji salama, utunzaji wa mazingira kwa wakati wetu na kadhalilika.


Nasema mkiamua mnaweza lakini hamuamui, hongereni. Mmeamua kuacha misingi ya Utawala Uora, Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha, mmeamua kuacha kuheshimu mali za umma, maadili ya viongozi, kanuni zetu za TANU vilivyowezesha taifa hili likiwa na amani na utengamano.


Hivi sasa kuna kufuru nyingi sana, kuna wizi uliokubuhu, kuna kujilimbikizia madaraka, kuna undugunaizesheni katika kuliongoza taifa ambalo katu siyo la kifalme, kuna uvivu wa kupindukia, kuna idadi kubwa ya wanasiasa badala ya wanataaluma, kuna wezi wengi kuliko waaminifu, ukweli hamjaamua mchukue hatua gani, kitendo cha kubaki kimya nacho pia ni uamuzi hongereni.


Taifa lolote lenye kuamini katika ujinga wa mitishamba litaangamia kwa uzembe wa wachache na ndio maana leo hii taarifa zetu za habari zinazungumzia mauaji ya kutisha ya vikongwe, mauaji ya albino, mauaji ya watoto lakini kwa kuwa hamjaamua bado nawapa kongole siku mtakayochukua hatua thabiti za kukabiliana na ujinga huu.


Ukimya huu maana yake ni kuhalalisha kilichopo mbele yetu katika mabango tuamini kuwa dawa ya Ukimwi ipo wakati dunia nzima inajua kuwa tiba hiyo haijapatikana, tuamini kuwa bila uganga huwezi kuwa tajiri na kwamba kuuana kwa imani za kishirikina iwe ni suluhisho la mmojawapo kufanikiwa katika maisha ni hawa wenye vibali kutoka serikalini na wenye mabango ambayo hata waziri wa biashara anayaona na kuyabariki yaendelee kuwepo bila kukemea.


Nasema tena ni wataalaamu hao hao ndio wanaoweka matangazo kuwa hata kazi za siasa unaweza ukazipata kama utapita kwao, utapata kazi yoyote iwe udiwani, ubunge, uwaziri nakadhalika hata kama hujui kusoma wala kuandika, tumeruhusu wawepo, waishi watajirike kupitia vipato vya watanzania wasio na kazi.


Ni nyie wenyewe wanangu ambao mmekubali matangazo ya kutisha kwa jamii ambayo sasa ilitakiwa iwe imestaarabika kupingana na imani ya utamaduni usioshikika kwa kuruhusu kuyaona matangazo hayo katika magazeti, redio na televisheni zenu.


Naandika barua hii kwa mara ya kwanza kwenu ili mjiulize, hivi kaulimbiu yenu ina akisi tunchokiona? Kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana kwa kutumia mbinu hii ya wataalamu kutoka Sumbawanga na huko Nigeria? Vipi kuhusu hawa wadogo ambao nao wameweka matangazo yao mbele ya nyumba za akina Mzee Zuzu na wengine? Vipi kuhusu njia panda na matangazo yao?


Pamoja na kwamba Mzee Zuzu nimezaliwa zamani lakini nilipata fursa ya kuajiriwa kwa kupata elimu ya kisomo cha watu wazima hadi hatua ya nne, niliajiriwa EAC, mgodi wa mawe Isanga, ujenzi wa mapomoko ya Hale, ujenzi wa barabara ya Dar-Tunduma, ujenzi wa kiwanda cha UFI na miaka kadhaa kabla ya Uhuru nilishiriki ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Pugu.


Pamoja na umri wangu na kufanya kazi sehemu zote hizo hatukupata kuamini katika ushirikina ambao leo naona umepata baraka kutoka katika vyombo vya dola, mimi nauona kama ni wizi wa macho na mchana ambao umepata baraka kutoka kwa viongozi wetu.


Kama ni bishara halali basi tuambiwe kwa vile nami naweza kuwa na ujanja wa kufungua ofisi na kutibu maradhi kama kipindupindu, mafua, kuzuia mafuriko mabondeni, kupunguza matumizi ya mafuta ya gari na umeme, dawa ya kupata urais, kujua kutumia kompyuta bila kusomea, kuongea kiingereza kwa dozi ya kikombe kimoja tu kwa siku moja.


Toeni uamuzi na amuaeni lakini pia kubaki kimya ni uamuzi hongereni.

Wasalaam

Mzee Zuzu

Kipatimo