Nianze na salamu japo si lazima sana kwa kizazi hiki chenye akili nyingi zisizokuwa na matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa lao, najua nitalaumiwa sana kwa kauli yangu lakini ni heri ya nusu shari kuliko shari kamili, nimeamua kusema ili nisemwe lakini ujumbe ufike.

Taifa letu limekumbwa na wimbi kubwa la vijana wenye misimamo ya kisiasa bila kujua hatima ya siasa wanayosogoa kila siku, kwa ufupi wana nguvu ya hoja kuwa na nguvu ya haja, wanaweza kuwa na hoja lakini hoja yao inalazimishwa na haja waliyonayo, naipenda siasa lakini inapofikia kiwango hiki siasa inakuwa mzigo kwa wenye kupenda maendeleo.

Nimeamua kushika kalamu kuwaandikia waraka huu kwa sababu nyingi, nitazisema chache kwa heshima ya umri wangu ili niweze kumaliza ngwe yangu vizuri bila kumwagiwa sifa mbaya kutoka kwa wanasiasa. Kwanza siasa ni mfumo ambao unalenga kukubalika na jamii yoyote, haulengi kuwafukuza watu kutoka katika mfumo wa muungano wa mawazo, hili ni bora watu wengi wakaelewa ili tuwe pamoja katika waraka wangu.

Wakati nikisoma ‘mido skulu’ (middle school) niliambiwa siasa ni uwezo wa kuwashawishi watu kuishi katika mfumo ambao wao wamekubaliana kiutamaduni, maendeleo, usalama, kiuchumi na kiuongozi. Niliiona maana hiyo kwa kiwango changu cha elimu wakati huo na ninajaribu kuihusisha maana hiyo na mfumo wa maisha tuliyonayo leo katika ulimwengu huu wa wingi wa demokrasia na siasa.

Leo ni vema nikajikita na mambo ambayo nayaona katika maisha ya kisiasa tuyaishiyo kama Watanzania kwa umoja wetu, tuna siasa ambazo bado sijajua kama zinatofauti na ile maana ambayo nilifundishwa, sitaki kulazimisha maana ile ibaki kuwa ile lakini nataka kuhoji uhalali wa siasa ya usasa na hatima ya taifa katika kuchagua mfumo wa siasa.

Hivi sasa kumuona mwanasiasa ambaye kazi yake ni kutukana wananchi ni jambo la kawaida, kuzisikia siasa za maji taka ni jambo la kawaida, hatuzungumzii sera wala mipango ya maendeleo itokanayo na siasa yetu, nchi imekuwa na vijana wengi wanaibuka kuwa na vipaji vya siasa za hovyo badala ya kuwa na vijana wenye kuibua mijadala ya maana kwa maana ya maendeleo, usalama, utamaduni na uongozi, najisikia vibaya sana hasa ninapojumuishwa katika uamuzi na matusi yanayotoka vinywani mwao.

Nchi yoyote duniani inaendeshwa kisiasa, lakini haiendeshwi na siasa zaidi ya moja, lakini kwa taifa letu tumehama kutoka katika siasa ya kuendesha nchi na tumeingia katika siasa za mashindano, kiufupi tunashindana na siasa inayotuongoza na kuipoteza dira ya kumfanya waliyopanga na kuanza kujibu lawama zinazotolewa.

Tatizo kubwa ambalo ninaliona kila siku kwa nchi yetu ni namna ambavyo siasa imegeuka na kuwa kijiwe cha watu wachache kulazimisha walio wengi kuamini kile ambacho wameamua kukiongea bila kuangalia mustakabali wa mafanikio ya siasa hiyo, siasa hizi zipo katika sekta mbalimbali, zipo katika masuala ya kiuchumi na hata katika sekta zingine kama michezo na kadhalika.

Siku za hivi karibuni taifa letu lilishiriki kikamilifu mashindano ya AFCON na matokeo ya mashindano hayo kila mtu anayajua, lakini wameingia wanasiasa wengi sana katika mitaa na vijiweni ukiachilia mbali maeneo rasmi kujadili masuala ya mashindano na kwa nini tumeshindwa.

Wapo waliotoa maoni yao kama wananchi wa kawaida, na wapo waliotoa maoni kama wanasiasa wa michezo na wapo waliotoa kama makocha wa kisiasa, lakini hakuna ambaye ameongelea siasa ya kukuza michezo katika miaka michache ijayo ili tuweze kuvuka japo hatua moja mbele kuliko hii ya makundi.

Nimetumia mfano huu ili tuweze kuangalia mifano mingine katika sekta zingine na jinsi ambavyo siasa imekuwa mkwamo mkubwa kwa maendeleo na utamaduni wetu, tumegeuza siasa kwenye mambo ya msingi ambayo yanahitaji utaalamu na kuchukua hatua, lakini kibaya zaidi wapo wanasiasa ambao kazi yao kubwa ni kukosoa tu lakini hawapo na njia mbadala wala kutoa mawazo ni kama wamekaa kwa ajili ya kukosoa na si kujenga nyumba yetu kwa uzalendo.

Nitumie fursa hii kuwaomba wanasiasa wote wa Tanzania ambao wamejiajiri kuwa wanasiasa wajaribu kufikiria namna ambavyo wataitumia siasa kwa maendeleo ya Watanzania.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

253 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!