Yah: Nimechoka na haki ya sheria!

Yah: Nimechoka na haki ya sheria!

Navuta shuka ambalo ni chakavu sana linaruhusu mbu waingie bila kipingamizi na kuning’ata, natumia dawa mseto kama tiba yangu kila wakati, sasa nimewazoea  mbu kiasi cha kutonifanya nishindwe kupata usingizi mzito.

Nahisi dalili zote za usingizi mzito lakini nawaza juu ya shamba langu la Kipatimo ambalo naona dalili zote za kupata dhuluma kutoka kwa wale wenye nguvu ya kucheza na sheria, usingizi unanichukua ndani ya fikra hizo na ndoto inabeba usiku wangu kwa ndoto hiyo, naanza kuota.

 

“….Huu ni mwaka wa tisa sasa ambapo nadai haki yangu ya shamba ambalo nilipewa kisheria na mamlaka au serikali ya kijiji, ni mwaka wa tisa tukiwa mahakamani lakini ni zaidi ya miaka hiyo tukiwa katika migogoro ya ardhi na hao wenye fedha ambao wameamua kuifanya sheria kama mchezo wa kucheza nao.

 

Niliamua kwenda mahakamani kwa sababu nilijua  kuwa sheria itafuata mkondo na sheria hiyohiyo itatamka kuwa ardhi hiyo ni mali yangu halali na ninaweza kuitumia katika shughuli za kimaendeleo.

 

Mpaka leo ni biashara ya nenda rudi na umri wangu sasa unaanza kukataa baadhi ya mambo, unaanza kukataa kumbukumbu, kutembea, kusikia, kugharamia baadhi ya nyaraka za mahakama, kwenda na wakati na mwisho kukabiliana na taratibu za haraka haraka  za mahakama.

 

Nimefuata sheria zote za kudai eneo langu kwa kipindi chote japokuwa utekelezaji umekuwa katika hali ya utendawili, sielewi hatima yake na ninachelea kusema labda hukumu ya kweli itafanyika baada ya kifo changu kutokea, nachukia haki ya sheria ni vema sheria ingeachwa mikononi labda amani ya umwagaji damu ingetawala.

 

Nahisi  kuwa sina nguvu tena ya kuendelea kudai eneo langu ambalo nimelitumia kwa miaka mingi na likiwa na makaratasi yote ya kijiji changu hadi wenye nguvu ya sheria ama, pesa ama ushirikina walipofika na kuanza kulichukua eneo hili na kulitumia huku wakijua wazi kuwa naishi hapo na ni makazi yangu kama mwanakijiji na wao ni wageni katika kijiji chetu ambacho tumegawana maeneo.

 

Ndoto inaendelea, nakumbuka nilipanda miti ambayo huyu mwekezaji wa kudhulumu ambaye nilimpeleka mahakamani ameamua kukata mbao kwa kinga ya mahakama, anauza eneo langu kwa kosa la sheria kuchelewa kutoa haki, nachukia sana, nawachukia wanaoongoza sheria, nawachukia wanasheria naichukia mahakama.

 

Kichwani naanza kukumbuka baadhi ya silaha zangu zilizopo uchagoni nina mkuki, upinde mishale na mawe kadhaa yenye nyongo ya mamba najiuliza hayawezi kunisaidia katika kudai haki yangu ambayo nigepaswa kupata kupitia sheria zetu?

 

Nakumbuka maneno ya Julius Nyerere aliyosema kuwa haki hainunuliwi, haki ni haki, pasipo na haki kuna uonevu, maskini hawatakuwa na kitu, najigeuza kitandani nagundua kuwa naendelea kuchana shuka langu na umaskini unazidi kunitawala, haki haipatikani…… mwisho wa ndoto.

 

Ninaposhituka  kutoka usingizini nakumbuka kuwa sikuzima redio na kipindi kilichopo hewani ni kutoka bungeni na ninasikia hoja ya kutenganisha mhimili wa Mahakama na Serikali kwa kuwa kila mmoja unajitegemea, najiuliza au ndio maana kesi yangu haiishi kwa sababu hata viongozi wa Serikali wanaingilia uhuru wa mahakama?

 

Sipati jibu kwa kuwa sina hakika na hilo lakini najiuliza bado ndani ya usingizi wa mang’amung’amu kesi yangu itaisha lini ili nipate haki yangu au nikose haki yangu?

Kama ni  kweli  kuna mkono wa mtu katika kesi hii ya shamba tu, huku Kipatimo kuna mikono mingapi katika mikesi yote mikubwa na midogo hapa nchini na nguvu ya mahakimu na majaji iko wapi kama mhimili unaojitegemea?

Mzee Zuzu

Kipatimo.